Sunday, January 24, 2021

JIULIZE MWENYEWE : JE, HIKI NACHOTAKA KUFANYA KINA ULAZIMA ?? NI MUHIMU SANA ?

Tumeingia katika matatizo mengi maishani kwa kujaribu kuona kila tunachokiona au kuambiwa na watu lazima tufanye. Maumivu na masumbuko mengi kumbe yangeepukika kwa kutoyaona ni mambo ya lazima kufanya. Watu wameingia katika shida hizo mf. Kutuma picha za kila unachokifanya kiwe mtandaoni na baadaye kimewagharimu watu wengi. Je hiki nachotaka kukifanya kina ulazima inaweza kuwa njia ya kwenda kuepusha matatizo mengi ya mtu kujitakia.

Mtu amekutukana, tulia na jiulize swali hili je kumtukana ni lazima ?, je kulipa kisasi na mimi kwake ni lazima?, kama utajiuliza swali hili mara nyingi basi utaona hakuna ulazima wa kumtusi mtu wala ulazima wa kulipiza kisasi. Kutofanya ulivyopanga kufanya kama wengine ambavyo wangefanya kunakuepusha na mambo mengi. Vipi mtu amekutana na wewe umtusi, je wajua athari zinazoweza kujitokeza hapo ?. Jiulize usichoke swali la je hiki nachotaka kufanya kina ulazima nifanye ?.

Umepata fedha nyingi, na tunavyojua unapokuwa na fedha nayo inakufungua akili ya matumizi ambayo hayakuwepo kabla ya kuwa na pesa. Jiulize je hiki nachotaka kufanya kina ulazima?. Je starehe, pombe, sigara na aina zote za starehe una ulazima kufanya kwa sababu unazo pesa ?. Ukitulia utaona mambo mengi unayotaka kufanya si lazima uyafanye na hili linakusaidia kuepuka matokeo ambayo kwa baadaye unayajutia kwanini ulifanya.

Zama tuishizo sasa hatuwezi kusahau namna fursa mpya mpya kila siku zinaibuka na watu wanakimbizana na kila fursa na mwisho hakuna wanachoambulia kizuri zaidi ya kupoteza muda, nguvu na fedha. Jiulize wakati wote je hii fursa ambayo imekuja kwangu ni lazima niiendee au ni lazima nijiunge nayo?. Utaona fursa nyingi si lazima ujiunge nazo au kukimbizana nazo kila kukicha. Jiulize wakati wote swali hili utajiepusha na matatizo mengi yakuepukika kabisa.

Usije kusahau kuwa marafiki wana nguvu kubwa katika maamuzi ya mambo yetu katika maisha. Mahusiano yao kwetu yanaweza kutuathiri kirahisi zaidi. Na kuna nyakati ambazo unakuwa na msimamo wako wa jambo ila marafiki wanakulainisha unasahau ulichopanga unawafuata wao. Jiulize kila wakati je hiki nachotaka kukubali au kufanya kutokana na hawa rafiki zangu ni lazima?. Najua unaweza kutengwa na watu unapokuwa umesimamia msimamo wako kuachana na mambo ambayo si lazima uyaunge mkono au kuyafanya.

Kadri unavyotumia hii kauli kwa kila muda unapokutana na hali au tukio lolote maishani inakusaidia kuwa na utulivu na kutokuwa mtu unayetumikishwa na hisia. KUANZIA   SASA  kwa kila utakalokuwa unakutana nalo basi jiulize, Je hiki nachotaka kufanya kina ulazima ? Muhimu sana ??

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU

+ 255 716924136 ( WhatsApp ) /  + 255 755 400128  /  + 255 688 361 539 /   + 255 629  748 937

EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment