Kupanga ni rahisi, ila kuchukua hatua kwenye kupanga ndipo wengi wanapokwama. Ni rahisi sana kupanga halafu wakati wa kufanya unapofika unaahirisha.
Hata haya uliyojifunza hapa, utafurahia kweli na kujiambia utayafanya, lakini inapofika wakati wa utekelezaji, unaona huwezi kuanza sasa, au unahitaji maandalizi zaidi na sababu nyingine lukuki.
Iko hivi rafiki, mazoea ni rahisi, kufanya kitu kipya kunaumiza, unakimbia kufanya kwa sababu hutaki maumivu.
Hakuna namna utaweza kufanya makubwa wewe peke yako, lazima utaishia kuahirisha na kujiambia haujawa tayari.
Hivyo ili kujijengea nidhamu na udhibiti kwenye kutekeleza mipango yako, unahitaji nguvu ya nje. Unahitaji mtu ambaye atakusimamia kwa karibu, ambayo hatakuachia kirahisi pale unapojipa sababu.
Unaweza kufanya hivyo kwa njia kuu tatu;
Njia ya kwanza ni kujiunga na kikundi cha watu wanaofanya kitu fulani, ukiwa ndani ya kikundi unasukumwa zaidi kufanya kwa sababu hutaki kuwaangusha wengine.
Njia ya pili ni kuwatumia watu wako wa karibu kukusukuma kufanya, hapo unaweza kumwambia mtu kwamba utafanya kitu fulani, na usipofanya basi utapaswa kumlipa kiasi fulani. Unapojua kwamba usipofanya utalipa gharama basi utapata msukumo wa kufanya.
Njia ya tatu ni kuwa na kocha ambaye anakusimamia kwa karibu. Kwa kuwa na kocha, mnaweka mipango na hatua za kuchukua, kisha kocha anakufuatilia kwa karibu kwenye utekelezaji na kuendelea kukupa mwongozo zaidi.
Tumia moja ya njia hizo au zote kwa pamoja kwenye yale unayopanga kufanya na utapata msukumo mkubwa wa kufanya kila unachopanga kufanya.
Kujijengea nidhamu na udhibiti ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yako, huwezi kufanikiwa kama unayaendesha maisha yako kikawaida. Lazima ujue pia kwamba kujijengea nidhamu na udhibiti kutakuja na maumivu, utakosa baadhi ya uliyoyazoea, lakini utapata yaliyo bora kabisa.
Fanyia kazi haya uliyoifunza hapa na hutaweza kubaki pale ulipo sasa.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
No comments:
Post a Comment