Monday, April 25, 2016

UJASIRIAMALI : NI UJASIRI , AU NI KUBAHATISHA ?




KATIKA miaka iliyofuatia Azimio la Arusha, kulikuwa na hekaheka nyingi za kukuza Kiswahili, na mojawapo ilikuwa ni kutayarisha msamiati wa masomo ya sayansi, na kwa upande fulani biashara. Lengo lilikuwa ni kutumika kwa msamiati huo katika kufundisha masomo ambayo yana vitabu vya kufundishia  au vya kitaaluma  vya Kiingereza, ikidhaniwa kuwa vikiandikwa kwa Kiswahili masomo hayo yataelewka zaidi. Hivyo ilianza shughuli ya kujenga misamiati katika maeneo mengi na mengi kati ya maneno yanayotumika sasa yalianza kubuniwa wakati huo.


Hali hiyo haikuondoa hali ya awali kuwa uanzishaji wa maneno mara nyingi unatokana na kudra tu katika mazungumzo na hasa katika uandishi wa riwaya au mashairi, ikatokea kuwa mtu aingize neno jpya. Kwa mfano Mwalimu alileta neno kung'atuka akisema kuwa ni neno la Kizanaki ambalo alilitumia kana kwamba ni Kiswahili, na likabaki hapo. Kuna uwezekano kuwa watungaji wa maneno katika mabaraza rasmi kama BAKITA au TUKI pale Mlimani, au wazungumzaji wengine wenye hadhi hii au ile, watakuwa wameingiza neno ujasiriamali katika msamiati.


Kinachoonekana katika neno hilo ni dhana ya ujasiri, ambayo inaanza kwa kuleta mashaka, kutafuta hasa ujasiri wenyewe uko wapi, kwani maana ya kawaida ya neno ujasiri ni kuthubutu kuingia au kufanya shughuli hatarishi, kutokana na malengo fulani ambayo ni muhimu. Neno ujasiri vile vile linahitaji shughuli hiyo iwe njema kijamii, hivyo ikiwa hatari yoyote itatokea au kutumia, mtu kama hiyo anaitwa shujaa, kwa mfano askari anapokufa vitani. Pale ambapo mtu anafanya shughuli hatarishi isiyo na manufaa kwa jamii, kwa mfano ujambazi, haitwi jasiri.


Kwa maana hiyo aliyetunga neno hilo alikuwa na maana ya kujipongeza kama alikuwa akijizungumzia, au kuwapongeza watu fulani kama alikuwa anawataja kwa maana ya kuthubutu, kudiriki, kujitoa (na siyo kujitoa mhanga, hasha). Kuna undani wa ujasiri unaozungumziwa na pia mpaka wa wazi, kuwa licha ya kuwa anayezungumza anatambua ujasiri huo, asingependa kutia chumvi. Ukivusha dhana hiyo ya ujasiri ikawa ya kina sana, inaanza kupoteza maana, iwe kichekesho.
Hivyo mjasiriamali ni jasiri kidogo tu, hawezi kuitwa shujaa kwani hatazamiwi kufa katika kutafuta mali kwani hakuna anakufa akiuza vitu, labda kama kuna uhalifu, ambao si ujasiri kijamii. Lakini ukifika katika magereza au kuwasikia watu ambao ndugu zao au majirani zao wana mtu aliyewahi kufungwa akatoka jela akaelezea wanayoongea huko, ni wazi mantiki yao ni tofauti na jamii, kwani kwao ujambazi ni "kutafuta maisha,' yaani ujasiriamali. Ni sawa na rushwa miongoni mwa polisi au 'ufisadi' serikalini, ubadhirifu ni 'kutafuta maisha,' tuite ujasiriamali.


Hata hivyo kinachosemwa ambacho kwa bahati mbaya kinauganisha jambazi na mchuuzi au mwanzishaji wa shughuli yoyote ile, ni udiriki wa jambo fulani, yaani kuacha kile unachofanya kila siku, chenye uhakika, uthubutu kuanza kitu kingine. Ujasiri uko katika ufahamu kuwa hakuna biashara inayoanzishwa na uhakika wa mia kwa mia ya kufaulu, na hivyo kuna majonzi tarajiwa au yanayowezekana pale mtu anapoanza shughuli ya biashara. Dhana ya ujasiriamali inasaidia kumpa mtu motisha ya kujituma, kumpa daraja ya wadiriki, na si wabahatishaji, wabangaizaji.


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao miaka kuanzia ya tisini wanaendesha shughuli za pamoja kwa Kiswahili badala ya ile jadi ya Kiingereza walianza kutumia neno 'wabangaizaji' kuzungumzia tabaka la 'wavuja jasho' badala ya neno la Mchungaji Christopher Mtikila, 'walala hoi.'  Wakati siyo kila 'mvuja jasho' ni mbangaizaji, kwani anaweza kuwa na kipato cha uhakika wakati mbangaizaji hana uhakika wa kipato - kwani anangoja atumwe, aitwe, ahitajiwe, au achuuze kwa bahati, ujasiriamali ni tofauti. Hauelekezi hisia katika jasho, na unakwepa na hata kupinga 'ubangaizaji' ambao una maana mtu hajui anachokifanya, hubahatisha tu.


Ujasiriamali una kiini cha ujasiri wake na ubunifu wake katika kugundua mahitaji ya soko, kuwa kina kitu kinachotakiwa, siyo kwa vile hakipo ila kinahitajiwa kwa wingi zaidi au kwa namna tofauti. Ndiyo maana ujasiriamali unajiumiza kwa kiini kile kile kinachouwezesha kuwa na umuhimu, yaani kutokuweza kuona tofauti kati ya kudiriki kushiriki katika shughuli fulani, na kujazana tu katika shughuli hiyo. Watu wanapojazana siyo lazima baadhi wakose riziki, lakini ushindani unakuwa mgumu na baadhi itabidi wapangue waondoke. Mtu anapofaulu kukaa katika eneo alilochagua na kujihakikishia riziki anakuwa mjasiriamali aliyefaulu; akishindwa anakuwa mbangaizaji (hata ingekuwa biashara ya mamilioni) hadi afaulu. Siri ya ujasiriamali ni kuwezesha biashara kuwa endelevu; ujasiri unapatikana kama kofia au pete pale mtu anapokuwa amefaulu, ndipo atambuliwe. Kabla ya hapo huwa anajitambua peke yake au aonekane akijaribu, hata akidhaniwa ni mbangaizaji tu.

CHANZO  CHA  HABARI: GAZETI  LA  MAJIRA NA  JOHN  KIMBUTE ,Jumatatu, Januari , 20   2014,

No comments:

Post a Comment