Sunday, January 24, 2021

MUDA WA KUTIMIZA NDOTO ZAKO NI SASA . ISHI UKIWA TAYARI KUAGA KILA DAKIKA INAYOPITA.

Muda wa sasa ni wa thamani kubwa mno ila watu wengi hawatalii maanani. Thamani ya maisha yetu hufungamanishwa na muda. Unaweza kupima maisha ya mtu kupitia muda na yale ambayo amejitoa kufanya. Mtu anapokufa huandika siku ya kuzaliwa na mwaka na siku ambayo alokufa. Utaona inaitwa RIP fulani xxxx alizaliwa 9/02/2021- kufa 9/7/2067 kinachopimwa hapa ni muda na mchango wa mtu katika siku za kuishi kwake.

Kuna watu ambao wameishi muda mrefu ila mchango wao unaweza kuwa mdogo na wengine wameishi muda mfupi ila mchango wao ukadumu miaka mingi. Utofauti ni namna kila dakika moja yao walivyoweza kuipa uzito na kuishi kitoshelevu kila siku. Ingekuwa kila mtu anajua siku atakayokufa na iko wazi kwake atakufa siku fulani, mwezi fulani au mwaka fulani sidhani kama mtu angekuwa yu tayari kupoteza hata dakika moja ya kuishi.

Tafiti zinaonesha wazi duniani kote kuwa watu ambao wanapokea taarifa za kuwa maisha yao hayatadumu bali watakufa katika kipindi kijacho cha muda. Jambo moja kubwa huambatana na watu hawa huanza kuishi kitoshelevu na kujali kila nafasi ya pumzi yao maana wanajua hawana muda mrefu wataendelea kuwepo. Watu wenye hatua mbaya za saratani ni moja ya makundi ambayo wakati mwingine hupokea taarifa toka kwa wataalamu wa afya kuwa kutokana na namna saratani ilivyoenea au kukua kiasi cha kuyatoa maisha hawana siku nyingi watakufa tu. Je unajisikiaje unapojua ndani ya miezi sita ijayo utakufa ?

Si hilo tu hutokea kwa wale wanaojua watakufa siku sio nyingi pia kuna kundi la watu ambao hunusurika na ajali, walowahi kuwa mahututi na walonusurika vifo mbali na ajali au umahututi. Watu hawa hujenga mtizamo mpya kabisa kuhusu maisha kuwa nafasi ambayo wanayo sasa walipaswa wasiwepo kutokana na kupona katika ajali ambazo watu hawakutegemea endapo wangepona au namna walivyokuwa mahututi watu hawakutegemea endapo wangeinuka tena. Ikitokea wamepona na kuishi tena ile hali ya kujali nafasi ya pumzi huthaminiwa sana.

Je tungoje kuwa tuna nafasi ndogo ya kuishi ?, ndipo tuanze kuishi ndoto zetu?, au kuanza kuihudumia jamii zetu kwa vipaji, uzoefu, hekima au maarifa. Je tungoje tupone katika mambo mazito tutambue thamani ya kila dakika moja ya maisha yetu. Kama wanafalsafa hatungoji kufika hizo hali bali tunaanza sasa kuthamini kila dakika ya maisha yetu tukijua hii dakika moja tunaweza tusiirudie tena au kuipata kwa siku za baadaye.

Weka uzito wa kila dakika ambayo unaipata maishani ukijua kuna watu ambao ndani ya dakika moja wapo wanaokufa, wapo wanaopata ajali, wapo wanaokata pumzi mahospitalini. Hivyo ukiwa na mtizamo wa juu wa kuyaona mambo hivi basi unasukumwa kila siku kuhakikisha unatumia nafasi ya pumzi na muda kuchangia mambo chanya kwa jamii, kuisaidia jamii kimaarifa na kiutambuzi na kuliishi kusudi la uwepo wako.

Hofu kubwa ambazo hutokea pindi maisha yetu yanapokaribia kuisha na tunapopata fursa ya kujua tuna muda mfupi wa kuishi ni hofu mbili kubwa. Hofu ya kwanza ni majuto ya kuwa tulikuwa na muda mwingi ila hatukuishi kitoshelevu au kutumia vipaji au mawazo kwa ukubwa. Pili ni hofu juu ya ulimwengu ujao kuwa je baada ya mwili wetu kuharibika na pumzi kutoweka nini kitakachofuatia. Hilo ni fumbo kubwa la kiimani ambalo mifumo mbalimbali ya dini inaelezea mengi. Fumbo hili gumu kwa kuwa hakuna aliyekufa na akaenda kutafiti na kurejea kusema maisha baada ya kifo yakoje

Ishi maisha kitoshelevu ukiwa unathamini kila dakika unayopata kuwa huenda ndio nafasi ya mwisho kuishi au kutenda jambo fulani. Umeonana na mtu fanya kitu ambacho unajua usipofanya leo basi huenda usipate nafasi hiyo tena katika maisha yako. Unaandika kitu au kitabu kama ndo kitabu unachoandika na hutaandika tena. Kujenga mtizamo huu ni kazi kwa kuanza ila kadri unavyojituma na kuishi hivi utaona siku zako za kushiba hata kifo kitakapokuja hutakuwa na kitu ulichobakiza kuihudumia Dunia. 

KOCHA  MWL   JAPHET   MASATU

 ( WhatsApp  + 255 716 924  136  )

 

No comments:

Post a Comment