Saturday, June 22, 2019

ELIMU YA FEDHA : MUDA WAKO NI PESA YAKO

Ndugu  yangu mpendwa, nimekuwa napenda kukuambia sana kauli hii, HAKUNA KITU CHA BURE. Ukiona mtu anakupa kitu bure, jua kuna namna unalipia ambayo wewe hujui au kuna mtu ameshalipa kwa ajili yako. Huu ni msingi ambao ukiweza kuuishi na kuusimamia kwenye maisha yako, utajiepusha na matatizo mengi mno. Mfano huwezi kutapeliwa kama utaishi kwa msingi kwamba hakuna kitu cha bure. 

Sasa tuje kwenye mitandao ya kijamii, orodhesha mitandao yote ya kijamii ambayo unaitumia. Je ni Instagram? Facebook? Whattsapp? Twitter? Snapchat? Na mingine zaidi. Swali ni je umekuwa unalipa kiasi gani ili kutumia mitandao hii ya kijamii?
Ukiacha bando (data) unazonunua ili kuweza kuingia mtandaoni, hulipi hata senti moja kutumia mitandao hii. Lakini unaweza kuitumia muda wowote, masaa 24 kwa siku, siku 7 za wiki.
Swali jingine unalopaswa kujiuliza ni je mitandao hii inapataje fedha za kujiendesha. Maana mitandao hii ina wafanyakazi wengi, na ambao ni wasomi kweli kweli, ina rasilimali nyingi na wamiliki wake ni matajiri wakubwa sana duniani. Ukichukua mfano wa mmiliki wa Facebook na Instagram, ambaye ni bilionea mkubwa duniani, ambaye yupo kwenye watu 10 matajiri zaidi duniani. Hizo fedha wanazitoa wapi?

Kama hujawahi kujiuliza swali hili basi leo unakwenda kupata mwanga, na utakufanya uangalie kwa mtazamo tofauti kabisa mitandao hii ya kijamii.
Mitandao ya kijamii inaingiza kipato kupitia MATANGAZO. Mfumo wao wa biashara uko hivi, kusanya watu wengi watumie huduma yako ya mtandao wa kijamii, kisha nenda kwa mtu mwenye biashara na mwambie unaweza kutangaza biashara yako kwenye mtandao wangu ambao una watumiaji wengi, na wanaotumia huduma hiyo kwa muda wao mwingi wa siku.
Sasa kama unavyojua tabia yetu binadamu, huwa tunafanya zaidi kile tunacholipwa ili kufanya. Kwa kuwa makampuni haya yanapata fedha kwa watu kutangaza kupitia mitandao yao, na kwa sababu wingi wa fedha unaamuliwa na wingi wa watembeleaji na muda ambao watembeleaji wanatumia kwenye mitandao hiyo, basi mitandao hii imekuwa inahakikisha inatumiwa na wengi, na ukishaitumia huachi, kila muda unataka kuitembelea. Kama nilivyokuambia kwenye kipengele namba moja, hujavutiwa kutembelea mitandao hii, umesukumwa kuitembelea kila wakati, kwa sababu unavyoitembelea zaidi, ndivyo wenye mtandao wanatengeneza kipato zaidi.
Hivyo basi, MUDA WAKO = PESA ZAO. Muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii ndiyo fedha ambazo zinawafanya wamiliki wa mitandao hiyo kuwa mabilionea wakubwa.
Swali jingine muhimu sana ni je, kwa matumizi yako makubwa ya mitandao ya kijamii, ni manufaa gani unayapata? Najua wengi mnajiambia naungana na marafiki na kujua yanayoendelea. Kama jibu hilo ni kweli, swali jingine litakuwa je unahitaji zaidi ya masaa mawili kwa siku kutembelea mitandao hii? Je kweli unahitaji kila baada ya nusu saa au saa moja kutembelea tena mitandao hii?
Rafiki, nafikiri unapata picha ni jinsi gani tumechagua kuharibu na kupoteza maisha yetu, kuwafaidisha wengine, huku sisi wenyewe tukibaki hatuna kitu.
Nikuache na mbinu moja ya kupima matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwako. Chukulia hili, kama kila dakika unayotumia kwenye mitandao ya kijamii ulikuwa unailipia shilingi elfu moja, je ungekuwa tayari kulipa shilingi ngapi kwa siku kutembelea mitandao hii?
Je ungekuwa tayari kulipa tsh 120,000/= kila siku ili tu utumie mitandao ya kijamii? (kwa wastani mtumiaji wa mitandao ya kijamii anatumia masaa mawili kila siku). Kama jibu ni hapana basi jua muda unaoweka kwenye mitandao hiyo unaupoteza. Kama kweli unatumia mitandao ya kijamii kuungana na marafiki na kujua yanayoendelea, utahitaji dakika 10 tu kwa siku kwa ajili ya hilo. Muda mwingine utakuwa na manufaa kwako kama utatumia kwenye mambo yenye tija.
Kila unapoingia kwenye mitandao ya kijamii jikumbushe hili, MUDA WAKO = PESA KWAO na jiulize kama kweli unataka kuendelea kuwa bidhaa inayouzwa.
Na mwisho kabisa, pima umuhimu wa mitandao hii kwa kujiuliza kama ungekuwa tayari kulipia ili kuitumia, maana bure inakudanganya na kukupotezea muda wako.

