Kitu pekee tunachojifunza kwenye historia ni kwamba hakuna
tunachojifunza kwenye historia, hiyo ni kauli aliyowahi kuitoa mwanafalsafa
Hegel.
Ni kauli nzito na inayopaswa kutufundisha mengi, lakini kama
Hegel alivyoeleza, haitufundishi chochote.
Iko hivi rafiki, hakuna kitu kipya kinachotokea hapa duniani
kwa sasa. Kila kinachotokea sasa kimewahi kutokea huko nyuma, kwa sasa
kimetokea tu kwa namna tofauti, labda kutokana na teknolojia kuwa ya juu.
Kuanzia matatizo yanayoikumba dunia, nchi na hata mtu mmoja
mmoja, yote yamewahi kutokea tena huko nyuma. Maisha tunayoishi sasa ni marudio
tu.
Lakini cha kushangaza, tunarudia makosa yale yale ambayo
waliotutangulia waliyafanya walipokuwa wanapitia hali kama tunazopitia sasa.
Kama tungechukua muda kujifunza kupitia waliotutangulia, tungepunguza makosa
ambayo tunafanya.
Lakini hatufanyi hivyo, kwa sababu ambazo nakwenda
kukushirikisha hapa. Kwa kila sababu nitakushirikisha hatua ya kuchukua ili
maisha yako yaweze kuwa bora na uweza kukabiliana na kila changamoto unayopitia
sasa.
( 01 ). WATU
KUACHA KUSOMA VITABU.
Uandishi ndiyo uvumbuzi mkubwa kuwahi kutokea duniani,
alinukuliwa Abraham Lincolin. Hebu fikiria, leo hii unaweza kusoma vitabu
vilivyoandikwa zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita. Ni kwa sababu uandishi
umeruhusu maarifa hayo kuweza kutunzwa na kurithishwa vizazi na vizazi.
Uzuri ni kwamba, kila unachopitia sasa, kuna mtu alishapitia
miaka mingi iliyopita na akaandika kitabu kuhusu uzoefu wake kwenye hilo
alilopitia. Kama mtu alipambana na kitu kwa miaka kumi na kukiandika kitabu,
unaweza kukisoma kwa siku chache na ukaokoa kupoteza miaka 10 kwa kurudia
makosa waliyofanya wengine.
Lakini cha kusikitisha ni kwamba watu wameamua kuacha kusoma
vitabu. Wana kila sababu kwa nini hawasomi vitabu, lakini hakuna sababu yenye
mashiko. Ni sawa na kukutana na mtu ambaye yuko mbio na unajaribu kumsimamisha
anakuambia anachelewa. Ukimuuliza kwani unawahi wapi, hajui, lakini yuko kasi.
Ondoka mara moja kwenye tabia hiyo ya kutokusoma vitabu,
chagua eneo unalotaka kubobea, amua wapi unataka kufika, kisha tafuta vitabu
bora kwenye hayo na visome.
Ukitenga saa moja kila siku ya kusoma, au ukaweka utaratibu
wa kusoma kurasa 10 za kitabu kila siku, kila mwezi utamaliza angalau kitabu
kimoja na kwa mwaka angalau vitabu kumi.
Kama utatafakari yale uliyojifunza kwa kina, kisha ukachukua
hatua kwenye maisha yako, huwezi kubaki pale ulipo sasa. Lazima utapiga hatua
kubwa, utaepuka kurudia makosa ya wengine na kujifunza njia bora zaidi za
kufanya unachofanya.
( 02 ). WATU KUPENDA KUSOMA
VITU VIFUPI.
Vitabu ni njia moja ya kujifunza, lakini pia zipo njia
nyingine za kujifunza, kama kupitia makala, tafiti, ripoti mbalimbali na hata
insha.
Uzuri ni kwamba, tunaishi kwenye zama ambazo mtandao wa
intaneti unarahisisha kusoma maarifa hayo mbalimbali, tena bure kabisa.
Lakini cha kushangaza, watu hawapendi kusoma vitu virefu.
