Kuna namna umewahi kuwahukumu watu katika maisha yako bila kujua ulihukumu haraka kabla ya kujua ukweli wa mambo ulikuaje. Mfano unaweza kumpigia mtu simu na isipokelewe ukaanza kuhukumu ndani yako kuwa huyu mtu mbona hapokei simu, kanidharau, hajali au si mtu makini. Ila huwezi jua ni kwanini hajapokea simu yako. Je huenda yupo mbali na simu utajuaje ?, huenda simu ipo katika chaji, huenda anafanya kitu ambacho kitamzuia kupokea simu kama kusali au kuswali ?. Ila wengi huwa tunahukumu mapema pale ambapo tulotegemea halijafanyika hivyo.
Mahusiano mengi ya watu hasa ya kimapenzi yamevunjika na mengine yakiwa katika misuguano isokoma kwa watu kuhukumu haraka bila kujua kwanini hali hiyo imejitokeza kwa watu wengine. Mfano mdogo ni ule ambao mpenzi mmoja anapiga simu na anakuta simu ya mwenza wake ikitumika “The number you are calling is on another call” ikiwa na maana namba unayopiga inatumika. Wengi huanza kuhukumu mapema kuwa huenda wenzi wao si waaminifu wanazungumza na michepuko yao. Ila je mtu amewahi fikiria vipi anayezungumza naye akiwa mzazi wake, mfanyakazi mwenzake, wateja na kadhalika.
Tumekuwa wepesi sana kuwa na hisia hasi juu ya watu pale ambapo mambo hayaendi vile ambavyo tulitaka iwe. Umepita sehemu na kumsalimia mtu hajakujibu basi unatoka na tafsiri yako kuwa huyu mtu anajiona siku hizi, anadharau au hathamini watu wengine. Huwezi jua kwanini hajaitikia salamu yako. Vipi ikiwa hakusikia, vipi ikiwa ana mawazo mengi katika akili yake au vipi huenda amepokea taarifa mbaya hajatulia. Ila kwa kuwa huwa tunategemea mambo na yasipotokea tunaumia au kuhukumu mapema. Mambo si hivyo huwa wakati wote tutegemeavyo.
Mfano mwingine ni pale ambapo mtu anakutusi. Kutukanwa ni kitu kinachoumiza sana hasa kuumiza hisia endapo utaendelea kufikiria ulichotukanwa. Mtu anayekutukana ukihukumu haraka haraka utaona amekudharau au kukushusha ila ukitulia na usipojibu kuhusu tusi lake na ukatafakari unaweza kujifunza mengi. Unaweza kujiuliza kwanini kaamua kunitukana, je nini kilichomsukuma kunitukana ?. Hapo unaweza kugundua mengi juu ya mtu huyo kuwa huenda ni matokeo ya malezi mabovu aloyapata hivyo ni maisha anayoishi, huenda mtu anayekutusi anatumia njia hiyo kujilinda au kujihami na tatu huenda ni mtu asiyejitambua. Unapoona kitu kwa mfumo huo hutakuwa unahukumu watu haraka bila kujua kwanini wamefanya ulichokiona.
Falsafa inatufundisha kuwa watu wenye kufikiri na kuamua vizuri na si kuongozwa na hisia. Mtu anayehukumu haraka jua kuwa bado hajakomaa katika kufikiri bali anateswa na hisia zake. Unahukumu mara nyingi katika kutofika kwa matarajio yako na mategemeo. Mtu aliyekomaa kifikara na kifalsafa huongozwa na kudadisi na kujiuliza maswali katika yote ambayo hujitokeza na kuja na njia nzuri ya kukabiliana na kitu au hali ilojitokeza.
Tutaendelea kuishi na watu wa kila aina na usiwe mwepesi kuhukumu bila kujua kwanini watu wamefanya hivyo. Utakapojua sababu za wao kufanya hivyo utajikuta ulihukumu haraka kabla ya kujua ukweli wa mambo ulivyo. Tumewahukumu watu wengi bila kujua kilichokuwa nyuma ya pazia kilikuwa kitu gani. Kila litakalotokea usiongozwe na hisia bali fikiri kwanini au ni msukumo gani ulofanya watu au mtu kufanya alichokifanya.
Tunapojua kwa undani kwanini watu wamefanya hicho walichokifanya bila kuwahukumu ni njia rahisi ya kuweza kuwasaidia zaidi.
KOCHA MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp +
No comments:
Post a Comment