Saturday, May 14, 2016

TRUMP AANIKA SERA ZAKE ZA KIGENI


Donald TrumpWASHINGTON, MAREKANI

MGOMBEA urais wa Chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump, ametoa hotuba muhimu kuhusu sera zake za kigeni huku kukiwa na wasiwasi kwamba hana uzoefu wala uelewa wa kutosha kuliongoza taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.
Katika hotuba hiyo, Trump aliahidi kuweka maslahi ya Wamarekani mbele akisema lengo la Marekani litakuwa amani na ufanisi na si vita na maangamizi.
Trump ambaye anapigiwa upatu kushinda tiketi ya chama cha Republican kutokana na kushinda katika majimbo mengi katika chaguzi za mchujo, alitumia muda mwingi katika hotuba yake kuhusu sera zake za kigeni kumponda Rais Barack Obama.
Alisema sera za kigeni za Obama ‘hazikuwa na mbele wala nyuma’ na zimewafanya washirika wa Marekani kupoteza imani na mahasimu kutoiheshimu.
Trump ameahidi kupambana dhidi ya itikadi kali za Kiislamu katika ukanda wa Mashariki ya Kati kwa kuimarisha udhibiti wa kikanda na pia ameahidi kuwa na uhusiano mzuri na Urusi.


CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA,IJUMAA, 29  MAY, 2016.

No comments:

Post a Comment