ELIMU YA FEDHA : CHANGAMOTO YA FEDHA

Fedha imekuwa changamoto kubwa sana kwenye zama tunazoishi sasa. Tunapoteza muda na maisha yetu kwenye kufanya kazi ngumu, lakini fedha tunazozipata tunazipoteza kwa kununua vitu ambavyo siyo mahitaji ya msingi.
Makampuni makubwa yanatumia mbinu za kisaikolojia kututangazia bidhaa na huduma zao kwa namna ambayo tunajisikia vibaya kama hatuna wanachouza.
Pia taasisi za fedha zimerahisisha sana matumizi yetu, hata kama mtu huna fedha za kununua kitu, basi ni rahisi kukopa fedha ili kununua unachotaka. Na hapo sasa mtu analipa mkopo pamoja na riba kubwa.
Yote haya ni matatizo ya kujitakia, kwa kushindwa kudhibiti tamaa zetu na kujilinganisha na wengine.
Ili kuondokana na changamoto hii ya fedha, fanya yafuatayo;
  1. Jua mahitaji yako ya msingi ambayo utayagharamia na yale ya anasa ambayo utaachana nayo. Mahitaji ya msingi ni manne, maji, chakula, moto na malazi. Mengine yoyote nje ya hapo ni anasa, yanaweza kusubiri.
  2. Kuwa na bajeti ya matumizi yako ya fedha, usitumie tu fedha kwa sababu unazo, bali weka bajeti na ifuate hiyo.
  3. Usikope fedha kwa ajili ya matumizi, ni kuchagua kupoteza fedha.
  4. Kwenye kila kipato unachoingiza, sehemu ya kumi hupaswi kuitumia kabisa, hivyo ni fedha unayojilipa kwa ajili ya uwekezaji wako wa baadaye.
  5. Usishindane na watu wengine wala kujilinganisha na yeyote kwenye mali, mavazi na hata maisha.
  6. Fanya tahajudi rahisi kabla hujanunua kitu. Kabla hujalipia jiulize je unachotaka kulipia ni hitaji la msingi au anasa. Hii itakuepusha kufanya manunuzi yasiyo muhimu.
  7. Fanya mfungo wa matumizi. Kwa mwezi mmoja, usinunue kabisa kitu ambacho siyo cha msingi. Jizuie kabisa kununua chochote ambacho siyo lazima kwa kipindi cha mwezi mzima, kisha ona jinsi maisha yako yatakuwa bora zaidi.
  8. Wekeza akiba yako kwenye maeneo ambayo yanazalisha zaidi baadaye.
  9. Usinunue vitu ambavyo thamani yake inashuka kadiri muda unavyokwenda.
  10. Ongeza kipato chako kwa kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya, toa huduma bora zaidi, wahudumie wengi zaidi na utaweza kuongeza kipato zaidi.

