Tuesday, September 29, 2020

USIWE MTU MWEPESI WA KUUDHIWA NA WATU , HATUA 09 ZA KUSHINDA DHIDI YA MAUDHI AU ADHA.

Habari mwanafalsafa, wadau  wangu  wa  MAISHA NA  MAFANIKIO  BLOG ,

Karibu katika mwendelezo wa safari ya kujifunza falsafa ya Ustoa. Falsafa hii imekuwa ni falsafa yenye msingi mzuri wa kuzalisha maisha matulivu na bora. Wiki hii nimejiwekea utaratibu wa kuendelea kujifunza falsafa hii ya ustoa kupitia mwandishi Dr. Chuck Chakrapani ambaye kaandika mfululizo wa kazi nyingi za kistoa kwa kukusanya nukuu na misemo ya wastoa kama Seneca, Epictetus na Marcus. Kitabu cha awali nilishirikisha kama mapendekezo katika moja ya mijadala ya kifalsafa kupitia substack kiitwacho “STOIC INSPIRATIONS”. Ni kitabu kizuri sana kukisoma

Mbali na hicho kitabu kuna kingine ambacho nimekipitia na ndio msingi wa kuandika makala hii unayoisoma. Kitabu hiki kinaitwa “UNSHAKABLE FREEDOM” kwa tafsiri iso rasmi inatafsiriwa kama “UHURU USOTIKISWA”. Uhuru ni hitaji mama la mtu yeyote yule sehemu yoyote Duniani. Uhuru unalindwa na uhuru wa maisha ni katika kujua mambo yapo makundi mawili; Mosi, ni yale yalo katika uwezo wako na pili yalo nje ya uwezo wako. Kitabu hiki kinagusa namna unavyoweza kuwa na uhuru usotikiswa. Kuudhiwa ni njia rahisi inayoweza kuharibu uhuru wetu katika maisha na usipokuwa na msingi wa falsafa utaishi kuamua ovyo.

Kuudhiwa kunaweza kukufanya ujisikie vibaya, upandwe na hasira na tatu unakupotezea utulivu wa akili na wakati mwingine mwili. Ila si vile ambavyo Marcus Aurelius anatushauri kuwa tuumie au tupandwe na hasira la hasha ila kutusaidia kuwa na utulivu pale tunapopitia hali ya kuudhiwa na watu wanaotuzunguka. Marcus Aurelius kaziweka kama hatua 09 za kufuata ili kwa lolote litakalojitokeza la kutuudhi basi tusipoteze utulivu wetu wa ndani.

Hatua hizi 09 zimegawanyika katika makundi mawili. Mosi ni hatua 04 za awali ambazo ni maswali 04 ya kujiuliza unapopitia hali ya kuudhiwa na pili ni hatua 05 za mwisho ambazo ni makumbusho/ tafakari kuhusu hali unayopitia ya kuudhiwa na mtu au matukio maishani.

Jiulize haya; [ Haya ni maswali ambayo Marcus Aurelius anatupa mwongozo wa kujiuliza pale ambapo tunakuwa kati kati ya hali za kuudhiwa au dakika chache ya tendo la kuudhiwa limejitokeza ]

1.       Usizidishe ukali wa tatizo- Je ni mahusiano gani ninayo na huyu mtu?

mfano mtu aliyekukosea ni ndugu yako wa karibu, mfanyakazi wako, mke au mume wako. Ukiondoa upande wa kosa ambalo limejitokeza la kukufanya uudhike ila upande mwingine mzuri huyo mtu ni ndugu yako, mfanyakazi wako, mke au mume wako. Unaporuhusu kuona mahusiano ya mtu aliyekutendea kosa unakuwa katika nafasi ya kupunguza ukubwa wa tatizo au tukio lilojitokeza.

2.       Jitahidi kufahamu nini msukumo wa mtu kufanya hivyo;

Mtu anapotenda kitu usifanye haraka kutoa hukumu maana unazibwa na kutokujua kwa kina, je nini ni msukumo wa jambo alotenda. Ukiangalia kwa kina unaweza kuona msukumo wa kutenda jambo hilo. Huenda ni msukumo wa chuki, ujinga, wivu au wakati mwingine kutokukusudia.

3.       Itafakari hali ilojitokeza

Usiwe na haraka ya kilichotokea kukipa tafsiri. Vuta ukimya na kuwa tayari kuona hali ilojitokeza imechangiwa na nini. Utaona pengine kuna nafasi ya ujinga kuwepo ndo maana tukio hilo limejitokeza. Usitoe mwitikio haraka tukio linapojitokeza.

4.       Hebu jiangalie hujawahi watendea wengine ulofanyiwa ?

Ni rahisi sana kuona watu wanaotuudhi wanamakosa zaidi na tukasahau hata sisi kuna watu wengi tunawaudhi kwa mambo yetu. Mimi na Wewe ni bado wanadamu na tuna mapungufu mengi kama wengine. Wanapokosea wengine tuwe waelewa kama ambavyo nasi tunavyotaka watu wengine watuelewe.

Jikumbushe haya; [Haya ni mambo ya kujikumbusha ambayo Marcus Aurelius anatupa mwongozo wa kujikumbusha pale ambapo tunakuwa kati kati ya hali za kuudhiwa au dakika chache ya tendo la kuudhiwa limejitokeza]

5.       Jua kuwa huna picha kamili ya jambo lilivyo

Wakati mwingine tunaona vitu kwa picha ndogo kuliko uhalisia ulivyo. Huwezi jua mtu aliyekukosea kwa wakati huo ni mambo gani anayoyapitia, au ni mambo yepi yalochangia yeye kufanya hivyo. Utaona mambo mengi ya watu walokosea ukichimba kwa kina kuna baadhi ya taarifa hatukuweza kuzijua kwanini hilo limejitokeza. Kila tukio linapotokea jua kuwa huna picha kamili ya mambo yalivyo. Usifanye haraka kutoa hukumu.

6.       Kumbuka Maisha ni mafupi

Miaka 200 toka sasa na kuifikiria ijayo hatutakuwepo; hii ikiwa ina maana wewe unayesoma hii makala miaka 200 ijayo sote hatutakuwepo. Hili linadhihirisha maisha yalivyo mafupi na hatupaswi kuhifadhi hasira au chuki na mtu yeyote yule. Kwa kujua hili unakazana kuishi katika kuchagua furaha kuliko kitu kingine chochote.

7.       Jua maoni ya mtu mwingine hayana nguvu dhidi yako endapo utapuuza au kuzuia kuyapa tafsiri

Kinachotuumiza sana siku zote kwa watu wanaotuudhi, wanaotutukana ni juu ya kuyapa tafsiri yale ambayo wamesema. Kuyapa tafsiri ni kuruhusu waloyasema yawe na nguvu dhidi yetu. Kwa kuona hilo Marcus anatushauri kutoyapa tafsiri au tukiweza tuyapuuze.

8.       Jua hasira ukiijenga itakuumiza zaidi ndani yako

Hasira inaunguza kama mtu aliye na kaa la moto katika kiganja. Ukiudhiwa na ukajenga hasira ndani yako, hasira inaanza kukuumiza wewe na pengine aliyekuudhi hana mpango wowote wa kukuwazia wewe. Hasira isiruhusiwe idumu ndani yako.

9.       Ukiweza tabasamu

Hakuna kitu kinachomfanya mtu aliyekuudhi au kukutukana pale unapotabasamu na wakati mwingine kucheka kwa kile alichokifanya. Inaonesha kwako kuwa alichokifanya hujakipa nguvu na pengine kukidharau. Lengo la mtu wakati mwingine kukutusi ni kutegemea kuona umekasirika, sasa unapokuwa unacheka unampa aumie zaidi kuona alichotegemea hakijafanikiwa.

Hizi hatua 09 ni mwongozo mzuri unaoweza kuutumia kila inapoitwa leo unapoendelea kukutana na watu mbalimbali. Maisha ya kila siku hatutaacha kukutana na watu ambao kwa namna moja wataleta adha dhidi yetu. Tutumie huu msingi kulinda utulivu wetu wa ndani maana tukumbushe maisha yetu ni mafupi.

 

4 comments: