Kutambua kuwa maisha ni mfululizo wa matukio, magumu na masumbuko kunarahisisha zaidi kuyaelewa maisha mbali na yule ajuaye maisha huenda yatakuwa rahisi kadri anavyoishi. Mapambano katika maisha ni mchezo endelevu unaokomea tu pale mtu anapofika ukomo wa maisha yake. Ukiwa hai basi mapambano hayaishi bali hupokezana gumu moja na kuja lingine. Ukweli huu wengi hawapendi kusikia au kuamini ila kadri muda unavyokwenda na matukio katika maisha yanavyojitokeza ukweli huu unaanza kuwa wazi kwa mtu na kujua kuwa ni kweli mapambano hayakomi katika maisha ya kila siku.
Ukirejea maisha yako nyuma kidogo kuna kipindi umewahi pitia cha magumu kweli na hadi ukafikiria huenda gumu hili halitapita au ni gumu zaidi hayatatokea mengine magumu zaidi ya hayo. Ila muda unapopita unakuja kukutana na jambo lingine ambalo ni gumu kuliko lile la awali. Hili hujitokeza katika maisha yetu ya kila siku namna tunavyokabiliana na mambo. Latoka hili laja hili na mzunguko huendelea hivi bila kuachana.
Zipo nyakati za maisha zinazojitokeza ambazo mtu hufikiria gumu linalojitokeza likiisha litampa mapumziko ila isiwe hivyo. Kuna watu wanafikiria kuwa watakapofanikiwa basi matatizo yataisha yote ila hujawahi ona watu licha kuwa wana utajiri ila wanakutana na ugumu wa namna wanakosa muda na familia zao. Kweli utajiri wameupata ila wanapoteza muda wa kuwa na familia kwa sababu ya muda mwingi kupambana na biashara zao. Wangapi umewasikia namna familia zimelaumu kuwa licha baba au mama kuwa na mafanikio ila wanakosa muda kuwa na wazazi wao wapo bize au kutingwa na mambo ya biashara. Hili limechangia watoto kukosa ukaribu na wazazi na hata malezi kuwa hafifu.
Kuna mwingine anaweza kuona akishapata umaarufu basi magumu yataisha ila umaarufu unakuja na gharama zake au magumu yake. Kuna mambo ambayo mtu akifanya ni ya kawaida ila akifanya mtu mwenye umaarufu haiwi kawaida. Hili linawatesa watu wengi walio maarufu kukosa uhuru wa kuishi maisha ya kawaida hata kama wanayatamani kuyaishi. Ila wanakabiliwa na ugumu wa vipi watu watanionaje, vipi watanifikiriaje ?. Maisha haya ni magumu mno kwao na huwa mabaya zaidi pale wanapokutana na hali za kushuka kimaisha au kiuchumi.
Mifano ni mingi namna maisha ni mapambano na mfululizo wa magumu katika kuishi kwetu. Kila panapojitokeza mafanikio basi magumu nayo yapo karibu. Magumu na mafanikio yapo pamoja hayaachani. Mtu anapofanikiwa kwa kitu fulani basi ina maana ni mshindi wa mambo fulani magumu aloyakabili iwe kwa watu kumwona au yeye mwenyewe kuyapitia kimya kimya. Huu ni ukweli wa maisha ambao mtu akiutambua mapema hatachukia magumu au kuyakimbia bali kuyakabili na kuyafurahia maana ni kupitia magumu ndipo palipo na maana ya maisha na mafanikio.
KOCHA MWL. JAPHET MASATU.
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755 400 128
EMAIL : japhetmasatu@gmail.com
No comments:
Post a Comment