Wastoa wana maeneo matatu ya kuzingatia kuhusu kifo.
Kwanza
ni kifo chako mwenyewe, ambapo wastoa wanasema hakuna sababu ya
kukiogopa kifo, kwa sababu ni sehemu ya maisha yako na kinaweza kutokea
muda wowote. Hivyo wakati wowote unapaswa kuwa tayari kukikabili kifo.
Inapofanya jambo lolote, lifanye kama ndiyo mara ya mwisho kwako
kulifanya, kama vile kifo kinakusubiri. Kwa njia hii hutaahirisha jambo
lolote muhimu na utafanya mambo kwa usahihi. Wastoa wanasema kama
unaogopa kifo, maana yake bado hujaanza kuishi. Lakini kama utachagua
kuishi maisha yako, kifo hakitakusumbua, kwa sababu wakati wowote
utakuwa tayari.
Mbili
ni vifo vya watu wa karibu kwetu. Wazazi wetu, watoto wengu, wenzi wetu
na ndugu wengine ni watu tunaowapenda na kuwajali sana. Inapotokea
wamefariki dunia, huwa tunaumia, tunalia na kuhuzunika sana. Kwa wengine
vifo vya watu wao wa karibu huwa vinawavuruga sana, vinaishia kuwapa
magonjwa ya akili. Wastoa wanatuambia vifo vya watu wa karibu kwetu
vinatuumiza kwa sababu vinatukuta hatujajiandaa. Wanatuambia kila
unapoongea au kukutana na mtu wako wa karibu, jiambie kimoyomoyo kwamba
hiyo ni mara ya mwisho kukutana naye. Epictetus anatuambia kila
unapombusu mtoto wako, jiambie unambusu mtu ambaye anaweza kufa muda
wowote. Kwa kuchukulia hivi, utajali sana, kwa sababu unajua mtu anaweza
kupotea muda wowote, na hilo linapotokea utaumia, lakini
halitakuvuruga, kwa sababu ni kitu ambacho ulijua kitatokea, a pia
ulishatumia fursa ulizokuwa nazo kabla mtu huyo hajafariki.
Tatu
ni kujiua. Wastoa wa zamani, wengi waliishia kujiua wenyewe au kupewa
adhabu ya kifo. Hii ilitokana na tawala za kidhalimu zilizokuwepo enzi
hizo na wastoa hawakuogopa kuzisema na kuzipinga. Hilo liliwafanya
wawekwe vizuizini, kufukuzwa au kuhukumiwa kufa. Wastoa walikuwa
wakipokea adhabu hizo bila ya kuruhusu ziharibu utulivu wao wa ndani.
Mfano mstoa alipohukumiwa kifo, alikipokea kama sehemu ya maisha na
kusimamia misingi yake. Lakini pia wapo wastoa ambao walipofika mwisho
wa maisha yao, yaani uzee na kuona wameshakamilisha jukumu lao la
maisha, basi walijiua. Hii ni dhana ambayo ilikuja kupotea, lakini zama
hizi imeanza kurudi. Wapo watu ambao wanachagua kuyakatisha maisha yao
kwa sababu mbalimbali. Hapa hatuzungumzii wale wanaojiua kukimbia
majukumu au matatizo waliyosababisha, bali wale ambao wanaona imetosha
sasa na wanataka kupumzika. Hilo pia ni zoezi la kistoa.
No comments:
Post a Comment