Saturday, January 23, 2021

TUNATEGEMEANA NA TUNAHITAJIANA KILA SIKU ILI MAISHA YAENDE.


Hakuna mtu anayeweza kusimama kwa ujasiri na kujipiga kifua mara nyingi nakusema nimeyaweza haya yote kama jeshi la mtu mmoja. Mtu huyu anayesema haya basi hajui maisha ni muunganiko na hakuna mtu awezaye kujisifu na kusema kafanya yote mwenyewe bila kuhitaji watu wengine. Utasema umefanikiwa kibiashara lakini je bila wateja kuja katika biashara yako ungefanikiwa ?

Kila kitu unachokifanya na kufanikiwa jua kuna pahala umehitaji msaada au umetegemea watu wengine. Mf umenunua gari na kuweza kujisifu kuwa unamiliki gari lakini ukiangalia kwa ndani si wewe uliyefanya ubunifu huo wa gari bali pana watu ambao wametengeneza na wewe umepata matokeo tu ya ubunifu wao. Huwezi jidai hapa kusema unaweza kila kitu mwenyewe bila kuhitaji wengine au kutegemea wengine.

Maisha yetu ni muunganiko wa vitu na vyote vyakaa katika umoja siku zote. Kuna msemo rahisi na huwa tunausikia sana “Umoja ni Nguvu”. Umoja ni nguvu kwa maana ya maisha unahitaji nguvu kutoka kwa watu wengine, utawahitaji wengine na utawategemea wengine ili katika umoja huo upate matokeo makubwa. Watu ambao wanaona ni wao wamefanikiwa kwa nguvu zao basi husahau mchango wa watu wengine ambao walijitoa kwa ajili yake.

Huwezi kusimama mwenyewe katika safari ya maisha. Ikiwa hata maiti husaidiwa basi ni zaidi ya mtu aliye hai ambaye kila hatua ya maisha yake inahitaji watu na kutegemea watu. Hili lilionwa toka zamani katika maisha ya wastoa kama Marcus Aurelius ambaye katika maandiko ya notibuku yake anaonesha namna ya kutambua mchango wa kila mtu katika maisha yake kuanzia utoto hadi utu uzima ikihusisha vipindi mbalimbali vya maisha. Hili linamshawishi kuandika kuwa tumeumbwa kwa ajili ya wengine.

Marcus Aurelius anasema “Meditate often on the interconnectedness and mutual interdependence of all things in the universe. For in a sense, all things are mutually woven together and therefore have an affinity for each other – Marcus Aurelius. Hii ikiwa na tafsiri iso rasmi “Tafakari nyakati zote juu ya muunganiko wetu sisi binadamu na mategemeano ya kila kitu katika asili. Jua kuwa kwa namna moja tunaunganishwa na kutegemeana kwa ukaribu kati ya mtu mmoja na mwingine”. Ni maneno mazito na fikirishi sana.

Ubinafsi wa watu na kuona wanaweza kufanya kila kitu ndiko kunachelewesha watu wengi kufanikiwa. Watu ambao wanakuwa wazito kuhitaji msaada au kutegemea watu wengine hawajajua maisha kwa upana. Kwa kuwa hakuna ambaye kapewa kila kitu ndani yake isipokuwa vingine vingi vipo kwa watu wengine. Hili ndilo ambalo linatualika kutegemeana na kuhitajiana maisha yetu ya kila siku ili yaende.

Ishi siku zote katika kuwa sehemu ya muunganiko wa kutegemeana na kuhitajiana. Kuna vitu vingine utavipata kwa wengine ukiwa tayari kujitoa na kujua maisha ni mategemeano na kuhitajiana. Tumeumbwa kuhitajiana kama ulivyo mwili na viungo vyake vinavyofanya kazi katika kusaidiana na kushirikiana.

No comments:

Post a Comment