Makala kama hii, wengi walioanza kusoma wameishia aya ya tatu, na wengine
wanapita wakiangalia vichwa au maneno yaliyokolezwa tu.
Watu hawana tena umakini na utulivu wa kuweza kutenda dakika
kumi za kusoma kitu kwa kina na kuondoka na maarifa ya kwenda kufanya kazi.
Usumbufu ni mwingi, kila mtu anapitia vitu juu juu, kinachotokea
ni maarifa mazuri yanaelea huko mtandaoni huku wanaoyahitaji wakiteseka. Ni
sawa na mtu ambaye anaogelea kwenye ziwa, lakini anakufa kwa kiu.
Kuondokana na hili, kwenye siku yako tenga muda ambao
utasoma vitu kwa kina, ni bora usome vitu vichache kwa kina kuliko usome vitu
vingi kwa juu juu. Kwa kila unachosoma, usikiache mpaka umeorodhesha nini
umejifunza na namna gani unaenda kuboresha maisha yako.
Chagua mitandao au waandishi ambao utakuwa unajifunza kwao
na weka umakini wako wakati unasoma kitu chochote kile. Usiwe na haraka wala
kukimbilia popote, hakuna mashindano wala tuzo za aliyesoma vitu vingi zaidi.
Tuzo pekee ni maisha yako kuwa bora, hivyo kazana na hilo.
( 03 ). WATU KUTUMIA
MUDA MWINGI KWENYE
MITANDAO YA KIJAMII.
Mitandao ya kijamii imepata umaarufu mkubwa na karibu kila
mtu anaitumia kwa sasa. Mitandao hii imetuhadaa kwamba inatupa nafasi ya
kuwasiliana na wengine na kutengeneza marafiki wengi.
Lakini ukweli wa mitandao huu umekuwa unafichwa. Mitandao
hii imetengeneza mabilioni ya pesa, kwa kukuuza wewe. Angalia, hii mitandao
haina bidhaa yoyote inayouza, na wewe unaitumia bure. Unajua inapataje pesa?
Kwa kuuza umakini wako kwa watu wanaotaka kutangaza biashara zao mbalimbali.
Mitandao hii pia imechangia watu kukosa muda na umakini wa
kusoma vitabu na mafunzo mengine mazuri.
Mtandao wa instagram umepata umaarufu mkubwa kwa sababu
huhitaji kufikiria chochote, wewe piga picha yako na weka, halafu subiri wa
kukusifia na kukupa likes.
Mtandao wa twitter umepata umaarufu mkubwa kwa sababu ukomo
wa unayoweza kuandika, ambao ni herufi 280 tu, huwezi kuandika zaidi ya hapo.
Hivyo ni vitu vifupi vifupi tu vinaandikwa huko, na kwa sababu watu hawataki
vitu virefu, wanafurahia sana mtandao huo.
Rafiki, kama hutumii mitandao hiyo ya kijamii kibiashara,
yaani kama huingizi fedha moja kwa moja kutoka kwenye mitandao hiyo, basi acha
kuitumia mara moja. Hakuna manufaa yoyote unayoyapata kwenye mitandao hiyo,
zaidi ya usumbufu, msongo na kupunguza umakini wako.
Jitoe kabisa kwenye mitandao yote ya kijamii, na ghafla
utaona jinsi ulivyo na muda mwingi wa kufanya yale muhimu kwako. Nilichukua
hatua hii mwaka 2018 baada ya kukaa kwenye mitandao hiyo kwa miaka 9 na
sijawahi kujutia maamuzi hayo.
(04 ). WATU
KUISHI KWA MAZOEA
NA KUFUATA MKUMBO.
Hivi umewahi kukaa chini na kujiuliza kwa nini unafanya kila
unalofanya? Umefanya kazi au biashara uliyonayo sasa kwa muda, lakini je unajua
kwa nini uliingia kwenye kazi au biashara hiyo? Unajua wapi unapotaka kufika?
Hata mengine unayofanya kwenye maisha, labda umechukua
mkopo, umejenga nyumba, umeoa au kuolewa, umewahi kujiuliza kwa nini ulifanya
maamuzi hayo?
