Friday, April 29, 2016

MAGUFULI AVUNJA BODI YA TCRA



RAIS Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Ally Yahaya Simba. Bodi ya TCRA imekuwa ikiongozwa na Prof. Haji Semboja.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilieleza kwamba Simba amesimamishwa kazi kutokana na kutosimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS).
Taarifa hiyo ilieleza kwamba hatua hiyo ilisababisha Tanzania kupoteza mapato ya takriban sh. bilioni 400 kwa mwaka.
Mamlaka ya Mawasiliano iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu Machi 22, 2013.
Kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano, lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), kwa mujibu wa serikali.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.

Aidha, amemtaka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

"Nataka tukusanye mapato yote ya Serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayekwamisha jambo hili," alisema Rais Magufuli. 

CHANZO  CHA  HABARI : GAZETI   LA  MAJIRA ,Jumatano , April,  27 , 2016.

No comments:

Post a Comment