Tuesday, September 29, 2020

KILA SIKU NI YA PEKEE SANA , ISHI KAMA LEO NA USIIPOTEZE.

Wanasema unaweza kulalamika huna viatu, ila ni mpaka siku utakayokutana na mtu asiye na miguu ndiyo utakumbuka kushukuru kwamba angalau wewe una miguu na hivyo viatu haviwi tatizo tena kwako.

Ni kawaida kwetu binadamu kuzoea vitu tulivyonavyo na kuvichukulia kawaida, kwa sababu tumekuwa tunaviona kila siku. Lakini vitu hivyo hivyo tunavyovichukulia pia, kuna wengine wanavitamani kweli ila hawawezi kuvipata.

Moja ya vitu hivyo ni hizi siku tunazokuwa nazo kila siku, tangu umezaliwa mpaka hapo ulipofika sasa, umekua unaanza na kumaliza siku zako na hivyo umeshazoea, asubuhi unaamka, unaenda na shughuli zako na siku inaisha, unalala na kuamka tena siku inayofuata.

Kwa kuwa umeshazoea sana siku zako, umekuwa unajiaminisha kabisa kwamba kesho ipo na huchelewi kuacha kufanya kitu leo kwa kujiambia utafanya kesho. Ni kitu gani kinakupa uhakika kiasi hicho?

Unapopata habari za misiba ya watu wa karibu, wale ambao uliwajua na walikuwa na mipango mikubwa ila wamefariki ghafla, huwa unapata mshtuko, unaona kweli maisha ni mafupi. Lakini haikuchukui siku nyingi unarudi kwenye mazoea yako, unazichukulia siku zako poa na kuahirisha mambo.

Tunawezaje kuondokana na hali hii ili tuweze kuzipa siku zetu uzito unaostahili na kuishi kwa ukamilifu?

Mwanafalsafa Seneca ana mengi ya kutueleza kwenye hili. Kwenye moja ya barua alizoandika kwa rafiki yake Lucilius akimweleza kuhusu wengi wanavyokihofia kifo, aligusia hili la kuishi kila siku kwa mazoea.

Seneca anasema wengi wamekuwa wakijiuliza maisha yao yataenda hivyo mpaka lini, kila siku kulala na kuamka, kuwa na njaa na kushiba, majira ya masika na kiangazi. Kwa kuyatazama maisha hivyo unaona kama ni mzunguko, hakuna kipya, kila kitu kinajirudia.

We slip into this condition, while philosophy itself pushes us on, and we say; "How long must I endure the same things? Shall I continue to wake and sleep, be hungry and be cloyed, shiver and perspire?  There is an end to nothing; all things are connected in a sort of circle; they flee and they are pursued.  – Seneca

Seneca anatutahadharisha kwamba tukiyaangalia maisha kwa mtazamo huo, tutayaona maisha ni maumivu yasiyo na mwisho, unaimaliza leo ukijua kesho inakwenda kuanza na kuisha kama leo. Majira ya masika yanaisha ukijua kiangazi kinakuja. Una njaa na kutafuta chakula kizuri kula, ila ukishashiba unajua kuna njaa itakuja tena. Kwa namna hii, maisha yanakuwa kama gereza la mateso, kusukuma siku usubiri kufa.

Lakini ipo namna nyingine ya kuyaangalia maisha kwa namna ambayo yatatunufaisha, mtazamo wa tofauti unaotusukuma kuyaishi maisha yetu kwa ukamilifu. Mtazamo huo ni kuyaona maisha kama zawadi, kila siku mpya unayoipata inakuwa kama nyongoza na hivyo unaitumia vizuri zaidi.

There are many who think that living is not painful, but superfluous. – Seneca.

Unapoiona siku mpya unayoianza kama nyongeza, unaitumia vizuri kwa sababu unajua huna uhakika kama utaiona siku nyingine kama hiyo. Huangalii jana ulifanya nini maana imeshapita, na wala huangalii kesho itakuwaje maana haipo, unachoangalia ni zawadi iliyo mbele yako.

Tukiweza kuziishi siku zetu kwa mtazamo huu, tutaacha kuona marudio yanayotuumiza na tutaanza kuona vitu vizuri vya kufanyia kazi.

Mahali pengine Seneca amewahi kutuasa jinsi ya kuziishi siku zetu kwa ukamilifu, mfano ni nukuu hizi;

“Anza kuishi mara moja na ichukulie kila siku mpya kama maisha tofauti.”

“Nitaendelea kuyaangalia maisha yangu na muhimu zaidi nitaitathmini kila siku yangu kwa kufunga vitabu vya maisha kila siku.”

Kama kauli za Seneca zinavyosisitiza, usichukulie poa hii siku uliyonayo leo, kuna wengine wangetamani sana kuwa nayo lakini haijawezekana. Iishi kwa upekee wake, ipangilie vizuri na fanya mambo ambayo mwisho wa siku ukiyaangalia unajiambia kweli umeiishi siku hii.

Kila unapoimaliza siku yako, jifanyie tathmini, pitia kila ulichofanya tangu kuamka mpaka unaporudi kulala na kisha jiulize maswali haya matatu;

Moja; Ni yapi mazuri nimefanya leo na ambayo nitaendelea kuyafanya nikipata zawadi ya siku nyingine?

Mbili; Ni yapi mabaya nimefanya leo ambayo sitarudia tena kufanya kama nitazawadiwa siku nyingine?

Tatu; Yapi ambayo sijayafanya kwa ubora unaostahili na ambayo nitayaboresha zaidi nitakapopata zawadi ya siku nyingine?

Ukijiuliza maswali hayo matatu kila siku na kujipa majibu sahihi, kisha kuyafanyia kazi, maisha yako yatakuwa bora, hutazichoka siku zako, hutaahirisha chochote na utayazuia matatizo mengi kabla hayajawa makubwa.

Wenye hekima wanajua, maisha siyo mateso bali zawadi, ichukulie hivyo na utakuwa na maisha bora na tulivu.

 

No comments:

Post a Comment