Pesa
ni kitu gani mpaka karibu kila mtu anaitafuta? Kama pesa inatafutwa na
kila mtu, lazima kujiuliza wapi hasa inapatikana. Je? Ni kweli wote
tunafahamu sehemu au mahali inapopatikana? Kama mahali pesa ilipo
hapajulikani tutawezaje kuipata? Maswali yote haya yanahitaji majibu
kwanza kutoka kwa kila mmoja wetu ambaye anazitaka pesa kwa dhati.
Maswali yote haya pia ndiyo yanatoatafsiri
halisi ya kwanini kila mmoja anakwambia kuwa anahangaika kutafuta pesa,
wengine wanakwambia siku hizi kuwa wanapambana. Yote haya yanaonyesha
dhahiri kuwa kuna vita ndani kwa ndani katika fikra, akili na nafsi zetu
juu ya wapi pesa itapatikana.
Uzoefu
unaonyesha kwamba mahali pesa ilipo bado hapajulikani kwa waliowengi.
Kutokana na hali hii, wengi suala la kutafuta pesa linabaki kuwa suala
la kubahatisha na kubangaiza. Kutafuta pesa kwa kubangaiza kumekuwa
ndiyo hali ya maisha ya kila siku kwa waliowengi.
Wakati
ukiendelea kutafuta majibu ya maswali hapo juu, ni vizuri kutambua
mambo makuu muhimu juu ya pesa; Moja ni kwamba, pesa halisi inapatikana
ndani yetu; Pili, pesa yote unayoiona ni ISHARA tu ya kitu fulani
kilichofanyika.
Pesa inakuwaje ISHARA na kupatikana ndani yako?
Nguvu ya hisia ikichanganyika na matamanio ndani ya akili, inaachia nguvu ya ubunifu wa vitu na huduma mbalimbali.
Baada
ya hapo akili yako inakusukuma ili ukamilishe kazi ya kubadilisha huo
ubunifu uliopo katika hali ya wazo kuwa vitu halisi ambavyo mwisho wake
hukuletea pesa.
Ndiyo
maana tunasema PESA ni ishara ya nguvu ya ubunifu ulionao katika hali
ya kuonekana kwa macho. Kwahiyo, pesa tunatembea nazo mawazoni mwetu,
tunalala nazo usingizini, tunakuwa nazo kila mahali tunapokua.
Kazi
tunayo moja tu nayo ni kuzitoa huko ndani yetu. Ili tuweze kuzitoa pesa
ndani yetu tunahitaji kuendelea kujifunza namna bora ya kuzitoa nje,
maana zikikaa tutakufanazo.
Binadamu
ukishapata kile unachohitaji na ukawa na uhuru wa kuchagua upate nini
na uache nini ndiyo unapata kuishi maisha ya furaha na kuridhika pia.
Unachotakiwa
kufahamu ni kwamba wewe umejaliwa nguvu ya ubunifu ndani yako na hiyo
ndiyo hazina ya pesa uliyonayo. Kwahiyo, unatakiwa kuwa mtu mwenye
matumaini na kuhakikisha hofu na mashaka havina nafasi kwako.
Habari njema ni kwamba leo hii kuna idadi ya watu wengi sana ambao tunakaribia kuwa watu bilioni tisa hivi.
Watu
wote hawa wako tayari kulipa pesa ili kukidhi mahitaji yao.
Unachotakiwa kufanya kama wewe ni kukidhi mahitaji ya asilimia ndogo
sana ya watu wote walioko hapa duniani.
Kwahiyo, ukiona umepata pesa ujue kuwa hiyo ni ishara inayoonyesha nguvu ya ubunifu ndani yako.
Wengi
wanaofikiri hawana pesa siyo kwamba hawana nguvu ya ubunifu tunayosema
BALI ni kwamba hawajachukua muda wao kutambua kuwa nguvu hiyo ipo lakini
pia hawajachukua hatua ya kuibadilisha nguvu hiyo kuwa vitu halisi
vyenye thamani na ambavyo vinaweza kuuzika kwa watu wengine tukapata
pesa.
Kila
wakati tuzame zaidi katika kutafiti na kufuatilia hitaji hasa la jamii
tunayoweza kuifikia na katika hitaji lao hilo tuone pesa kwa macho yetu
ya rohoni.
Tukishaona
kwa macho ya ndani tuanze kufanyakazi ya kuitoa ndani kwa maana ya
kufanyakazi kwa vitendo ili kukidhi hitaji lililopo kwenye jamii
husika.
Kazi
ya nguvu ya ubunifu ikishakamilika, watu wenye uhitaji wataleta pesa
kwako na utaanza kuikusanya kwenye kapu, hapo ndio itaanza kuonekana kwa
watu wengine.
Baadae,
utaanza kusikia watu mtaani wakisema fulani amezipata pesa, sijui
amezitoa wapi wakati wao ndio wamezileta kwako….hivyo ndivyo maisha
yanavyokwenda.
Mpendwa
msomaji wa makala hii litafakari sana suala hili la kuitoa nje pesa
iliyoko ndani kwani ni rahisi kuutokomeza umaskini moja kwa moja.
Najua
unapenda kufuata njia za mkato lakini ukweli ni kwamba ukae ukijua kuwa
pesa inayopatikana kwa njia za mkato inadumu kwako muda mfupi sana na
wakati mwingine njia inayotumika siyo rahisi kuitumia wakati mwingine.
Kwahiyo,
wakati ukiendelea na njia zako za mkato anza taratibu kufuata kidogo
kidogo njia hii ya nguvu ya ubunifu ili kutengeneza mfereji wa pesa
zitiririkazo kuja kwako bila kikomo.
No comments:
Post a Comment