ELIMU YA FEDHA : MAISHA ULIYOPOTEZA

Watu wengi wamekuwa wanakutana na hali hii, akiwa hana fedha anakuwa na mawazo na mipango mizuri sana ya kutekeleza anapopata fedha. Anakuwa mpole na mwenye akili nzuri juu ya matumizi ya fedha. Akiona wengine wanatumia fedha vibaya anajiambia kama mimi ningepata fedha hizo, basi ningefanya mambo mazuri sana.
Lakini mtu huyo huyo anapopata fedha, anajikuta anafanya vitu ambavyo hata hakupanga kufanya. Mtu akishapata fedha zile akili nzuri na mipango aliyokuwa nayo anasahau kabisa. Anajikuta ananunua vitu ambavyo hakupanga kununua, mahitaji muhimu ambayo hayakuwepo awali yanaanza kujitokeza. Ni mpaka fedha hiyo inapoisha ndiyo mtu anarudi kwenye akili zake na kujiuliza zile fedha zimeishaje bila kufanya mambo mazuri.
Kama umewahi kukutana na hali kama hii usijione kama una bahati mbaya, au ni mjinga sana inapokuja kwenye fedha. Jua hiyo ni hali inayowakumba watu wengi kwenye fedha, na inatokana na wengi kutokuielewa vizuri saikolojia ya fedha. Fedha ni nguvu, na nguvu yoyote isipodhibitiwa na kutumiwa vizuri inaleta uharibifu.
Leo nakwenda kukushirikisha dhana itakayokuwezesha kuwa na udhibiti mzuri kwenye fedha zako, dhana itakayokuzuia usitumie hovyo fedha pale unapokuwa nazo.
Dhana hii ni kuhesabu fedha kwa kulinganisha na maisha ambayo umepoteza kupata fedha hizi. Wote tunajua kwamba muda ni fedha, na pia tunajua kwamba muda ni maisha, hivyo basi maisha pia ni fedha.
Sasa chukua kipato chako unachopata kwa mwezi, kisha gawa kwa masaa unayofanya kazi. Mfano kama kipato chako ni milioni moja, halafu unafanya kazi masaa 8 kwa siku, siku 5 au 6 za wiki, kwa mwezi unafanya kazi kwa masaa 160 mpaka 200. Ukigawa milioni moja kwa masaa 200 utapata shilingi elfu 5. Hii ina maana kila saa unayofanya kazi unalipwa shilingi elfu 5.
Sasa kwa sababu muda ni fedha na maisha ni muda hivyo maisha ni fedha, kila elfu 5 unayoipata, unapoteza saa moja ya maisha yako. ukipata elfu 10 umepoteza masaa mawili.
Sasa kila unapotaka kununua kitu, kabla hujafanya maamuzi ya kukinunua jiulize kwanza swali hili, je kitu hiki ninachokwenda kununua, kina thamani sawasawa na maisha niliyopoteza?
Kwa mfano umekutana na nguo ambayo inauzwa shilingi elfu 20, umeipenda kweli na unataka kuinunua. Jiulize kwanza je nguo hii ina thamani sawa na masaa manne ya maisha yangu? Je kama nikiambiwa nichague kupata nguo hii na kupata masaa manne zaidi kwenye maisha yangu nitachagua nini?
Kwa kuchukulia fedha zako kama maisha ambayo unapoteza, utajijengea nidhamu kubwa sana ya fedha na kuacha matumizi ya hovyo, yasiyo na manufaa kwako. Pia utapata muda zaidi wa kufanya yale muhimu kwako, pamoja na kuwekeza fedha zako maeneo ambayo yanazalisha na hivyo kukusaidia usifanye kazi muda mrefu kupata fedha za kupoteza.
Linganisha kila fedha unayotaka kutumia na maisha unayopoteza, na utaona jinsi gani vitu vingi unavyopenda kununua havina thamani unayovipa.