Kwa bahati mbaya sana, maamuzi mengi ambayo watu wanafanya
ni kwa mazoea au kufuata mkumbo. Mtu anaambiwa wenzako wameshaoa au kuolewa, na
yeye anafanya hivyo. Mtu anaona wenzake wanachukua mkopo na yeye anachukua.
Maisha ya aina hii yamekuwa hayakosi changamoto, kwa sababu
mtu anahangaika na mengi lakini hayana maana kwake. Hivyo mwisho wa siku
anayaona maisha yake yakiwa tupu, anaweza kuwa na kila anachoambiwa anapaswa
kuwa nacho, lakini hana furaha.
Huwezi kuwa na furaha kwenye maisha kama hujayaishi maisha
yako, kama hujajijua wewe mwenyewe na kuishi kwa uhalisia wako. Unaweza kupata
kila ambacho wengine wanacho, tena wengine wakakuonea wivu kwa nafasi
uliyonayo, lakini ndani yako ukajiona ni mtupu.
Acha sasa kuishi maisha ya mazoea au kufuata mkumbo, kwa
kila jambo unalofanya, jua kwa nini unafanya. Kwanza kabisa jitambue wewe
mwenyewe, jua uimara na udhaifu wako, jua wapi unataka kufika na maisha yako.
Kisha hoji kila unalotaka kufanya linaendanaje na wewe na linakufikishaje kule
unakotaka kufika.
Usiogope kufanya kitu peke yako, usiogope kupingwa,
kukosolewa na kuchukiwa na wengine. Wewe pekee ndiye unayejijua kuliko wengine
wanavyokujua, chagua kuyaishi maisha yako na siyo kuwafurahisha wengine.
( 05 ). KUTEGEMEA
FURAHA KUTOKA KWNEYE
VITU VYA NJE.
Kama unajiambia ukishafika hatua fulani au kuwa na kitu
fulani ndiyo utakuwa na furaha basi jua unatembea na laana. Hiyo ni kwa sababu
hakuna furaha ya kudumu utakayoipata kwa kitu chochote cha nje yako. Unaweza
kupata raha ya muda mfupi, lakini siyo furaha ya kudumu.
Kutegemea furaha kutoka kwenye vitu vya nje imekuwa ndiyo
chanzo cha matatizo ambayo wengi wanakutana nayo kwenye maisha. Ulevi ambao
wengi wanaangukia ni kutafuta furaha za nje na za haraka, kitu ambacho kimekuwa
hakidumu.
Tambua kwamba furaha ya kweli na idumuyo inaanzia ndani
yako, inaanza na wewe mwenyewe na haitegemei chochote cha nje. Kama huna furaha
kabla hujapata unachotaka, hata ukikipata huwezi kuwa na furaha.
Mafanikio hayaleti furaha, bali furaha ndiyo inaleta
mafanikio. Hivyo anza na furaha, jitambue, jua wapi unakwenda, jipende, penda
unachofanya na kila siku piga hatua kuwa bora zaidi. Kwa njia hizi, utakuwa na
furaha bila kujali uko kwenye ngazi ipi.
Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo sababu kubwa tano za
changamoto nyingi tunazopitia kwenye maisha ya zama hizi. Tukiweza kutatua hizi
kwa kuzingatia yale tuliyojifunza, hakuna kitakachokukwamisha, utakuwa na
maisha tulivu, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo
mengine mazuri
ENDELEA KUSOMA HAPA "
MAISHA NA MAFANIKIO( LIFE AND YOU ) BLOG " KARIBU PIA UJIUNGE KATIKA " DARASA LETU--ONLINE " KWA KUWA MWANACHAMA.
Makala Hii Imeandikwa Na MWL. JAPHET
MASATU , Ambaye Ni MWALIMU
KITAALUMA , KOCHA WA MAISHA
NA MAFANIKIO , MSHAURI ,
MWANDISHI NA MJASIRIAMALI, PUBLIC SPEAKER
Tuwasiliane kwa WhatsApp + 255 716924136 / +
255 755 400128 / + 255 688361539