Friday, August 9, 2019

HII NDIYO NGUZO MUHIMU KWA KIONGOZI YEYOTE YULE

Mpendwa rafiki yangu,  Mdau  wangu
Unapokuwa kiongozi unakuwa na mamlaka makubwa juu yaw engine, una uwezo wa kuamuru chochote  na kikafanyika. Hivyo basi, kama ukisema utumie mamlaka hayo vibaya lazima utaharibu watu. Utatumia vile unavyotaka na matokeo yake cheo kinakupa kiburi utajiona wewe ndiyo wewe hakuna mwingine.
Tukianzia hata uongozi ndani ya familia zetu, kama baba akiwa ni mtu wa kutumia madaraka yake vibaya lazima ataharibu familia yake. Kama umepewa madaraka basi yatumie vizuri hayo madaraka kuleta matokeo mazuri. Watu wakufurahie uwepo wako kwa kufanya makubwa ambayo yanakuwa ni msaada kwa wote.
Mfano baba anaweza kuwa ni kiongozi wa familia lakini huwa anatoa adhabu kwa watoto kupita kiasi au kwa upendeleo sasa hii inaleta mpasuko kwa watoto, inaleta vinyongo na kuwagawa watoto katika familia.

Kama kiongozi unatakiwa kuwa na nguzo muhimu katika uongozi wako ambayo nguzo yenyewe ni msamaha. Msamaha ni nguzo muhimu sana kwa kiongozi yoyote yule. Siyo kila kosa linahitaji adhabu, kama kiongozi unatakiwa uwe na msamaha katika uongozi wako.

Ukiwa ni mtu wa kufuata sheria katika uongozi wako, yaani kila kosa wewe ni adhabu tu basi utawapoteza watu wengi. Kwa sababu watu wengi wana udhaibu wa kibinadamu na huwezi ukakosa kosa kwa mtu kama ni mtu unayesimamia sheria.
Hapa ndiyo inakuja nguzo muhimu sana ya uongozi ambayo ni msamaha. Msamaha unaleta amani kwenye eneo lolote la uongozi. Msamaha unaleta utulivu,kama kuna mahali watu walikuwa hawana utulivu basi baada ya kiongozi wa sehemu husika wanafurahia msamaha huo na kuwaletea utulivu wa wa akili.
Msamaha unafanya eneo kuwa tulivu,mtaa, nchi, mkoa, kijiji, familia na hata dunia kiujumla. Kwa kupitia msamaha unawaleta watu na kusahau hata tofauti walizonazo.


Kama kiongozi unatakiwa uwe unavaa sifa ya uungu ndani yako, kama ingekuwa Mungu anatoa adhabu kama binadamu basi leo hii hakuna ambaye angeweza kusimama lakini kwa kuwa kuna msamaha, tunaweza kujirudi na kuwa watu wapya tena.
Hatua ya kuchukua leo; kama wewe ni kiongozi siyo kila kosa unapaswa kutoa adhabu muda mwingine unasamehe. Na kumbuka kuwa siyo kila kosa ni la kusamehewa ukiwa unatoa msamaha kwenye kila kosa watu wataacha kufuata tena sheria.
Kwahiyo, kumbuka kuwa kila nafasi ya uongozi uliyonayo ni kama vile unamsaidia Mungu, hivyo angalia sifa za Mungu je unavyoongoza watu wako una nguzo za huruma, msamaha na siyo mwepesi wa hasira? Kuwa mtu wa msamaha na usiwe mwepesi wa hasira maana utawapoteza wengi kama siyo kuwamaliza.

No comments:

Post a Comment