Saturday, May 14, 2016

KARIAKOO MARKET 1949 MOJA YA KITUO CHA HARAKATI ZA SIASA DAR ES SALAAM

Wanamajlis,

Mara nyingi nimekuwa kila nikieleza historia ya TANU na harakati za kudai uhuru nimekuwa nikimtaja Abdulwahid Sykes na Kariakoo Market ambako alikuwa akifanya kazi kama Market Master. 

Soko lenyewe ndilo hilo hapo juu kama lilivyokuwa katika miaka 1950 hadi miaka ya 1970 lilipovunjwa na kujengwa soko hili tulionalo sasa. 

Bahati mbaya huwezi kuona ofisi ya Abdul Sykes lakini mkono wa kulia wa picha hiyo ni Mtaa wa Swahili ukikatizwa na Mtaa wa Tandamti (Mtaa wa Mshume Kiyate). 


Ukiufuata mtaa huo moja kwa moja utakutana na Mtaa wa Mkunguni na ndiyo mwisho wa soko. 



Kushoto ni Mtaa wa Nyamwezi.

Ofisi ya Abdul Sykes ilikuwa katikakati ya Mtaa wa Swahili na Tandamti na Swahili na Mkunguni. 

Hapo ndipo Mwalimu Nyerere alipopelekwa na Abdul na akawa Nyerere akija pale ofisini kwa Abdul kila alipokuja mjini kutoka Pugu. 

Hapo sokoni ndipo Mwalimu Nyerere alipojuana na Shariff Abdallah Attas mmoja wa watu maarufu wa Dar es Salaam enzi zile na mtu aliyekuwa anajua mengi katika historia ya TANU.



Abdul aliuza kadi za kwanza za TANU ndani ya ofisi ile kiasi kwamba iko siku alizozana na Town Clerk Mzungu aliyetaka kujua kwa nini kadi za TANU zinauzwa pale. 

Katika miaka ile ya 1950 mwanzoni hapo palikuwa moja ya vituo vya harakati na kituo kingine kilikuwa Ilala Welfare Centre ofisini kwa Hamza Mwapachu.


Hizi ndizo zilikuwa baadhi ya sehemu za harakati wakati wa mchana. 

Baada ya kazi walikuwa wakikutana Tanga Club New Street na Mkunguni kujiburudisha na kuzungumza siasa.

CHANZO  CHA   TAARIFA :  MOHAMED  SAID  WEBSITE.

No comments:

Post a Comment