Saturday, June 4, 2016

MAUAJI HAYA SI BURE , KUNA TATIZO



KARIBU vyombo vyote vya habari hapa nchini, vimeripoti kuhusu mauaji mbalimbali yaliyotokea hapa nchini katika kipindi cha mwezi mmoja. Takribani watu 15 wamepoteza maisha kwa kuuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Katika historia ya nchi yetu, huu ni mfululizo mkubwa zaidi wa mauaji kuwahi kuripotiwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Taarifa hizi hazijapata uzito mkubwa kwa vile tu labda haujahusisha makundi ambayo vyombo vya habari vya kimagharibi vinapenda kuripoti kuhusu.
Kinachosikitisha ni kwamba mauaji hayo yamefanyika kwa njia ya kikatili mno- kwa waliouwa kuchinjwa au kupigwa kwa kutumia silaha za jadi. Kwa tafsiri ya harakaharaka, wauaji ni kama walifanya hivyo kwa kutaka kufikisha ujumbe mahususi kwa jamii au familia husika.
Katika kipindi hichohicho, kumetokea pia tukio la vijana wawili kushiriki kumbaka mwanamke na kisha kusambaza picha za tukio hilo katika mitandao ya kijamii. Haya ni baadhi ya matukio yanayoonyesha kuwa jamii yetu sasa haiku sawa.
Picha ya kwanza tunayoipata ni kwamba sasa hatuko salama tena. Jamii ya Kitanzania iliyokuwa ikifahamika kwa amani, kupendana na kuheshimiana; sasa taratibu inageuka kuwa ya manyang’au.
Imekuaje tumefikia hapa? Je, ni kwa sababu ya aina ya malezi ambayo jamii yetu inayatoa kwa vizazi vyake? Ni kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi? Ni kwa sababu ya ukosefu wa wataalamu wa kisaikolojia ambao wangeweza kubaini matatizo haraka na kuzuia kabla tatizo halijatokea?
Nani anahusika na ulinzi wa roho za Watanzania na mali zao? Inakuaje majambazi yanavunja mlango na kuua watu ambao wanaishi katika maeneo yenye majirani ambao bila shaka walisikia sauti ya kelele za waliouawa? Uko wapi ulinzi wa Sungusungu uliokuwa ukisaidia kulinda mali na maisha ya Watanzania?
Ni lazima tukubali kwamba nchi yetu sasa inapita katika kipindi kigumu. Ni lazima, kama Watanzania, tujiulize ni wapi tunakoelekea. Tujiulize swali hili katika kila ngazi. Kuanzia ngazi ya familia, nyumba za ibada, mitandao ya kijamii na katika kila namna inayoweza kufaa.
Haitoshi tu kusema kwamba ugumu wa maisha, visasi, ushirikina na kushuka kwa maadili ndiyo chanzo cha yote haya. Swali la kujiuliza na kupata majibu yake ni hili; tumefikahe hapa? Tunatokaje?

CHANZO  CHA  HABARI:  GAZETI  LA  RAIA  MWEMA, Na   Mwandishi  Wetu, 01, june, 2016.

No comments:

Post a Comment