Kinachowatofautisha
wale wanaofikia ubobezi na wale wanaoishia kuwa kawaida siyo
wanachofanya, bali namna wanavyofanya kile wanachofanya. Watu wawili
wanaweza kuwa wanafanya kitu kimoja, lakini mmoja akabobea na mwingine
asibobee.
Mwandishi anatuambia zipo aina tatu za ufanyaji ambazo zinawatofautisha wanaobobea na wanaokuwa kawaida.
Aina
ya kwanza ni kufanya kwa kawaida, hapa mtu anafanya kile ambacho
amezoea kufanya kila wakati, hakuna kipya anachofanya na hivyo hawezi
kubobea. Hivi ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao, wanaonekana
kufanya sana lakini hakuna hatua wanapiga. Hii ni kwa sababu wanafanya
kwa mazoea.
Aina
ya pili ni kufanya kwa malengo, hapa mtu anafanya kitu kwa malengo, na
hivyo anakuwa na hatua anazopanga kupiga zinazomsukuma kufanya zaidi.
Katika kufanya kwa malengo mtu anapiga hatua zaidi kwa sababu malengo
anayojiwekea yanamsukuma zaidi. Kwenye kufanya kwa malengo mtu anakuwa
na sifa nne; moja anakuwa na lengo la wapi anataka kufika, mbili anaweka
umakini wake wote kwenye kile anachofanya. Tatu anakuwa na njia ya
kujipima na kupata mrejesho wa hatua anazochukua na nne anajisukuma
kutoka nje ya mazoea, kufanya vitu vipya ambavyo vinamwezesha kupiga
hatua zaidi.
Aina
ya tatu ni kufanya kwa makusudi, kama mwandishi anavyoita DELIRATE
PRACTICE, hapa mtu anakuwa na kusudi kubwa linalomsukuma kufanya kitu.
Hii ndiyo aina ya ufanyaji ambayo inazalisha watu wenye ubobezi wa hali
ya juu. Kufanya kwa makusudi kuna sifa kama za kufanya kwa malengo,
lakini ina sifa nyingine mbili za nyongeza. Ya kwanza ni eneo ambalo mtu
anakuwa amechagua kubobea linapaswa kuwa na wabobezi ambao wanaweza
kuangaliwa na mtu akajifunza kwao. Mtu anapoweza kuwaangalia wabobezi na
kujifunza kile wanachofanya na namna wanavyofanya, inakuwa rahisi kwake
naye kufanya. Sifa ya pili ni kuwa na mwalimu au kocha ambaye
anamfundisha na kumsimamia mtu kwenye hatua anazochukua. Kwa kuwa na mtu
wa nje anayetoa maelekezo au kupima hatua mtu anazochukua na kutoa
mrejesho, kunamfanya mtu apige hatua kubwa zaidi.
Hizo
ndizo aina tatu za ufanyaji na aina ya tatu ndiyo mwandishi ameijadili
kwa kina sana kwenye kitabu cha PEAK.
No comments:
Post a Comment