Adui wetu wa kwanza katika chochote tunachotaka kukifanya katika maisha yetu ya kila siku ni Mwili. Mwili umeumbiwa tamaa katika asili yake na utumwa wowote wa maisha basi umekaa katika mwili wa mtu. Tamaa za mwili, tamaa za chakula, ulafi, ulevi vyote vinatoka katika utumwa wa mwili. Mwili unapokosa udhibiti toka ndani ya mtu ni njia rahisi ya maharibifu ya maisha kutokea. Hujaona watu wanavyobadilika kimaisha kwa kukosa udhibiti wa tamaa zitokanazo na mwili ?
Yote haya yanatokea katika mili yetu kwa kuwa hatutoi nafasi ya kujenga mahusiano mazuri na miili yetu. Hili ni kosa kubwa ambalo tunafanya na linatugharimu kushindwa kuishi maisha bora na ya kifalsafa. Mwili ndio ulio na ulimi, macho, miguu, via vya uzazi, ubongo, tumbo na kadhalika. Maeneo yote haya ya mwili yakikosa udhibiti toka ndani hutumika kuleta maisha ya mateso na masumbufu. Hebu fikiria unapokosa kutumia kiungo ulimi vizuri namna utaumiza wengine wengi kwa kauli zako au kutumia vibaya ubongo wako utafikiria mambo mabaya na yenye kuleta madhara kwa wengine.
Lini umekaa na kuushukuru mwili wako kwa mazuri na kuona ni chombo cha thamani kinachokupa heshima ya uwepo wako ?, Lini mwili wako umeupenda na kuupa chakula kizuri, maarifa safi, mapumziko na udhibiti wa mihemko?. Mahusiano mazuri unayojenga katika wewe na mwili wako ni mwanzo wa maisha bora na yenye furaha.
Hiyo ni ngazi moja ya mahusiano matatu makubwa ya maisha yetu. Maeneo mengine muhimu mawili ni “Utambuzi wa Asili yako Kiroho” na Tatu ni “Mahusiano ya Watu wanaokuzunguka Kutenda Haki na Ukarimu”. Ukiziweka ngazi hizi tatu kwa pamoja ni matokeo ya maisha bora na ya furaha.
Ngazi ya pili ya utambuzi wa asili yako kiroho ni mahusiano mengine ambayo watu wengi wamejisahau, wapo gizani na hawalipi uzito katika maisha yao. Kukosekana kwa mahusiano mazuri ya mtu na asili yake ndo panapozaliwa utupu “emptiness” ndani ya mtu. Hii utakuwa unaona mtu ni tajiri, maarufu, kiongozi mkubwa lakini asiye na furaha ndani yake licha kuwa mmiliki wa utajiri mkubwa. Mtu anaweza kuonekana nje ni mwingi wa utajiri ila ni maskini wa roho yake. Utajiri wa roho au utambuzi wa asili kiroho ni mahusiano yanayoleta tuone furaha na maana kubwa ya uwepo wetu katika maisha.
Ngazi hii ya kiroho inatupa kuwa na mtizamo mpana wa maisha. Inatupa tuweze kukabiliana na jambo lolote gumu linaloweza kujitokeza maishani. Ngazi hii inatuunganisha na umoja wetu wa asili na kuwa tu sehemu ya asili na tu wamoja. Ngazi hii inatukumbusha namna lolote tunalofanya kwa wengine si kuwa tunawafanyia hao bali sisi nasi tunaathirika kwa kutenda huko. Mahusiano ya ngazi hii ni sawa na pigo la maji na jiwe linavyoweza yatawanyisha wimbi moja hadi lingine. Ukikomaa ngazi hii utaona namna chochote kinachotokea katika asili kina maana na kinatufungua kufahamu mambo yaliyo zaidi ya kuona kwetu.
Ngazi ya tatu na ya mwisho na ngumu ni “kuishi na watu wanaokuzunguka”. Mtu aliye na jina jema kwa watu wengine utagundua kitu kimoja kikubwa anakimiliki ndani yake. Hicho kitu ni kuwa na mahusiano mazuri ya ngazi mbili tulizozungumzia. Hii ikiwa na maana ana mahusiano mazuri ya yeye mwenyewe “mwili wake” na ana mahusiano mazuri na utambuzi wa kuwa yeye ni mtu wa kiroho. Hutaweza kuona taabu kutenda haki na ukarimu kwa watu wote endapo ndani yako kuna utajiri wa kujua binadamu wote tumeumbwa kusaidiana na kutegemeana. Matatizo yote tunayofanyiana sisi binadamu kwa ubaya ni kwa kuwa ndani yetu tu maskini wa kujitambua na kutambua asili yetu ya kiroho. Watu wote walowahi kuishi na kuacha alama za matendo yao mema basi wana sifa kuu ya haki, ukarimu, upendo, kujitoa na kuwa tayari kufa au kuteketea ili wengine wapate kufaidika.
Hitimisho, navutiwa na kazi za Marcus Aurelius katika kitabu chake cha “The Meditations” ikiwa na maana ya “Tahajudi/Tafakari za Kina” akisema “You have three relationships: First, to your own body; second, to the divine Source of all life and existence; third, to your fellow human beings. And so you have three responsibilities: First, to use your reason to master your body and make right judgments; second, to gratefully accept all that happens in the universe; third, to treat all people with justice and generosity”.
Maana ya kifungu hapo juu Marcus Aurelius anasema “Una mahusiano matatu: Mosi, juu ya mwili wako: Pili, juu ya kiini chako cha kiroho na uwepo wako duniani: tatu, ni juu ya binadamu wenzako. Katika mahusiano haya matatu una majukumu matatu: Mosi, kutumia kufikiri na kuutawala mwili wako na kuamua sahihi; pili, kuwa mwenye shukrani na kukubali kila litokealo katika asili; tatu, ni kuwatendea watu wote haki na ukarimu”.
Yaweke haya mambo matatu pamoja mwaka 2021 na siku zote za maisha yako. Haitakuwa rahisi kwa kuanza lakini kadri unavyoweka nia ndivyo utakavyoendelea kuimarika kwa hizi ngazi zote tatu kwa pamoja. Utoshelevu mkubwa unaokuja kwa kuishi ngazi hizi tatu hauelezeki.
KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp +255 716 924 136
No comments:
Post a Comment