Falsafa
ya Ustoa ilianza miaka 300 kabla ya Kristo ambapo Zeno, mwanzilishi wa
falsafa ambaye kwa wakati huo alikuwa mfanya biashara alikuwa safarini
na chombo chake kikaharibika akiwa Athens Ugiriki. Akiwa hapo Athens,
alitembelea maktaba na kuperuzi maandiko yaliyokuwepo, alikutana na
mafunzo ya Socrates na yakamvutia sana. Akamuuliza mhusika wa maktaba
ile, ni wapi anaweza kuwapata watu ambapo atajifunza zaidi kuhusu
falsafa, na hapo akaoneshwa mwanafalsafa Crates na akamfuata, hapo ndipo
safari yake ya kujifunza na kuwa mwanafalsafa ilipoanzia.
Zeno
alijifunza kupitia Crates ambaye alikuwa kwenye shule ya falsafa
inayoitwa Cynics, ambao ni watu ambao hawakujali kuhusu chochote,
waliishi maisha kwa wakati waliokuwa nao na walihoji na kutilia mashaka
kila kitu.
Baada
ya kujifunza kwenye falsafa hii kwa muda, Zeno aliona falsafa ya Cynics
ilikuwa na mapungufu, kwa sababu huwezi kupuuza kila kitu kuhusu maisha
na ukawa na maisha bora. Hivyo alianzisha shule yake ya falsafa, ambapo
alikuwa akifundisha chini ya mti ulioitwa stoa. Na hapo ndipo jina la
Ustoa (Stoicism) lilipoanzia.
Tangu
kipindi cha Zeno, pamekuwepo wanafalsafa ambao wameiendeleza na kuikuza
zaidi falsafa hii ya zeno. Wanafalsafa kama Cato, Musonius Rufus,
Seneca, Epictetus na Marcus Aurelius kwa nyakati tofauti waliishi na
kufundisha falsafa hii.
No comments:
Post a Comment