Inawezekana kweli umedhamiria kuacha tabia fulani au mwenendo fulani wa maisha ila unajaribu na kuangukia tena katika ule ule mtindo wa zamani. Usiumie kwa hilo unalopitia maana kuanzisha vitu vipya ni kazi maana mwili huwa ndo kikwazo cha kwanza kabisa katika safari ya mabadiliko. Utatamani kuanza kitu toka ndani ila mwili utaanza kukupa sababu za kushindwa, kujihisi umechoka kuendelea na hatua za mabadiliko. Hili linawakatisha tamaa watu wengi ambao wamejitoa kutamani kuona wakiacha na mambo wasoyapenda kufanya.
Hutaweza kitu kwa siku moja kikakaa kwa uimara. Utaanza na kuanguka, utainuka na kujaribu tena na tena. Ni vile mtoto anavyoanza kujifunza kutembea huwa haanzi mara moja tu kutembea bali hujaribu kushikilia vitu, kuanza kujaribu mwenyewe huku anaanguka na hadi kuanza kutembea mwenyewe. Ila hadi kufikia kutembea mwenyewe huwa anakuwa amepitia hatua nyingi za kuanguka anguka na kuinuka. Ndivyo hali hiyo apitiayo mtoto katika ukuaji hujitokeza katika maisha ya kila siku.
Utapenda kuishi falsafa na kuanza kuiishi ila unajikuta kuna wakati unashawishika kurejea maisha yako ya kale na hili linawatokea watu wengi. Je urudi nyuma ? au usonge mbele ndo wakati ambao kila mmoja aliyeanzisha safari fulani ya maisha husukumwa kubakia pale pale. Ukiwa tayari kutaka mabadiliko lazima ulipie gharama ya kukubali kuwa utakutana na hali za kuanguka na kuinuka tena. Ukianguka usikate tamaa kuwa siendelei mbele bali ni kuendelea kujaribu tena na mwisho utaweza.
Si wakati wote yale unayoyajua utayaishi maana kuna muda utayasikia ila unakumbana na kikwazo cha kuyaishi. Ila usikate tamaa ikiwa shauku yako haishuki katika kutamani kuishi kile unachojifunza kila siku. Endelea kujaribu, kujifunza na kuishi falsafa na unapoanguka usirejee maisha ya zamani.
Inuka na endelea mbele kila unapoendelea kujifunza kukiishi kitu. Hili ni jambo la kawaida hujitokeza katika maisha kuwa unapotaka kuishi kitu kipya utakutana na nafasi za kuanguka ila ukianguka inuka na uendelee mbele. Utapata ukinzani wa watu mbalimbali unapojitoa kwa moyo wako wote kuishi maisha yenye kanuni au falsafa.
KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp + 255 716924136 / + 255 755 400128
No comments:
Post a Comment