Naamini umewahi kujikuta kwenye hali hii, unakuwa na mawazo na mipango mizuri sana.
Unapanga vizuri kwamba utakapozipata fedha, basi utakamilisha vizuri mipango hiyo.
Lakini pia unawashangaa sana wale wenye fedha kwa jinsi wanavyozitumia hovyo, unajiambia kama ungezipata basi ungefanya mambo ya tofauti kabisa.
Inatokea na wewe unazipata fedha, na hapo unasahau kabisa mipango mizuri uliyokuwa nayo, unazitumia fedha vibaya mpaka pale zinapoisha ndiyo unakumbuka ile mipango yako mizuri.
Na ukitaka kudhibitisha hilo, angalia wale watu ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mmoja.
Labda ni kushinda bahati nasibu, au kupata mafao au kufanya biashara yoyote ambayo inaleta kipato kikubwa kwa mara moja.
Wengi huwa kama akili zinahama , wanafanya mambo ya ajabu, na fedha zinapoisha ndipo akili zinarudi na wanaanza kujutia walivyozitumia vibaya.
Siyo kama watu hao akili zao zinahama, bali kinachotokea ni fedha wanazokuwa wamezipata , zimepitiliza kiwango cha fedha walichonacho kwenye akili.
Hivyo akili inashindwa kufikiri kwa usahihi na kufanya kile ambacho ni rahisi.
Wanatumia fedha hizo mpaka zikiisha ndipo akili zinaanza kutafuta fursa za kufanya.
Watu hao hawana tofauti kabisa na wewe, ambaye ukipata pesa mawazo mazuri yanapotea.
Ndio mnafanana.
Umekuwa unajizuia wewe mwenyewe kupata fedha zaidi, kwa sababu kiwango chako cha kifedha kwenye akili ni kidogo.
Umeridhika sana na mshahara unaoupata, au faida unayopata kwenye biashara yako ya sasa.
Na umeyajenga maisha yako kuhakikisha mambo yanaenda hivyo.
Maana angalia hata wale wanaokuzunguka, utaona wote mna viwango vya fedha vinavyofanana.
Mnaishi maisha ya aina moja, hadithi mnazopiga zinafanana na hata changamoto za kifedha kwenu ni zilezile.
Ni mpaka pale utakapoamua kuongeza kiwango chako cha kifedha kwenye akili, ndipo unaweza kutoka hapo ulipo sasa.
Ndipo utakapoweza kuacha kujizuia kupata fedha zaidi ya unavyopata sasa.
Hili litakuondoa kwenye mazoea na utajisukuma kuchukua hatua zaidi.
Utaanza kuongea hadithi tofauti, utaanza kujichanganya na watu tofauti na utaanza kutafuta taarifa tofauti , ambazo zitakusukuma wewe kuwa zaidi.
Jambo muhimu sana ambalo nitaendelea kukusisitiza kila mara ni kwamba hakuna kitu kitakachofanya kazi kama wewe hutachukua hatua.
ReplyDeleteNIkutakie usomaji mwema, upate maarifa sahihi na uweze kuchukua hatua kwa ajili ya mafanikio yako.