Sunday, March 28, 2021

MCHEZO UITWAO MAISHA.

 

Chochote kile kinaweza kutokea au kumpata yeyote katika maisha yetu ya kila siku. Hii ndilo somo pana la maisha na asili linavyotuandaa kuwa lolote linaloweza kujitokeza bila kujali mtu, cheo au mazingira. Tumekuwa tunaona mfano kifo kinavyoweza kumkuta yeyote yule na wakati mwingine hata bila kutarajia tunasikia habari za vifo vya watu ambao tulifikiria huenda hawakutakia kufa sasa. Hilo ni moja linalojitokeza ambalo linatufundisha kuwa kwa yeyote yule kifo kinaweza kujitokeza.

Maisha ni mfululizo wa matukio ambayo yanaendelea kutokea na kutufundisha kuwa yale ambayo tulikuwa tukiamini hayawezi kujitokeza hujitokeza. Kuna namna huwa tunafikiria sisi kuwa mambo yataenda vizuri kwa kuwa tumejiandaa vizuri ila huwa tunashuhudia namna mambo yanavyoenda vibaya licha maandalizi yalikuwa mazuri. Asili wakati mwingine inatufundisha tuone mambo kwa sura mpya kabisa.

Maisha yetu yanapokaribia nafasi ya ujana na utu uzima huwa ni masomo mengi tunayoendelea kuyapitia kupitia visa na watu. Kuna mambo huwatokea watu wengine na hili linatuzindua akili kuwa hata kumbe watu wengine nao wanapitia magumu, wanaanguka, wanashindwa au wanafeli. Ukijifunza hili utajiandaa kuwa maisha yataenda kufundisha masomo magumu na kutuondoa ujuaji wetu wa mambo.

Falsafa inatuandaa kwa hili kuwa tutaenda kushuhudia mengi ambayo tulidhani hayawezekani kutokea yatakatokea. Hili litagusa pia hata maisha yetu moja kwa moja kuwa mengine ambayo tutafikiria kuwa hayawezi kujitokeza kwetu basi yatajitokeza. Maandalizi ya kuwa mambo yanaweza kwenda tofauti ni muhimu mno ili uepuke kushangaa au kushangazwa na mambo yatakavyokuwa tofauti. Wengi huwa hawaamini hili mpaka pale ambapo mambo hujitokeza na kugundua kuwa maisha mambo hujitokeza si vile tutakavyo sisi ila hujitokeza namna yalivyo yenyewe tu.

Katika kusubiri au kushuhudia wakati unaokuja mambo yaloonekana hayawezekani yakawezekana linaweza kujitokeza hata katika magumu au matatizo ambayo yapo sasa kuja kuwa na majibu wakati ujao. Magumu yalokuwepo jana na kuonekana ilikuwa ngumu kumalizika basi leo yamepata majibu. Ndivyo inavyojitokeza kuwa magumu ya sasa yataenda kupata majibu na njia itapatikana siku zijazo.

Maisha ni mchezo wa ajabu usoacha kutufunza na kutubadilisha namna tulivyokuwa tukichukulia mambo yalivyo.

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

 (  WhatsApp + 255 716  924 136 / ) /  +  255 755 400128  /  + 255 688361  53 9

EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment