Monday, March 22, 2021

JE , NI ALAMA GANI UTAKAYOIACHA UKISHAMALIZA SAFARI YA KUISHI KWAKO HAPA DUNIANI ?

Mtu akisikia habari za kifo huogopa na kuona maisha hayana maana yoyote. Hususani habari za kifo za wale tunaowajua hutuumiza mno na kutuachia maumivu yasomithilika. Tunaumizwa na kifo kwa sababu kubwa mbili. Moja ni namna watu hao walivyoyagusa maisha yetu kwa namna nzuri kiasi kwamba tungetamani wadumu milele. Pili ni namna tulivyojenga ukaribu nao hao watu na hivyo wanapokufa huwa tunaona ndani yetu limeachwa pengo, ombwe au upweke usopimika. Kifo ni sehemu ya maisha yetu ambayo imekuwapo toka vizazi hadi vizazi.

Kifo ni kufunga kwa ukurasa wa maisha ya mtu ya kimwili. Baada ya kufa kwa mtu kinachoanza kuelezwa ni juu ya matendo aloyaacha mtu nyuma yake au alama alizoacha katika namna mbili. Moja ni alama katika mioyo ya watu, hapa tunaona namna watu walikufa zamani ila bado unazo kumbukumbu zao namna walivyogusa maisha yako kiasi huwezi kuwasahau. Pili ni alama za vitu kama majengo, viwanda, vitabu, picha, nyimbo na kadhalika. Tatu ni watoto walowaacha nyuma baada ya kufa kwa mtu. Hizi ni alama kubwa ambazo hubakia na mtu kuendelea kukumbukwa.

Hatujui lini siku tutakayokufa na ikiwa wanaojua siku ya kufa kwao basi ni wale wenye bahati kupata kugundua kuwa hizi ni dakika zangu za mwisho wa maisha basi huandaa wosia, kuandaa msimamo au wengine huandika hata vitabu. Ila kwa watu wengi kifo hutokea kama ajali wakati mwingine. Mtu hajui hili wala lile maisha yanapotea kupitia ajali, kuvamiwa, ghafla, magonjwa na kadhalika. Hili ndilo lifanyalo kuwa kifo kionekane ni FUMBO. Hatujui ni kwa namna gani tumebakiza siku zetu za kuishi.

Kifo ni njia yetu sote ambayo hakuna aliye hai ataiepuka kuwa ataondoka katika Dunia bila kufa. Kifo kipo na kila mmoja kwa nafasi yake na namna yake atamaliza siku alizopewa za kuishi. Nini kitakachobakia baada ya mtu kufa ndilo jambo la muhimu pia tunapoendelea kuishi na tukiwa tungali bado hatujafikia mwisho wa maisha yetu.

Wengi hatuna utaratibu wa kutafakari ukomo wa maisha yetu maana ni habari zenye kutisha mno, tunaziogopa na huwa hatudhanii kuwa tutakufa. Ukweli ni kuwa hata tusipowazia bado njia ya kifo hatuwezi kuiepuka maana ni njia halisi katika maisha yetu ya kila siku baada ya kuisha maisha haya.

Tukifa ndipo huwa tunaanza kuishi katika mioyo ya watu, watu huanza kutukumbuka baada ya kufa kwetu. Ni wakati ambao watu huanza kukufuatilia juu ya kazi ulizowahi kufanya, urithi uloacha au alama yoyote uloiacha kipindi uko hai. Maisha ya mtu huelezwa sana pindi anapokufa kuliko anapokuwa hai. Wengi watafahamu mengi kukuhusu wewe pale watakaposikia umefariki. Alama unazoacha sasa iwe ni kitabu, biashara, namna ya utu wako ulivyogusa watu ni nafasi ya maandalizi itakayosimulia sana ukishamaliza safari ya kuishi kwako hapa duniani.

Je ni alama gani ukatayoiacha katika nafasi ambayo bado ipo sasa ukiwa hai ?. Swali zito ila litakupa maana kubwa ya kuanza kuishi kitoshelevu.

 
NA  KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU
WhatsApp + 255 716924136 ) /  + 255 755 400 128 
EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment