Sunday, October 4, 2020

UCHAMBUZI WA KITABU , MINDSET ( SAIKOLOJIA MPYA YA MAFANIKIO )

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Mindset: the new psychology of success kilichoandikwa na mwanasaikolojia Carol S. Dweck.

Hiki ni kitabu kinachoelezea mitazamo ambayo watu tunayo na jinsi inavyoathiri maisha na mafanikio yetu.

Kupitia kazi zake, tafiti mbalimbali na maisha ya wengine Carol anawagawa watu kwenye makundi makuu mawili;

Kundi la kwanza ni wale wenye MTAZAMO MGANDO ambao anauita FIXED MINDSET.

Huku kundi la pili wakiwa wale wenye MTAZAMO WA UKUAJI ambao anauita GROWTH MINDSET.

Tofauti hii moja na ndogo tu kwenye mtazamo, ndiyo inaleta tofauti kubwa kwenye maisha kati ya wale wanaofanikiwa sana na wale wanaokuwa na maisha ya kawaida.




Mtazamo ambao mtu unakuwa nao, uwe ni mgando au wa ukuaji, unatokana na imani ambazo umekuwa nazo kwa maisha yako yote. Imani hizo hujengeka mapema tangu ukiwa mdogo, kulingana na mazingira yanayokuzunguka.

Kile ambacho wengi tunaita haiba, ni mtazamo wa kuendesha maisha ambao mtu unakuwa umeuchukua na kwenda nao maisha yake yote. Na kitu ambacho kimekuwa kikwazo kwa wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao, ni aina ya mtazamo wanaokuwa nao.

Kwenye kitabu hiki, Carol anakwenda kutuonesha jinsi mitazamo tuliyonayo inavyojengwa, jinsi inavyokuwa kikwazo kwa mafanikio na pia jinsi ya kubadili mtazamo ambao mtu unao na kuwa na mtazamo bora zaidi.

Kitabu kimesheheni tafiti mbalimbali pamoja na mifano ya wale waliofanikiwa na kushindwa kwenye michezo, biashara na hata elimu, kutokana na aina ya mtazamo ambao mtu anakuwa nao.

Kitabu pia kinatusaidia jinsi ya kuwajenga watoto kwenye mtazamo sahihi ambao utawawezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.




Tofauti kuu za mitazamo miwili kwa ufupi.

Mitazamo miwili ambayo watu wanayo, yaani mgando na ukuaji huwa inaleta tofauti nyingi kwa watu, lakini kubwa kabisa na zinazopelekea baadhi kufanikiwa na wengi kushindwa ni hizi;

1. UWEZO WA KIAKILI.

MGANDO; huona uwezo wa akili una ukomo na hivyo hawakazani kujiendeleza.

UKUAJI; huona uwezo wa akili hauna ukomo na hivyo hujiendeleza kwa kujifunza.

2. CHANGAMOTO.

MGANDO; huzikimbia changamoto.

UKUAJI; huzikaribisha changamoto.

3. VIKWAZO.

MGANDO; huona ndiyo mwisho wa safari yao na kukata tamaa.

UKUAJI; huona ni njia ya kufika wanakotaka na hivyo hung’ang’ana.

4. JUHUDI.

MGANDO; huona juhudi hazihitajiki, maana uwezo wao una ukomo.

UKUAJI; huweka juhudi kubwa wakijua zitabadili uwezo wao.

5. KUKOSOLEWA.

MGANDO; huepuka kila aina ya ukosoaji na hawajifunzi.

UKUAJI; hupokea ukosoaji na kujifunza.

6. MAFANIKIO YA WENGINE.

MGANDO; huona wivu pale wengine wanapofanikiwa na kuona ni hatari kwao.

UKUAJI; hufurahia mafanikio ya wengine na kujifunza kutoka kwao.

7. MAFANIKIO.

MGANDO; mafanikio yao hufikia kilele mapema na hawafanyi makubwa.

UKUAJI; wanafikia mafanikio makubwa na kuendelea kufanikiwa zaidi.


No comments:

Post a Comment