KWANINI UTAKE KUUZA BIASHARA YAKO ?

"John  Warrillow "  katika  Kitabu   Chake  " BUILT  TO  SELL " anatuambia zipo sababu mbalimbali za wewe kutaka kuuza biashara unayokuwa umeianzisha.
  1. Biashara yako inaweza kuwa ndiyo chanzo chako cha mafao unapostaafu, hivyo kuweza kuiuza kunakupa kiasi kikubwa cha fedha cha kustaafu bila ya shida.
  2. Unaweza kuwa unataka kuanzisha biashara nyingine. Wajasiriamali huwa wanachoka kitu haraka, hivyo ukianzisha biashara na kuona tayari umeichoka na kuna biashara nyingine unapenda kuingia, unaweza kuuza ile uliyonayo sasa.
  3. Unaweza kuwa na uhitaji mkubwa wa fedha kutatua matatizo mbalimbali yanayokukumba. Biashara yako inaweza kuwa kama akiba au uwekezaji wako, ambao unaweza kuuza pale unapokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha kutatua changamoto mbalimbali za maisha yako.
  4. Unaweza kuwa unahitaji kupata muda zaidi kwa ajili yako na familia yako. Pale unapoona biashara yako inachukua muda kuliko unavyoweza kuipa, unaweza kuchagua kuiuza.
  5. Unaweza kuwa unahitaji kulala vizuri usiku bila ya wasiwasi, kwa sababu unapokuwa mjasiriamali, unakuwa na usiku mwingi ambao hulali, unafikiria biashara itakuaje, ushindani utaushindaje, mishahara utalipaje, mikopo unarejeshaje na mengine mengi ambayo yatakunyima usingizi. Lakini unapojua kwamba unaweza kuiuza biashara hiyo muda wowote, unakuwa na utulivu mkubwa wa akili.

KWANINI BIASHARA NYINGI HAZIFAI KUUZA ?

Biashara nyingi hazifai kuuza kwa sababu zinaendeshwa kwa vurugu. Kwa nje biashara inaweza kuonekana inakwenda vizuri, lakini kwa ndani mambo ni vurugu. Hakuna mpangilio wowote wala mfumo ambao unafuatwa. Kila kitu kinafanywa kwa namna ambavyo mtu anajisikia kufanya. Hakuna viwango vyovyote vinavyofanyiwa kazi.
Wateja wanaokuja kupata huduma kwenye biashara, hawaji kwa sababu ya biashara, bali wanakuja kwa sababu ya mtu. Na wengine wanasema wazi kwamba wanataka kuhudumiwa na fulani tu.
Wafanyabiashara wengi hufurahia pale wateja wanapotaka wahudumiwe na wao tu, wakiona ni wateja wanawaamini na kuwakubali sana. Lakini wasijue kama hicho ndiyo kifungo chao.
Huwezi kuuza biashara ambayo haiendeshwi kwa mfumo na kila kitu kinamtegemea mmiliki wa biashara hiyo.
Na biashara ya aina hii inakuwa mzigo kwa mmiliki na kumnyima uhuru.
Karibu tujifunze jinsi ya kutengeneza biashara inayokupa uhuru na unayoweza kuiuza muda wowote na hili litakuwezesha kuwa na biashara bora na isiyokutegemea kwa kila kitu. Na hata kama hutaki kuuza biashara yako, kitendo cha biashara kuweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo, utakuwa ushindi mkubwa sana kwako.

HATUA NANE (8 ) ZA KUTENGENEZA BIASHARA INAYOJIENDESHA YENYEWE NA UNAYOWEZA KUIUZA MUDA WOWOTE

Kutoka kwenye kitabu "BUILT TO SELL", mwandishi " John Warrillow " anatushirikisha hatua nane za kufuata katika kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kuwepo kwa mwanzilishi wa biashara hiyo na pia inaweza kuuzwa muda wowote.
(1). Chagua bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua.
Hatua ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza biashara inayojiendesha yenyewe na unayoweza kuiuza ni kuchagua bidhaa au huduma ambayo ina uwezo wa kukua.
Bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua ina vigezo vitatu;
Moja, inafundishika. Ni rahisi kumfundisha mtu mwingine jinsi ya kufanya kitu hicho na akaelewa.
Mbili; ina thamani kwa mteja. Hivyo mteja anakuwa tayari kulipa bei ambayo umeiweka. Kama kitu kinapatikana kwa wengine, mteja ataenda kwenye bei rahisi. Lakini kama kinapatikana kwako tu na mteja anakihitaji kweli, atakuwa tayari kulipa bei uliyopanga.
Tatu; manunuzi ni ya kujirudia. Mteja anahitaji kuwa anarudia tena na tena kununua. Isiwe ni kitu ambacho mteja ananunua mara moja kwenye maisha yake.
Baada ya kuchagua bidhaa au huduma ambayo inafundishika, ina thamani na manunuzi yake ni ya kujirudia, unahitaji kukaa chini na kuandika mchakato mzima wa jinsi unavyofanya biashara yako. Kila kitu kinachohusika kwenye biashara kinapaswa kuandikwa kwa namna ambayo mtu mwingine anaweza kufundishwa na akaelewa na kufuata. Huu unakuwa ndiyo mwongozo mkuu wa ufanyaji wa biashara yako.
Baada ya kuwa na mwongozo, unapaswa kuipa jina bidhaa au huduma yako. Unaipa jina kuitofautisha na bidhaa au huduma nyingine, hivyo inakuwa ya kipekee kwa wateja wako. Kadiri bidhaa au huduma inavyokuwa ya tofauti na zinazopatikana sokoni, ndivyo inakuwa na thamani kubwa kwa wateja wako.
Baada ya kuwa na jina linaloitofautisha bidhaa au huduma yako, andika maelezo mafupi kuhusu bidhaa au huduma hiyo ambayo yanajumuisha faida zake na jinsi inavyotatua changamoto za wateja wako, na tumia maelezo hayo kwenye masoko.
Katika hatua hii ya kwanza unachagua bidhaa au huduma moja au chache ambao unaweza kuweka nguvu zako zote na ukawafikia wateja wengi na biashara kukua pia. Ukifanya hatua hii kwa bidhaa au huduma nyingi utashindwa.
(2). Tengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara.
Mzunguko wa fedha ndiyo uhai wa biashara yako. Yeyote anayetaka kununua biashara yako, akishaangalia kama inajiendesha yenyewe, anakwenda kuangalia mzunguko wa fedha wa biashara hiyo.
Mzunguko wa fedha kwenye biashara unaweza kuwa chanya au hasi. Mzunguko unakuwa chanya pale mapato ni makubwa kuliko matumizi na hasi pale matumizi ni makubwa kuliko mapato.
Ili kutengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara yako, bidhaa au huduma unayouza inapaswa kuwafanya wateja walipe kwanza kabla ya kuipata. Epuka kuendesha biashara ambayo mteja anapata bidhaa au huduma kwanza halafu analipa baadaye. Hii inaifanya biashara ikae muda mrefu bila ya fedha na hivyo kuwa na mzunguko hasi wa fedha.
Biashara inapokuwa na mzunguko chanya, yule anayetaka kuinunua atakulipa zaidi kwa sababu tayari biashara inazalisha, tofauti na biashara yenye mzunguko hasi ambayo inahitaji kupokea fedha nyingi ili kujiendesha.
(3 ). Ajiri timu ya mauzo.
Baada ya kutengeneza bidhaa au huduma ambayo utaiuza kwa wateja kulipa kabla ya kuipata, unahitaji kujiondoa kwenye kuiuza bidhaa au huduma hiyo. Na hapa ndipo unapohitaji timu ya mauzo, watu ambao wanaenda kuuza bidhaa au huduma kwa niaba yako.
Hii ni hatua muhimu sana ambayo wengi hukwama, unapouza bidhaa au huduma yako mwenyewe, unawafanya wateja wakutegemee wewe. Lakini unapokuwa na mfumo wa mauzo, ambao unaendeshwa na watu wa mauzo, wateja hawakutegemei wewe bali wanategemea mfumo wa biashara.
