Moja; Chagua unaowalenga.
Hatua ya kwanza kabisa kwenye biashara ya maarifa ni kuchagua watu gani unaowalenga na maarifa unayoandaa na kutoa.
Ndiyo
unatoa maarifa ya hamasa, lakini je unataka kuhamasisha watu gani?
Unataka kuhamasisha wanafunzi wafaulu? Au wafanyakazi wapige hatua? Au
wafanyabiashara wakue zaidi kibiashara.
Kamwe
usijidanganye kwamba mafunzo yako yanamlenga kila mtu, kwa kuanza na
kila mtu unakuwa huna unayemlenga kabia. Utatoa mafunzo ya wazi ambayo
hayamlengi yeyote na hivyo hakuna atakayekuwa anakufuatilia.
Nakumbuka
wakati naanza kufanya biashara hii ya mafunzo, nilijifunza kuhusu
kutengeneza msomaji unayemlenga, kumpa sifa anazokuwa nazo. Nilifanya
zoezi hilo na mpaka sasa sehemu kubwa ya wasomaji wanaonifuatilia
wanaingia kwenye sifa zile kwa kiasi kikubwa.
Jua
kabisa maarifa yako yanawalenga watu gani, ili unapoyatoa yawe yanaenda
kwao moja kwa moja badala ya kuwa ya wazi kwa wote. Cha wote siyo cha
yeyote.
Mbili; Jua changamoto zao kubwa.
Ukishachagua watu unaowalenga kwenye maarifa unayotoa, jua changamoto yao kuu.
Kila mtu kwenye maisha kuna changamoto anakabiliana nayo, inayomzuia asipige hatua.
Hivyo
lazima uwe na njia ya kujua wale unaowalenga wana changamoto gani.
Inaweza kuwa kupitia maoni wanayoyatuma wanaposoma, kuangalia au
kusikiliza mafunzo yako, inaweza kuwa yale wanayokutafuta uwasaidie na
kadhalika.
Tatu; Wape maarifa ya kuvuka changamoto hizo.
Baada
ya kujua changamoto kuu za wale unaowalenga, sasa mafunzo yote
unayoyaandaa yanapaswa kuwa ya kuwasaidia kuvuka changamoto hizo.
Jua
watu hawana muda kabisa, na hawaji kusoma kwa sababu umeandika, bali
wanakuja kusoma kwa sababu wana changamoto, wana maumivu ambao hawawezi
kuendelea nayo.
Hivyo kama unakuwa na maarifa yenye manufaa kwao, watakuja kuyapata ili waweze kuondokana na changamoto zao.
Kitu
kingine kikubwa nilichojifunza wakati naingia kwenye tasnia hii ni
kuhakikisha kwa kila mafunzo unayoandaa, kuna hatua ya mtu kuchukua,
hata kama ni ndogo, lakini itakayompa matokeo tofauti.
Kuna
ambao watafurahia tu kujifunza na kufurahia, hao huwezi kuwategemea
sana, lakini wale watakaojifunza na kuchukua hatua kisha wakapata
matokeo tofauti, unaweza kuwategemea kuwa wataenda na wewe kwa muda
mrefu, watajifunza, watakulipa na wataleta watu wengine.
Hivyo
andaa mafunzo yenye hatua za mtu kuchukua ili kuondoka kwenye
changamoto zinazomkabili, kadiri anavyopata matokeo mazuri ndivyo
atakavyoendelea kuwa na wewe.
Nne; Tengeneza mfumo wa watu kujiunga ili kupata maarifa zaidi.
Usijenge
nyumba kwenye kiwanja cha kukodi, naweza kusema hili ni jambo
nililojifunza kwenye hii tasnia na ambalo limekuwa na manufaa makubwa
mno kwangu.
Iko
hivi rafiki, unapotoa mafunzo kupitia mitandao ya kijamii, pale siyo
kwako, hivyo chochote unachofanya huko, hakipo kwenye udhibiti wako.
Unaweza kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao ya kijamii kama instagram,
facebook, youtube na twitter, lakini jua mitandao hiyo ina nguvu ya
kukufungia kwa sababu yoyote ile na ukapoteza kila kitu. Kama
unafuatilia yanayoendelea duniani unajua raisi wa Marekani anayemaliza
muda wake, Dinald Trump amefungiwa kabisa na mitandao mikubwa, pamoja na
kuwa na mamilioni ya wafuasi kwenye mitandao hii.
