Wednesday, May 4, 2016

MAHAKAMA YATOA HATI YA KUKAMATWA MEYA KINONDONI


 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imetoa hati ya kukamatwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob akidaiwa kutofika mahakamani.

Meya Jacob anakabiliwa na shtaka la kumshambulia mwandishi wa Habari wa Gazeti la Uhuru, Christopher Lissa na kumsababishia maumivu makali.

Kesi hiyo ililetwa mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa kwa ajili ya kusikilizwa ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na shahidi mmoja.

Wakili wa Serikali Onolina Mushi, alidai mshtakiwa pamoja na wakili wake hawajafika mahakamani hivyo aliiomba mahakama itoe hati ya kukamatwa mshtakiwa na kupanga tarehe nyingine ya kuendelea kusikiliza shauri hilo.

Hakimu Riwa alikubali maombi hayo likiwemo la kutoa hati ya kukamatwa Meya huyo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 23, mwaka huu, kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika kesi hiyo, Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 11,2015 katika maeneo ya Kinondoni, kipindi hicho akiwa Diwani wa Kata ya Ubungo. Ilidaiwa mshtakiwa huyo alimpiga Lissa mateke na ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.

Shtaka la pili ilidaiwa mshtakiwa siku hiyo hiyo kwa makusudi na kinyume cha sheria, aliharibu kamera aina ya Nicon yenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kampuni ya Uhuru Publication Limited.

CHANZO  CHA   HABARI:  GAZETI  LA  MAJIRA, Jumanne, mei  , 2016.

No comments:

Post a Comment