Friday, April 2, 2021

WATENGENEZA NJIA NI WACHACHE , KUNAMTAKA MTU AMBAYE AMEVUKA UBINAFSI , WATAZAMAJI NI WENGI.

Kutengeneza njia kwataka moyo kweli pale ambapo unapotengeneza njia inayosaidia wengine nao kupita kupitia wewe. Ugeni wa mambo, vikwazo na changamoto za kujitoa sadaka ili uwe wa kwanza kuonesha njia kwa wengine kumefanya pawe na watu wachache ambao wapo tayari kuingia gharama, mateso na magumu huku wakijua huenda wasije kushuhudia au kutambuliwa hata baada ya wao kutengeneza njia kwa ajili ya wengine.

Jamii zetu zina wingi wa watu ambao wameyaona mambo yakienda isivyotakiwa na wanajua hatua ambazo zinaweza kufanyika ila nani aanzishe, nani athubutu ? hapo ndipo wengi huyaacha tu yaendelee kuwepo na kuishi nayo wakiyazoea. Mabadiliko ili yatokee eneo kama hilo ni mpaka pale mmoja ambaye ni jasiri, imara, mwenye nia anapokubali jukumu zito la kutengeneza njia ili wengine waone namna ya kuvuka hapo. Watu hawa si kuwa hawana hofu bali wanaweza kuwa na hofu ila wamechagua kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine wapite na kufaidika.

Kutengeneza njia kwa eneo lolote la maisha ili wengine waanze kuona njia kunataka moyo thabiti, ukakamavu na kuwa tayari hata kufa kwa ajili ya wengine. Kutengeneza njia kunaogopesha maana ni sawa na mtu anayesafiri kwenda safari asiyokuwa nayo wenyeji. Mashaka makubwa hutokea pale ambapo mtu hajui nini matokeo yanayoweza kujitokeza kutokana kwa utengenezaji wa njia kwa ajili ya wengine. Kujitoa ili njia itengenezeke kumegharimu wengine hata maisha yao kukosa kuwa na watu wa karibu ili tu wengine wapate nafasi ya kuvuka.

Kutengeneza njia kunamtaka mtu ambaye amevuka ubinafsi bali kajitoa kubeba magumu, kuwa tayari kujeruhika, kuwa tayari kuvumilia ili njia ipatikane. Hii kazi si rahisi ndo maana huwezi kushangaa kwanini hatuna watu watengeneza njia katika jamii zetu wengi kwa kuwa kazi hii ni ya hatari na ngumu.

Mbali na kufahamu kuwa kutengeneza njia kugumu ila kuna manufaa makubwa sana ya watengenezaji njia ambayo hudumu vizazi hadi vizazi. Mateso ya watu ambao walikubali kuyapoteza maisha yao kwa kupambana, kuvumilia, kustahimili kuanzisha mambo, kubuni vitu, kufikiri na kutengeneza mifumo ni alama kubwa ambayo huwa haifutiki katika maisha kuwa mchango wao ulikuwa mkubwa na mhimili wa maisha tulonayo sasa.

Wakati mwingine wa safari ya kutengeneza njia kwa ajili ya wengine kunaweza kuambatana na upweke na ukiwa. Wengi huona kutengeneza kwao njia kunakuwa kugumu, hali ya kukata tamaa hutokea na wengine hata kurudi nyuma kabisa. Manufaa wanayoyafikiria yatatokea kwa kutengeneza njia ni makubwa ambayo huwasaidia waendelee hilo huwafanya wao wajikaze na kuhakikisha wanafika hadi mwisho wa kuandaa njia kwa ajili ya wengine.

Ukiwa umejitoa kutengeneza njia kwa ajili ya wajao basi jiandae kuwa utakutana na magumu, upweke, mateso na kujikuta peke yako ila alama utakayoacha itakuwa na manufaa makubwa tofauti na ukiacha mambo yaendelee kuwa hivyo hivyo wakati unayo nafasi ya kuonesha njia.

NA  KOCHA  KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM

WhatsApp  + 255 716 924136 /    + 255 755 400128 /  + 255 688 361 539 

EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment