Saturday, January 30, 2021

WAWEZA KUPOTEZA BAADHI YA VITU , ISHI KWA KUTHAMINI VITU VINGI ULIVYONAVYO SASA.

 Nyakati nyingi huwa tunajisahau kukumbuka na kushukuru namna licha tutapitia magumu mengi katika maisha lakini bado tukawa hatujapoteza kila kitu katika maisha yetu ya kila siku. Inaweza ikawa imetokea ajali ila umeharibu gari pekee ila umepona wewe hujajeruhiwa na chochote ila unasahau kuwa umepona hilo ukakosa kushukuru. Watu wengi wanakosa kuona walivyobakiwa navyo baada ya kupoteza walivyokuwa navyo kwa kutokujua kuwa kila kitu tulichonacho sasa kipo kwa muda tu kuna siku tunaweza kuvipoteza.

Usiwe kama wengine wanaochukulia kiwepesi vitu walivyonavyo sasa. Usiwe kama watu wengine wasio na shukurani kuwa licha wamepitia magumu bado maisha yanaendelea mfano; bado wapo hai, hawajapoteza kila kitu kama wanavyolaumu. Marcus anatusisitiza namna tunahitaji kushukuru kwa kila kitu kuhakikisha kuwa tunashukuru kwa vile tumebakiwa navyo mbali na tulivyovipoteza.

Hivi umewahi kufikiria ulivyonavyo sasa ungekuwa huna ungesikiaje au kuishije?. Kweli unapitia magumu lakini una watoto, una afya, una ujuzi, una marafiki, una wazazi, una mke au mume. Vipi endapo licha kupoteza vingine ungepoteza na ulivyonavyo sasa ingekuaje. Ona haja ya kushukuru kuwa hujapoteza bali unavyo sasa. Usije kusahau kuwa kwa kila utakachokipoteza vipo utakavyobakiza na hata usipobakiza basi kuna jambo utajifunza kupitia kupoteza ulivyokuwa navyo.

Huwa tunachukulia kiwepesi baraka tulizonazo katika maisha kama kuwa na familia, kuwa hai, kuna na marafiki au watoto, uwezo wa kula au kutembea. Usichukulie kiwepesi vitu kama hivi ambavyo wengine hawana ila wewe unavyo. Hesabu Baraka zako namna unavyomiliki ni vingi pengine ulivyovipoteza. Utaona ukiwa unahesabu vitu ulivyonavyo ni vingi kuliko vile ulivyovipoteza.

Kuhesabu na kushukuru ulivyonavyo vinakupa nguvu na kuthamini zaidi ulivyoachiwa uendelee kuwa navyo. Watu wote wenye moyo wa shukrani wamekwisha kutambua kuwa kila kitu tulichonacho sasa kipo kwa mkopo au kuna siku kitaondoka. Watu hawa huthamini vitu hivi vinavyokuwepo kabla ya kutoweka kwake.

Ishi kila siku kana kwamba chochote kinachojitokeza kuwa tayari kukiona kama ni baraka. Unapotanguliza mtizamo huu kila kitakachokutokea utachagua upande chanya wa kitu hicho. Kila kinachojitokeza huwa kina pande mbili “Double handles”. Moja upande chanya na mwingine hasi. Hata kama utapoteza vitu vingi bado vitakubakizia somo kubwa namna unahitaji kushukuru pia kwa vidogo utakavyobakiziwa katika maisha. Ishi katika moyo wenye kuthamini na kuheshimu vitu vingi ulivyonavyo sasa.


KOCHA  MWL.   JAPHET   MASATU

WhatsApp  +255 716924136

No comments:

Post a Comment