Kwenye Falsafa ya Ustoa, vitu vimegawanyika katika makundi matatu;
Kundi la kwanza ni vitu vizuri kufanya au kuwa navyo (virtues), ambavyo ni vinne; hekima, ujasiri, haki na kiasi.
Kundi
la pili ni vitu vibaya kufanya au kuwa navyo (vices), ambavyo ni
kinyume na hivyo vizuri, yaani, upumbavu, woga, udhalimu na tamaa.
Kundi
la tatu ni vitu ambavyo siyo vizuri na wala siyo vibaya (indifferent),
ambavyo hakuna ubaya kuwa navyo, lakini pia hupaswi kujitesa ili kuwa
navyo. Hapa vitu vingine vyote kwenye maisha vinaingia hapo, kuanzia
afya, kazi, biashara, fedha na kadhalika.
Sasa
kwa misingi ya ustoa, wengi hufikiri inawataka wawe masikini, watu
wasiojali fedha wala utajiri. Lakini katika historia, moja ya
wanafalsafa waliokuwa na maisha mazuri basi ni wastoa. Seneca alikuwa
tajiri mkubwa enzi zake na mwanasiasa, Marcus Aurelius alikuwa mtawala
wa Roma. Kwa kifupi wastoa walijihusisha na maisha ya kila siku na ya
kawaida, wakifanya yale ambayo kila mtu anafanya.
Na
hii ni sababu nyingine nzuri kwa nini tunapaswa kuwa wastoa, kwa sababu
ni falsafa ambayo haipingi mtu kuwa na fedha, au kujihusisha na mambo
mengine, kama tu hayavunji msingi wa wema.
Zipo
baadhi ya dini na falsafa ambazo zinawafundisha wafuasi wake kuachana
kabisa na mambo ya dunia, kutoa maisha yao kwa ajili ya falsafa au Mungu
pekee. Lakini wote tunajua maisha yana mahitaji yake, hutaenda kulipa
ada za watoto kwa falsafa, na wala hutaenda dukani kupata chakula kwa
kusema wewe ni mwanafalsafa.
Hivyo
kwa kuishi kwa falsafa ya ustoa, unakuwa huru kufanya upendacho, ila tu
kiwe sahihi kwako na kwa wengine, na pia unakuwa huru kujikusanyia
fedha utakavyo, ila tu ufanye hivyo kwa usahihi na kwa manufaa ya
wengine pia.
Na
kikubwa nilichojifunza ni kwamba ukiishi misingi ya falsafa ya ustoa,
una nafasi kubwa ya kuwa tajiri, lakini pia utakuwa huru na utajiri huo.
Kwa sababu kwanza utakuwa unafanya kilicho sahihi na kuachana na yasiyo
sahihi, pia utaepuka kufanya mambo ambayo yatakupotezea fedha, kwa
kudhibiti vizuri hisia zako. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kwamba
hutafungwa na utajiri wako, hata kama utapoteza kila kitu, bado utabaki
imara na maisha yako yataendelea.
Naweza
kuhitimisha kwa kusema, Ustoa ni falsafa ya watu wakuu na matajiri,
najua unapenda kuwa mkuu, unapenda kuwa tajiri na kuwa huru na maisha
yako, hivyo basi, ijue na kuiishi misingi ya ustoa.
No comments:
Post a Comment