Sunday, March 7, 2021

UKIWA NA RAFIKI KAMA HUYU USIMPOTEZE MAISHANI.

Kipimo ninachotumia kujua faida ya kuwa na rafiki maishani mwangu ni yule aliye na utayari wa kunisaidia nipate kukua na kukomaa katika kuyaelewa mambo na kuyachukulia mambo. Ukuaji na kukomaa “growth & maturity” ndio lengo mama la maisha yetu ya kila siku. Kadri tunavyokua na kukomaa kimwili, kihisia, kiroho na kiakili ndivyo tunavyoweza kuyatawala maisha, kujidhibiti na kujizuia. Unapopata rafiki anayekusaidia ujitambue, ukue na kukomaa ni kupata dhahabu katika maisha yako. Wengi wana marafiki ambao hawawasaidii kutimiza hayo mambo mawili; kukua na kukomaa.

Maisha ya mstoa Marcus Aurelius ni maisha ninayoyapenda mno ingawa mstoa huyu alipata wahi kuishi yapata miaka zaidi ya 2000 ilopita. Namna alivyoishi kupitia rekodi ya maandishi yake aloyaandika kwa siri kupitia kijitabu “Meditations” yamekuwa ni msingi mkubwa wa falsafa ya Ustoa duniani kote. Lengo kubwa la kuandika au kufanya tahajudi ambazo zilikuwa zikimzalia tafakari na kuandika kimekuwa ni chanzo kizuri cha miongozo mizuri ya kuishi kifalsafa na kuyaongoza maisha katika utulivu, kiasi, hekima na ujasiri.

Katika kitabu chake cha “Meditations” Marcus Aurelius anaandika katika kifungu kidogo cha maneno kumhusu rafiki yake Rusticus na ndipo nami nimepata mambo machache ambayo tunaweza kujifunza kutoka kwa Rusticus yatakayoweza kutusaidia kukua na kukomaa katika maisha yetu ya kila siku. Marcus anasema “Rusticus showed me that my character needed discipline and development. He taught me not to be led astray by sophists or by speculative, esoteric philosophies. Not to show off, whether in flowery orations, feats of asceticism, or public acts of charity. To speak and write simply, without rhetorical flourish, following the example of his letters. To react calmly when wronged or offended; not to hold grudges; to reconcile with others as soon as they show willingness. To read books deeply, not superficially. He loaned me books from his own collection, and introduced me to the teachings of Epictetus”.

Maana ya maneno hapo juu Marcus Aurelius anasema“Rusticus alinionesha kuwa tabia au mwenendo wa maisha huhitaji nidhamu. Yeye alinifundisha kutotenda yaliyo kinyume, kuepuka kujionesha kwa chochote kile kwa watu. Nizungumze na kuandika kwa maangalifu huku nikizingatia barua zake. Nijifunze kukabiliana na hali zozote za maisha katika utulivu, kutokuwa na kinyongo; ila katika kusuluhisha na watu pindi wanapokuwa tayari. Kusoma vitabu kwa kina, na kuepuka kusoma kwa juu juu. Rusticus aliniazimisha vitabu toka katika maktaba yake, na kunitambulisha na mafundisho ya Epictetus”.Maneno haya anaandika Marcus Aurelius akitafakari namna rafiki yake Rusticus alimwachia mafunzo makubwa ambayo kwa zama tuishizo kumpata rafiki wa aina hii huenda pakawa ni nadra.

Kutoka katika maandishi haya ya Mstoa Marcus tunapata mafunzo makubwa sita ambayo tutagusia na kujifunza kutoka kwa rafiki yake Rusticus.

Nidhamu Kama Nguzo ya Maisha na Maendeleo;

Nidhamu inaanza katika kujisimamia katika ulichopanga kufanya bila kuanzisha visingizio. Hii ni ngazi ngumu kwa wengi maana wanaweza kufanya kazi pale tu wanaposimamiwa na wengine ila wanapokuja kujisimamia wenyewe wanashindwa kufanya hivyo. Nidhamu binafsi kama kujali muda, kujielimisha, kujidhibiti ni mwanzo wa maisha matulivu na kuweza kuendelea katika maisha. Unapokosa uwezo wa kujisimamia ni dalili ya kutokuwa imara katika nidhamu binafsi ambayo ukiweza inakusaidia kukua na kukomaa.