Nilipojifunza dhana hii ya kutokujenga nyumba kwenye kiwanja cha kukodi, niligawa majukwaa kwenye sehemu tatu;
Sehemu
ya kwanza ni mitandao ya kijamii, hii niliita ni kijiwe, unaweza
kukutana na mtu kijiweni mkaongea mengi, lakini kile kijiwe siyo chako
na mtu huyo anaweza asiwe rafiki kwako, mnakutana tu.
Sehemu
ya pili ni blogu unayoimiliki mwenyewe, hii niliita nyumbani, mtu
unayemkaribisha nyumbani kwako ni rafiki na unamwamini na yeye
anakuamini zaidi ya yule mnayekutana naye kijiweni.
Sehemu
ya tatu ni mfumo wa email (email list), hii niliita chumbani, mtu
unayemruhusu kuingia chumbani kwako ni unayemuamini kweli kweli, na yeye
anakuamini kweli kweli na kuwa tayari kufanya yale unamwambia.
Hivyo
nikawa nashauri watu hili, kama upo kwenye mitandao ya kijamii, lengo
lako siyo kujenga hadhira kule, lengo lako ni kuileta hadhira kwenye
blogu yako. Na watu wakishafika kwenye blog, washawishi wajiunge kwenye
email list yako.
Mitandao
ya kijamii huimiliki, lakini blog ni yako, hata wakitaka kuifungia,
bado unaweza kuipakua na usipoteze chochote. Email list ndiyo mali yako
zaidi, maana hapo wasomaji wako wanakupa taarifa zao na mawasiliano yao,
email na namba za simu. Hata kama jukwaa unalotumia kuendesha mfumo wa
email watataka kukufungia, unapakua taarifa za wasomaji wako na kwenda
nazo kwenye jukwaa jingine.
Pamoja
na kushauri hilo kwa kina, bado wengi wamekuwa hawalipi uzito, sasa
hivi nimeona watu wanafanya kosa kubwa zaidi, wanaandaa mafunzo na
kuyatoa kwa njia ya wasap status, kitu ambacho siyo kibaya, ila mafunzo
hayo yanapotea kila baada ya masaa 24, huoni ni kazi bure.
Nirudie
msisitizo ambao nimekuwa natoa, kama unajihusisha na utoaji wa maarifa,
iwe ni kwa kuandika, sauti au video, hakikisha unakuwa na hatua zote
tatu, unatumia mitandao ya kijamii kuwaleta watu kwenye blog kisha
kwenye blog unawapeleka kwenye email list yako na huko kwenye email
ndiyo mambo mazuri yanaendelea.
Tano; Waombe wawakaribishe na kuwashirikisha wengine.
Wale
ambao watakuwa wanajifunza kwako na kurudi mara kwa mara watakuwa
wanakutumia shuhuda na kukushukuru jinsi ambavyo maarifa waliyopata
kwako yamewasaidia.
Washukuru kwa hilo na wape ombi moja muhimu, wakusaidie kuwakaribisha wengine ambao nao wanaweza kunufaika kama wao.
Kuna njia mbili za kupata wateja wapya, kwa wewe kuwatafuta au kuwatumia wateja ulionao kuleta wateja zaidi.
Njia
ya kutumia wateja ulionao huwa ina nguvu kubwa, kwa sababu mtu
anayeambiwa na mtu wake wa karibu na anayemuamini aje kwako kujifunza,
atazingatia zaidi kuliko akisikia wewe ukijinadi.
Kwa
kila mfuatiliaji uliyenaye, lenga kupata watu wengine angalau kumi na
kisha kuwa na njia mbalimbali za kuwashawishi walete wafuatiliaji zaidi.
Hiyo ndiyo njia nzuri na ya uhakika ya kukuza hadhira yako.
Kuna njia nyingine za matangazo, unaweza kuzitumia lakini kwa uzoefu wangu huwa hazileti watu ambao ni bora.
Sita; Endelea kutoa kazi bora zaidi.
Kosa
moja kubwa la kuepuka kwenye biashara ya maarifa ni ‘kukopi na
kupesti’. Kama unachukua maarifa ya watu wengine na kuyafanya kama yako
halafu unategemea upate wasomaji wanaokuamini na kuwa tayari
kukufuatilia unajidanganya.
Unaweza kuwadanganya watu kwa muda, lakini baadaye watajua na hilo litakuwa anguko lako.
Kwa
maarifa yoyote uliyochagua kutoa, toa mapya na halisi kabisa, kwa namna
unavyoona wewe ni sahihi. Weka utu na upekee wako kwenye maarifa
unayoyatoa kwa kuzingatia kuwasaidia watu kutatua changamoto zao.
Toa maarifa ambayo watu hawawezi kuyapata kwingine kule isipokuwa kwako tu na hicho ndiyo kitawafanya waendelee kuja kwako.
Na
usihofie watu kuiba maarifa yako na kuyatumia kama yao, wewe toa kazi
halisi, kazi bora na wale wanaokopi wanakutengenezea wateja wa baadaye,
kuna siku watajua chanzo na kuja kwenye chanzo.
Saba; Tengeneza mfumo wa kuingiza kipato.
Nimalizie hatua ya mwisho ya kuchukua katika biashara hii ya maarifa, ambayo nimeona wengi wakifanya makosa makubwa hapa.
Wengi
huingia kwenye biashara hii kama hobi, wanatoa maarifa kwa sababu ndiyo
kitu wanapenda. Lakini kadiri wanavyokwenda wanajenga hadhira kubwa
ambayo inataka mtu aipe vitu zaidi na zaidi. Mtu anajikuta akiendelea
kutoa, mpaka inafika mahali anakuwa anatumia muda mwingi kuihudumia
hadhira kuliko uwezo wake.
Lakini
ubaya anakuwa ameizoesha hadhira hiyo kupata huduma bure kutoka kwake.
Siku akipata wazo la kuitaka hadhira ilipie, inamuona kama mtu mwenye
tamaa na hapo mtu anaogopa kuitaka hadhira imlipe, anaishia kuitumikia
bure, kitu kinachokuwa kinamuumiza.
Usifanye
kosa hili, wakati unaanza weka kabisa mfumo wa hadhira kukulipa. Yagawe
maarifa unayotoa kwenye makundi mawili, kuna kundi la maarifa ambayo
unayatoa bure kabisa halafu kuna kundi la maarifa ambayo ili mtu ayapate
anapaswa kulipia.
Na
watu wajue tangu mwanzo, mtu anapojifunza na kufurahia kisha kukutafuta
akitaka zaidi, mwambie ndiyo yapo zaidi, lakini unalipia kiasi fulani
kupata zaidi. Hapo unaijenga hadhira yako mapema kulipia ili kupata
zaidi.
Kama
umeshachelewa, tayari una hadhira kubwa na hukuweka mfumo wa kulipwa,
anza sasa. Endelea na mpango wa maarifa ya bure unayotoa lakini anza
mpango mwingine wa maarifa ya kulipia na ieleze hadhira yako kwamba kama
kuna wanaotaka kujifunza zaidi basi kuna maarifa ya kulipia.
Andika
vitabu kulingana na maswali yanayoulizwa sana na mtu anapokuomba
ushauri kwenye eneo husika basi mwambie asome kwanza kitabu
ulichoandika. Andaa kozi za kufundisha mtandaoni na mtu kulipia
kujifunza. Kuwa na blog au kundi ambalo ili mtu aingie lazima alipe.
Njia ni nyingi, angalia hadhira yako inataka nini zaidi, kuwa na viwango
vya juu vya maarifa hayo na kiasi cha ada ambacho hadhira yako itamudu
na weka mpango huo.
Rafiki
yangu mpendwa, umejifunza mengi hapa kuhusu uendeshaji wa biashara ya
maarifa, nihitimishe kwa kukuambia kitu kimoja, unaweza kuona kama soko
la biashara hii limejaa na watu ni wengi, lakini mimi nimekuwa kwenye
biashara hii kwa muda nakuambia kitu kimoja, soko halijajaa, fursa bado
ni nyingi mno. Wengi wanaofanya biashara hii hawaifanyi kibiashara bali
wanafanya kwa hobi. Watu wana changamoto nyingi ambazo wanakosa maarifa
sahihi kuzitatua. Ukichagua unaowalenga na kujua changamoto zao kisha
kuwaandalia maarifa bora ya kuzitatua huku ukijipa muda wa kujenga
hadhira yako, kuna fursa kubwa.
Nikutakie
kila la kheri kama tayari upo kwenye tasnia hii na nikukaribishe kama
ndani yako una ujumbe ambao unasukumwa kuutoa na uko tayari kuweka kazi.
Maana kingine kinachowaangusha wengi ni kufikiri ni njia ya haraka ya
kupata fedha. Kwa uzoefu wangu binafsi, ndiyo watu watakuwa tayari
kukulipa kiasi kikubwa ili wajifunze, lakini haitakuja haraka,
imenichukua zaidi ya miaka mitano mpaka kuweza kuwatoza watu ada za juu
kwenye mafunzo mbalimbali. Na hiyo yote ni kwa sababu nimekuwa naisaidia
hadhira yangu kupiga hatua na kadiri wanavyopiga hatua wanaweza kumudu
gharama zaidi.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako
MWL JAPHET MASATU