Wednesday, August 19, 2020

MAMBO 03 UNAYOHITAJI ILI UNUFAIKE NA USOMAJI WA VITABU

 



Wengi wa wanaosoma vitabu wanapoteza tu muda wao, wanakazana kusoma ili waweze kuwaambia wengine wamesoma vitabu vingapi, huku maisha yao yakiwa hayabadiliki kwa namna yoyote ile.

Huu siyo tu upotevu wa muda, bali pia kuchafua akili, maana kama ambavyo Alexander Pope amewahi kusema, “Maarifa kidogo ni kitu hatari, unapaswa kunywa kwa kina au usionje kabisa maji ya chemchem ya maarifa. Maarifa ya juu juu ni sumu kwa akili.”

Hili tumekuwa tunaliona wazi, mtu anapata maarifa kidogo ambayo hata hajayaelewa kwa kina na kuanza kuona anajua kila kitu, kuanza kuwadharau wengine ambao hawana maarifa hayo, lakini cha kushangaza, maisha yao yanabaki vile vile.




Mtu anaweza kusoma kitabu kimoja au vichache na kujifunza juu juu kwamba elimu rasmi ni upotevu wa muda na ajira ni utumwa. Akatoka hapo na moto wa kwenda kuacha shule au kuacha kazi, lakini anakuwa hajaiva kwenye nini aende kufanya, kinachotokea ni majuto baadaye.

Wapo wanaokuja kukiri wazi kwamba waliponzwa na vitabu na wapo ambao hawataki kuona kosa ni lao, bali hutafuta wengine wa kuwalaumu. Na siku hizi limepatikana kundi rahisi la kulaumu kwenye kupotezwa na maarifa ambalo ni la wahamasishaji au kama wanavyojulikana ‘motivational speakers’.

Mtu anapata maarifa ya juu juu, anatoka akiwa amejaa upepo na kwenda kuchukua hatua, ambazo zinamwangusha vibaya. Badala ya kuangalia tatizo liko wapi, ambalo ni yeye, anatupa lawama kwa mwingine.

Leo tunakwenda kujifunza vitu vitatu unavyohitaji ili uweze kunufaika na usomaji wa vitabu. Ukizingatia vitu hivi vitatu, hutakuja kulaumu usomaji wa vitabu, maana utakuwa na manufaa makubwa kwako.

Kwenye kitabu cha Fahrenheit 451, mhusika mkuu, Guy Montag ni mzima moto (Fireman), ambaye kwenye jamii yao kazi yao siyo tena kuzima moto, bali kuchoma vitabu moto. Ni jamii ya watu ambao wameacha kusoma vitabu na kuendekeza starehe na burudani mbalimbali kama kuangalia tv na michezo mingine.

Guy amefanya kazi hiyo kwa miaka kumi, lakini hajawahi kupata nafasi ya kutafakari kama kazi hiyo ina maana kwake au inampa furaha. Kwa udadisi, amekuwa akiiba vitabu kwenye nyumba wanazokwenda kuchoma, ila hajawahi kuvisoma, amekuwa anavificha ndani.

Siku moja Guy anakutana na binti ambaye anamhoji maswali yanayomfanya aanze kuyatafakari maisha yake na hapo anagundua kwamba maisha anayoishi siyo sahihi.

Anaamua aanze kusoma vitabu, lakini tatizo linakuja kwamba haelewi chochote anachosoma. Siku nzima anakazana kufungua vitabu na kusoma, lakini haelewi chochote.

Anakumbuka aliwahi kukutana na mzee mmoja ambaye alikuwa profesa aliyepoteza kazi yake baada ya watu kuacha kusoma. Anamtafuta ili amsaidie jinsi anavyoweza kusoma vitabu na kuelewa.

Profesa huyo anampa vitu vitatu anavyopaswa kuzingatia ili aweze kusoma vitabu, kuvielewa na maisha yake yabadilike. Hapa nakwenda kukushirikisha vitu hivyo vitatu ili na wewe uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kupitia usomaji wa vitabu.

Kitu cha kwanza; jua jinsi ya kuchagua vitabu vyenye maarifa bora.

Vitabu havifanani, ubora wa maarifa unaopatikana kwenye vitabu haulingani. Kuna vitabu ambavyo ni bora, vyenye maarifa mazuri na unayoweza kutumia kupiga hatua.

Halafu kuna vitabu ambavyo ni vya hivyo, vyenye maarifa ambayo hayana manufaa kwako.

Kitu cha kwanza kuzingatia ni ubora wa maarifa yaliyo kwenye kitabu. Unapaswa kujua jinsi ya kuchagua vitabu bora kwako kusoma ili uweze kupata maarifa ambayo ni bora.

Kwa zama tunazoishi sasa, mitandaoni kunapatikana kila aina ya vitabu, na vingi sana ni vya hovyo. Ikiwa unataka kuanza kusoma vitabu kwa sasa, utajikuta njia panda usijue ni vitabu gani vya kuanza navyo.

Njia rahisi kwako kujua vitabu vya kuanza navyo, ni kuchagua watu ambao wamepiga hatua kwenye eneo unalotaka kupiga hatua, kisha waulize ni vitabu gani wamesoma.