Kuepuka Kusema au Kuweka Mambo Yako Yote Wazi “Usiri”;

Tunaishi katika zama ambazo watu hawana kujizuia kusema au kuweka mambo yao yote hadharani. Usiri umepungua na watu wanatamani kila wanachokifanya hadi visivyopaswa kushirikishwa katika mtandao wanasukumwa kuwashirikisha wengine. Ukikosa usiri katika zama tuishizo ni kukaribisha kukosa utulivu na sio lengo la falsafa hii kuwa uwe mtu unayeshindwa kujidhibiti katika kuyaweka mambo yako mengine katika usiri au udogo “low profile life”. Epuka kusema ovyo bila kufikiri na epuka mambo yako yote kuyaweka wazi.

Kuepuka Kuzungumza Sana;

Usizungumze kila kitu kwa kusukumwa kutoa maoni kwa mambo yote yanayojitokeza katika maisha. Watu wengi huwa hawana akiba ya maneno pale ambapo wanajaribu kuwa wasemaji wa kila kitu kinachojitokeza hasa kupitia majukwaa ya mtandaoni. Rusticus anamwambia Marcus Aurelius ajiepushe na kuzungumza sana maana katika kuzungumza sana kuna kukosea kwingi kuliko mtu asiyezungumza mara kwa mara.

Kupokea Hali Zote Katika Utulivu;

Watu wengi ikitokea wametukanwa, wamesikia habari za misiba, wamesikia habari za hofu wanavurugika kabisa katika hisia na akili. Ni kweli watu hutofautiana katika kupokea habari au kukabiliana na hali mbalimbali ila kwa walio na msingi wa falsafa Rusticus anamwambia Marcus kuwa ajifunze na kuwa mtulivu nyakati zote anapokuwa katika hali mfano kutukanwa, kuudhiwa, misiba, habari za hofu. Unapokuwa na utulivu unajipa nafasi ya kufikiri na kutambua yaliyo katika uwezo wako na yaliyo nje na uwezo wako. Wengi wasio na msingi wa ustahimilivu si wavumilivu wanapokutana na hali mbalimbali katika maisha. Wakitukanwa nao wanataka kujibu au kulipiza matusi, wakiudhiwa wanakasirika.

Kuachilia Vinyongo;

Unapoweka kinyongo unaziba nafasi ya furaha na utulivu. Unapoweka kinyongo unabaki kuteseka na mawazo au picha kuhusu hali fulani au mtu fulani. Huwezi ukatulia ukafikiria vingine bila kumfikiria mtu aliyekutendea vibaya. Huu ni utumwa mkubwa na kukosa utulivu katika maisha. Rusticus anamwambia Marcus ajifunze kuachilia vinyongo. Funzo hili lipo hata kwetu kuwa tuachilie vinyongo ili tuwe huru, tuache nafasi ya kuwa na furaha. Maisha ni zaidi ya vinyongo

Kutafuta Kusuluhisha Migogoro mapema;

Kuomba msamaha na kuhitaji suluhu ya matatizo ni njia safi na yenye maana kwa maisha ya mwanafalsafa. Rusticus anatoa angalizo kuwa unapohitaji kutatua matatizo basi tafuta suluhu mapema na wakati ambao watu wapo tayari kufanya hivyo. Wakati mwingine watu huwa hawahitaji suluhu na hilo ni suala lililo nje ya uwezo wako. Inapotokea suluhu ipo ifanye ili uendelee na hatua zingine katika maisha.

Kusoma Vitabu Kwa Kina;

Rusticus anajitolea hadi kumpa vitabu Marcus Aurelius ili asome na kukomaa. Pia anamtambulisha katika mafundisho ya kifalsafa ya Epictetus. Rafiki anayekuhimiza kusoma vitabu tena kwa kina anakupa msingi mkubwa wa kujitambua, kukua na kukomaa. Angalizo kubwa analotoa Rusticus ni kuwa Marcus asome vitabu kwa kina na kuepuka kusoma juu juu. Kusoma vitabu kwa kina kuhahusisha kusoma kwa kukirudia kitabu, kufanya tafakari, kuishi au kuyajaribu yaloandikwa na hata kuweza kukosoa kitabu. Usomaji wa namna hii unakupa kukielewa kitabu kwa kina zaidi. Kupitia hili kumenifunza kusoma vitabu vingi kwa kuvirudia mara nyingi zaidi kunakonipa nielewe vizuri na kwa kina.

Umpate wapi rafiki kama Rusticus ?. Kama unaye anayefanana na Rusticus hakikisha unamtunza maishani maana hutabaki ulivyo. Utakua na kukomaa unapoendelea kuishi. 

 

KOCHA    MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

 ( WhatsApp  + 255 716924136 )    /   +  255 755  400  128  /  + 255 688  361  539

 

1 comment: