Ni kawaida kwa watu wengi mambo yanapoenda vibaya au tunapoangukia kufanya mambo mabaya au mambo yasofaa au yasokubaliwa na jamii huwa tunajilaumu kwanini tulifanya hayo mambo. Huenda tulifanya hayo mambo sababu ya ujinga, uchanga wetu au katika hasira ila matokeo yanapokuja ndipo huwa tunajilaumu kwanini tuliamua kufanya vile. Ila inaweza isiwe mara kwa mara kujilaumu kwa fursa nzuri au nafasi nzuri zilizowahi kujitokeza katika maisha zikapita bila kuzifanyia chochote tusijue zimebeba kitu kikubwa kwa ajili yetu.
Tunajua kabisa au kuona namna watu fulani wanachokifanya ni kitu kizuri ila hatusemi mpaka pale ambapo wanaacha kufanya au kuishia njiani. Wanapoangukia katika kwenda njia mbaya tunaanza kuwasema au kujilaumu huenda tungewatia moyo au kuwapongeza wangefika mbali. Hili linajitokeza zaidi katika kuathiri watoto pale wanapoonesha mwelekeo mzuri wa vipaji vyao ila wazazi hawawapi pongezi na wao ni rahisi kuvunjika moyo na kuacha kuendeleza vipaji vyao. Ila si kwa watoto hata watu wazima wengi wameishia njiani katika mambo mazuri waloyaanzisha ila waliowazunguka hawakuwaunga mkono.
Mfano mmoja mkubwa ambao unaendelea kujitokeza katika jamii zetu ni kufikiria kuwa kila tulichonacho kitaendelea kuwepo hususani watu wetu wa karibu; wazazi, wenza, watoto, rafiki na wafanyakazi wanaotuzunguka. Nafasi yao ya kuwa nasi huwa tunaichukulia kiwepesi na pengine huwa tuna mipango mikubwa ya kufanya dhidi yao kama kuwashukuru, kupiga nao picha, kufanya mazungumzo na kusikiliza hekima zao, kuwapa tuzo au kuwapongeza ila ngoja ngoja hiyo nafasi hufika kikomo pale wanapohama, kupoteza uwezo fulani au kufa kabisa.
Kuna nafasi inaweza kujitokeza ambapo ulikuwa na nafasi ya kusaidia mtu ila pengine hukuchukulia uzito ikapita na ukasikia matokeo ambayo unajua ungehusika matokeo mabaya yasingetokea. Huenda ni mtu mgonjwa au mtu anahitaji ushauri wako ambapo kwa msaada wako ungeweza kuepusha matatizo kama ya watu kujiondoa uhai na kadhalika. Katika jamii kumekuwepo na matukio kama ya watu kuingia katika vitendo hatarishi, kujikatisha maisha kwa sababu ya watu wanaowazunguka kushindwa kutumia nafasi zao kuwasaidia na huenda wangeepusha mambo mengi yafananiayo na hayo.
Huwa tunasahaulishwa sana pale mambo yanapoenda vizuri na kudhania yataendelea kuwa hivyo siku zote. Hivyo zile nafasi nzuri tunazokuwa tunazipata hatuzipi uzito mpaka pale ambapo zinapita. Unaweza kupata nafasi kubwa ya kuwa mtu mwenye ushawishi na kuna vitu ambavyo unajua kwa nafasi yako ungeweza kufanya na kusaidia watu wengi ila mtu haitumii nafasi mpaka anapokuja kuipoteza. Mstoa Marcus anasema tujilaumu pia pale ambapo nafasi nzuri zinajitokeza ila hatuzitumii zinapita.
Anza leo kutumia nafasi zote nzuri unazokuwa nazo kuhakikisha kabla hazijapotea unakuwa umezitumia vizuri na usijilaumu kwa baadaye. Una nafasi ya kuwa na watu basi ishi nao vizuri, una nafasi ya wazazi basi waheshimu na fanya yale ulotegemea kuwafanyia, una mtu unataka kumpongeza au kumshukuru kwa namna kakusaidia basi mshukuru akiwa hai au tamka ajue hilo. Usije kuanza kujilaumu baadaye kuwa ulikuwa na nafasi zote ila ukaziacha tu bila kufanya chochote.
Nukuu ya Mstoa Marcus ina mengi ya kutufikirisha zama za sasa tuishizo. Nanukuu toka katika kitabu cha MEDITATIONS, “We need to repent not just for the bad things we do, but for the good things we don’t do—such as helping a person in need when we have the opportunity.” Ikiwa na maana “Tunapaswa Kujirekebisha sio kwa Vitu Vibaya Tunavyofanya, Lakini Hata kwa Vitu Vizuri Ambavyo Hatukuvifanya”.
KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755400128
Nafasi Ngapi Nzuri Zimepita Hukufanya Chochote ?
ReplyDelete