Kwa miaka mingi watu wamekuwa wakiamini kwamba kuna watu ambao
wamezaliwa na vipaji ambavyo vimewawezesha kufikia kwenye ubobezi mkubwa
ana katika maeneo waliyobobea.
Na
mifano ipo mingi sana, kwenye utunzi wa nyimbo na upigaji wa vyombo,
Morzat anaonekana kuwa mmoja wa watu wenye kipaji kikubwa. Kadhalika
kwenye mchezo wa golf, Tiger Woods anaonekana kuwa mchezaji ambao ana
kipaji kikubwa kwenye mchezo huo. Na hata michezo mingine na hata kwenye
taaluma mbalimbali, wale ambao wamefanikiwa sana wanaonekana kuwa na
kipaji kikubwa.
Lakini
unapokwenda kuchimba ndani, na kuangalia kwa undani maisha ya wale
wanaosemekana wana vipaji, huoni kipaji bali unaona juhudi kubwa na za
muda mrefu. Katika mifano niliyotoa hapa, Morzat ambaye anaonena alikuwa
na kipaji, alianza kufundishwa kupiga vyombo vya muziki akiwa na miaka
minne, ana akawa anafanya hivyo kila siku. Huyu ni mtoto ambaye alikuwa
akijua kufanya kitu kimoja tu, muziki. Je utamlinganisha na mtu mwingine
anayekuja kujifunza muziki ukubwani?
Ukiangalia
kwa Tiger Woods pia, wazazi wake wanakiri kumpa michezo ya kitoto
inayoendana na mchezo wa golf tangu akiwa na miezi tisa, huyu ni mtu
ambaye tangu anapata utambuzi wake, anajua kitu kimoja tu, golf, je
utaweza kumshindanisha na mtu mwingine ambaye amejua mchezo huo baadaye?
Chagua
mtu yeyote unayeamini ana kipaji, iwe ni mchezaji, mwanasayansi na hata
kiongozi, na angalia maisha yake tangu utotoni, utagundua kuna
mazingira ambayo yalimweka kwenye juhudi ambazo zilimwandaa kufikia
ubobezi huo. Hata wachezaji wenye ubobezi mkubwa kama Christiano Ronaldo
na Messi, ukiangalia utoto wao, wametumia sehemu kubwa kwenye kujifunza
mchezo wa mpira. Angalia maisha ya wanasayansi kama Eistein, Newton na
wengineo, wote waliweka muda na juhudi kubwa kabla hawajafikia ubobezi
ambao wengi wanakuja kuamini ni vipaji vimewafikisha pale walipo.
Hivyo
ujumbe kwako rafiki yangu ni huu, unaweza kubobea kwenye jambo lolote
lile, kama tu utaweka juhudi ambazo zinapaswa kuwekwa ili kufikia
ubobezi. Na kwenye kitabu cha juma hili cha PEAK, tunakwenda kujifunza
juhudi sahihi unazopaswa kuweka ili kufikia ubobezi.
Usijiambie
tena kwamba huwezi kufikia ubobezi kwa sababu huna kipaji au uwezo.
Tafiti zote ambazo zimefanywa kwenye ubobezi zimekuja na jibu moja, wale
wanaofikia ubobezi wana uwezo mkubwa sana, lakini ni uwezo ambao upo
ndani ya kila mmoja wetu. Kinachotutofautisha sisi na wale waliobobea
sana ni kiasi ambacho tumeendeleza uwezo ambao upo ndani yetu.
Uwezo tayari unao, unachohitaji ni juhudi ili kubobea, aina gani ya juhudi utakwenda kujifunza kwenye kitabu cha juma.
No comments:
Post a Comment