Kazi yako kama mjasiriamali ni kuuza kampuni yako, siyo kuuza bidhaa au huduma za kampuni hiyo. Ajiri na tengeneza timu bora ya mauzo na ipe mwongozo wa kuuza bidhaa au huduma yako na wewe utapata muda mwingi wa kuikuza zaidi kampuni yako.
Unapoajiri watu wa mauzo, ajiri ambao wana uzoefu wa kuuza bidhaa na epuka sana watu ambao wana uzoefu wa kuuza huduma. Hii ni kwa sababu wauzaji wa bidhaa huwa wanamuuzia mteja kile kilichopo, wakati wauzaji wa huduma wanabadilika kulingana na mahitaji ya mteja. Kwa sasa biashara yako inauza bidhaa, hata kama ni huduma, unapaswa kuiuza kama bidhaa, hivyo watu waliozoea kuuza bidhaa watakusaidia kuuza vizuri bila ya kutaka kubadili chochote.
Pia unapoajiri watu wa mauzo, ajiri angalau wawili. Hii inaleta hali fulani ya ushindani baina yao na inawasukuma kujituma zaidi. Mfano kama mmoja ameuza kwa wateja 10 kwa wiki, na mwingine akauza kwa wateja 7, yule wa wateja saba atakazana naye afike wateja 10. Kadhalika wa wateja kumi atakazana zaidi ili asipitwe. Watu wa mauzo huwa wanapenda kujipima kwa namba, unapokuwa na wawili na kuendelea, wanakuwa na ushindani ambao unawasukuma zaidi.
(4 ). Acha kuuza vitu vingine vyote.
Tumeona chanzo cha biashara nyingi kutokuuzika ni zinaendeshwa kwa vurugu, kila kitu kinauzwa na mteja akisema anataka kitu cha tofauti anapatiwa. Sasa hutaweza kuikuza wala kuiuza biashara kama inaendeshwa kwa vurugu kiasi hicho.
Hivyo baada ya kuchagua bidhaa au huduma moja kuu unayouza kwenye biashara yako, acha kuuza vitu vingine vyote. Inawezekana kuna vitu vingine ulikuwa unauza ambavyo vinakuingizia faida. Lakini kama vipo nje ya ile bidhaa au huduma uliyoiainisha kama msingi mkuu wa biashara yako, basi unapaswa kuacha kuuza vitu hivyo vingine.
Unahitaji kuweka nguvu zako zote kwenye kuikuza biashara yako kupitia bidhaa au huduma yenye fursa ya ukuaji zaidi. Unapojihusisha na kuuza vitu vingine, unawapa wateja wako wakati mgumu kukuelewa na kukutegemea.
Wateja wana tabia ya kujaribu wafanyabiashara, watakujaribu kwenye kutaka bei ya chini zaidi, watakujaribu kwenye kutaka kitu cha tofauti na unachotoa na watakujaribu kwa kutaka uboreshe zaidi kile unachotoa kiendane na wao. Epuka sana mitego na majaribu haya ya wateja, simamia kile ulichopanga na wateja wanapojifunza kwamba unasimamia nini, wanakuheshimu kwa hilo na kuwa tayari kununua kile unachouza.
Muhimu ni uzingatie hatua ya kwanza ya kuwa na bidhaa au huduma yenye thamani kwa wateja na ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
(5). Kuwa na mpango bora wa motisha kwa mameneja wako.
Kadiri biashara yako inavyokwenda, inazidi kukua. Timu ya mauzo inaleta wateja na biashara inakuwa kwenye mzunguko chanya wa fedha. Kwa kuwa wewe huhusiki moja kwa moja kwenye mauzo na wala kuandaa bidhaa au huduma, unahitaji kutengeneza viongozi kwenye biashara yako.
Hata mtu anayetaka kununua biashara yako, anaanza kuangalia uongozi uliopo kwenye biashara hiyo. Hivyo utahitaji kuwapandisha cheo wafanyakazi wako na kuwafanya kuwa mameneja, kisha kuajiri wafanyakazi wengine watakaofanya kazi chini ya usimamizi wao.
Ili mameneja hawa wajitume kweli unahitaji kuwa na mpango bora wa motisha kwao.
Zipo njia mbalimbali za kutoa motisha kwa mameneja wako, ipo njia ya kuwalipa bonasi mwisho wa mwaka kutokana na ongezeko la faida, hii inawasukuma kujituma zaidi ili kutengeneza faida kubwa.
Lakini pia baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanawapa mameneja wao sehemu ya umiliki wa biashara hiyo, kwa kuwapa hisa. Kama lengo lako ni kuuza biashara yako, usitumie njia hii, kwa sababu ukishawapa umiliki, mchakato wa kuiuza biashara hiyo unakuwa mgumu zaidi.
Tumia mfumo wa kulipa bonasi kutokana na ongezeko la faida. Na pale biashara inapouzwa, basi wape zawadi ya bonasi kutokana na mauzo hayo.
(6).Tafuta dalali sahihi kwako.
Baada ya biashara yako kuwa inajiendesha yenyewe, kwa kuwa na timu bora ya uongozi na mzunguko chanya wa fedha, sasa unaanza kuangalia uwezekano wa kuiuza.
Hapa ndipo unapohitaji kutafuta dalali au wakala ambaye atakuunganisha na wanunuaji wa biashara. Zipo kampuni ambazo hizi ndiyo kazi zake, kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji au wanunuaji wa biashara.
Unahitaji kuchagua kampuni ambayo utafanya nayo kazi, ambayo itakuwa upande wako. Hivyo ongea na watu mbalimbali mpaka upate ambaye unaona anaweza kukuwakilisha vizuri kwa wanunuzi wa biashara hiyo.
Kampuni hizi za udalali huwa zinalipwa kwa asilimia ya mauzo bada ya mauzo kufanyika, lakini zinakusaidia sana kukutana na wanunuzi na kuweza kuuza biashara yako.
(7). Iambie timu yako ya uongozi kuhusu mpango wa kuuza biashara.
Timu ya uongozi wa biashara yako ni watu ambao wana imani kubwa sana na wewe. Ni watu ambao wanajitoa sana ili biashara yako ikue zaidi. Hivyo unahitaji kuwa makini sana pale unapotaka kuuza biashara yako.
Kwanza unahitaji kufanya mchakato huo kwa siri mwanzoni wakati unatafuta mteja. Ukishapata mteja sasa, unahitaji kuiambia timu yako kuhusu mpango wako wa kuuza.
Inaweza kuwa wakati mgumu sana kwako kuiambia timu ambayo inakuamini kwamba unapanga kuuza biashara hiyo, wapo ambao watakuchukulia wewe ni msaliti na huwajali wao bali unajali fedha tu.
Hivyo unapopanga kuwaambia, waoneshe kwamba biashara inapouzwa, hata wao pia wananufaika. Mfano biashara ikinunuliwa na kampuni ambayo ni kubwa zaidi, wao wanapata nafasi ya kukua zaidi. Wanakuwa kwenye mazingira bora zaidi ya kufanya kazi na pia wanaweza kupata nafasi za juu zaidi.
Pia waahidi kupata bonasi pale ambapo biashara itauzwa. Kwa njia hii watakubaliana na wewe na watakuwa tayari kusaidia ili mchakato wa mauzo ukamilike vizuri.
Ni muhimu uiambie timu yako kwa sababu anayenunua atahitaji kukutana na timu yako ya uongozi na pia kuna ukaguzi wa kina utakaofanyika kwenye biashara yako, ambao utahusisha kila aliyepo kwenye timu ya uongozi.
Hatua ya nane; geuza ofa kuwa makubaliano ya kisheria.
Wale wanaoonesha nia ya kununua biashara yako huwa wanatoa ofa ya kiasi wanachopanga kulipa ili kununua biashara hiyo. Lakini ofa siyo makubaliano, wakati wowote wanaweza kubadilika.
Na katika makubaliano ya kibiashara, watu huwa wanakuwa na mbinu mbalimbali za kupata kitu kwa bei ya chini. Mfano kwenye kuuza biashara, mtu atatoa ofa yake, kisha atafanya uchunguzi kwenye biashara na baadaye atakuja na matokeo ya uchunguzi na kukuambia kuna mambo ambayo ameyaona na hataweza kulipa ofa ya kwanza na hivyo kupunguza.
Ili kuepuka kujikuta kwenye hali hiyo, kwanza chagua ni kiasi gani upo tayari kupokea kwa kuuza biashara yako. Hivyo wanapokuja na ofa ya juu ya kiasi hicho kubali. Lakini pia wape muda wa ukomo, la sivyo zoezi litachukua muda mrefu zaidi.
Wanapofanya uchunguzi na kuja na majibu yao, ambapo watapunguza ofa yao, angalia kama bado inaendana na mpango wako wa awali. Kama ndiyo basi kubaliana nao na kamilisheni dili. Kama ofa yao iko chini ya mpango wako wa awali kataa na tafuta mnunuzi mwingine.
Zoezi la kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe linategemea zaidi mfumo unaoweka kwenye biashara hiyo, unapokuwa na mfumo bora ndivyo kazi inakuwa rahisi kwako.
Zoezi la kuuza biashara yako huwa ni gumu na linalokuweka kwenye wakati mgumu mno. Hivyo kama unachagua kuuza biashara, lazima ujue una kipindi kigumu mbele yako, kuanzia kupata mnunuzi mpaka kufikia makubaliano.
Iwe unapanga kuuza biashara yako au la, bado utanufaika sana kama biashara yako inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja. Hivyo fuata hatua hizi nane na utaweza kutengeneza bishara bora sana kwako.

USIOGOPE KUCHEKWA , JIFUNZE KUPUUZA


Kwenye maisha, wapo watu wengi sana ambao watakucheka. Labda ni kwa kile ulichosema au unachofanya. Wengi wanapochekwa, hukata tamaa na kuona hawawezi na hawafai pia. Hivyo huacha kabisa kile ambacho wanafanya na kurudi kwenye maisha ya kawaida, kitu ambacho kinaua ndoto zao.
 
KWANINI  WATU  WANAKUCHEKA ?
 
Sababu ya kwanza ni kama unachekesha, kama umeongea au kufanya kitu ambacho kinachekesha, basi watu watacheka. Kama unafanya vituko, watu hawawezi kujizuia, watacheka.
 
Sababu ya pili ni kama hawakuelewi, kama watu hawaelewi kile ambacho umeongea au unafanya, watakucheka. Na hapa ndipo kundi kubwa la watu wanaocheka lipo. Kwa sababu kila ambaye alikuja na wazo la kufanya mambo makubwa, alichekwa. Mwanzilishi wa simu alichekwa, waliotengeneza ndege kwa mara ya kwanza walichekwa, wanasayansi wakubwa kama kina Newton na Einstein walichekwa kwa nadharia zao na hata Viongozi wakubwa wa kifalsafa na kiimani kama Yesu, Mohamad na wengine walichekwa sana wakati wanaanza na maono yao.
 
Hivyo basi, watu wanapokucheka, chagua ni kwa sababu ipi kati ya hizo mbili, kama ni kwa sababu unachekesha basi endelea, maana kuwapa watu kitu cha kucheka ni jambo jema pia. Na kama ni kwa sababu hawakuelewi, endelea kufanya, itafika hatua na watakuelewa, kama wote waliochekwa huko nyuma walivyokuja kueleweka baadaye. Kwa vyovyote vile, usiache kufanya unachofanya, na wala usiogope kusema unachotaka kusema kwa sababu watu wanakucheka. Watu kukucheka hakuna uhusiano wowote na wewe kuacha, ni wao wenyewe.