Kama kuna mtu amefanikiwa zaidi yako, kwenye eneo lolote la maisha, kuna vitu anajua ambavyo wewe hujui. Badala ya kumwonea wivu au kumwogopa, mwombe akushirikishe ni aina gani ya vitabu anasoma, hapo utapata vya kuanzia.

Uzuri wa zama hizi ni mitandaoni kuna orodha za vitabu ambavyo wale waliofanikiwa wamekuwa wanashauri watu wavisome.

Hicho ni kitu cha kwanza, kuweza kuchagua vitabu ambavyo ni bora kwa maarifa yaliyo ndani yake.

Kitu cha pili; muda wa kutafakari yale uliyoyasoma.

Kusoma pekee, hata kama ni kitabu chenye maarifa bora kabisa hakutakuwa na manufaa kwako. Kwanza kabisa hutaweza kukumbuka kila ulichosoma na pili siyo kila maarifa yaliyo kwenye kitabu yatakuwa na manufaa kwako.

Hivyo unapaswa kupata muda wa kutafakari kile ulichosoma. Na hapa ndipo wengi wanapofeli na kuja kulaumu wengine. Wanasoma au kusikia kitu na kukimbilia kuchukua hatua kabla hawajatafakari kwa kina.

Kila maarifa unayoyapata, yatafakari kwa kina. Angalia maisha yako yalipotoka, yalipo sasa na kule yanakokwenda. Angalia ni jinsi gani maarifa uliyoyapata unaweza kuyaingiza kwenye maisha yako.

Kwa bahati mbaya sana, kutafakari ni kitu unachopaswa kukifanya mwenyewe, kwa sababu ni wewe pekee unayeyajua maisha yako kwa undani. Watu wawili mnaweza kusoma kitabu kimoja na wote mkakielewa, lakini hatua za kuchukua zikawa tofauti, kwa sababu maisha yenu ni tofauti.

Ambacho nimekuwa nashauri watu kwenye usomaji wa vitabu ni hiki, anza kwa kujua unataka nini kwenye maisha yako, kisha kila kitabu unachosoma jiulize kinakusaidiaje kupata au kufika pale unapotaka kufika.

Ikiwa hujafanya maamuzi unataka nini, kwenye kila kitabu unachosoma utakuja na vitu vipya. Utasoma kitabu cha kilimo cha tikiti na kuona ndiyo kitu bora, unaenda kufanya, unasoma kitabu cha ufugaji wa kuku unaona huo ndiyo wenyewe, unaenda kufuga. Unasoma kitabu cha forex na kusema siwezi kupitwa na hii, unaenda kufanya. Mwisho unajikuta umejaribu mengi lakini hakuna hatua uliyopiga.

Anza na unachotaka, kisha kwa kila kitabu unachosoma, tafakari kinakusaidiaje kufika kule unakotaka kufika.

Kitu cha tatu; kuchukua hatua kwenye yale uliyojifunza na kutafakari.

Kusoma maarifa ambayo ni bora na kuyatafakari jinsi unavyoweza kuyatumia kwenye maisha yako ili kupata unachotaka ni asilimia 10 ya manufaa ya kitabu.

Asilimia 90 inapatikana kwenye kuchukua hatua. Usikubali usome kitabu halafu maisha yako yabaki kama yalivyokuwa kabla hujasoma kitabu hicho. Chukua hatua, hata kama ni ndogo kabisa, kuhakikisha unakuwa bora kuliko ulivyokuwa kabla ya kusoma kitabu hicho.

Hivyo kwa tafakari unayoifanya, weka hatua utakazochukua na anza kuzichukua mara moja. Hazihitaji kuwa hatua kubwa sana, bali zinapaswa kuwa hatua zenye tija kwako, kiasi kwamba ukijiangalia unaona kitabu ulichosoma kimekuwa na manufaa kwako.

Siyo maarifa yote unayoyapata kwenye kitabu utaweza kuyatumia kwa mara moja, kuna mengine utayahifadhi kwa ajili ya baadaye. Lakini hupaswi kusoma kitabu na ukamaliza kisha ukarudi kwenye maisha yako ya awali kama yalivyokuwa. Badili kitu kwenye maisha yako, hata kama ni mtazamo wako au jinsi unavyotumia muda wako na kuendesha siku zako.

Kuna mengi ya kufanya pale unapopata maarifa bora na kuyatafakari yanakufaaje kwenye maisha yako.

Soma vitabu kwa tija na viwe na manufaa kwenye maisha yako, chagua vitabu vilivyo bora, pata muda wa kutafakari ulichojifunza na chukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Ukizingatia hayo matatu, usomaji wa vitabu utayafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri , JIUNGE  NA   DARASA  ONLINE---NA  ENDELEA   KUSOMA  KILA   SIKU  HAPA   "MAISHA  NA   MAFANIKIO   BLOG "  LIFE   AND   YOU  

Tuwasiliane  kwa  + 255 716 924136 /   + 255  755 400128 /  + 255 688 361 539  

Ndimi  KOCHA   MWL    JAPHET   MASATU


No comments:

Post a Comment