(1).LENGO LINAPASWA KUWA MAALUMU (SPECIFIC).
Kigezo cha kwanza muhimu kwenye kuweka
malengo ambayo utayafikia ni umaalumu wa lengo husika. Unapaswa kuweka
lengo ambalo linaeleweka ni nini hasa unachotaka.
Unapaswa kujua ni nini kwa hakika
unachotaka kwenye lengo hilo, unakipata wapi, utashirikiana na nani, kwa
nini unakitaka na hatua zipi unapaswa kuchukua.
Tukienda kwenye mfano wetu wa fedha,
usiweke lengo kwamba nataka fedha zaidi, au nataka kuwa bilionea.
Unapaswa kuweka kiasi cha fedha unachotaka na kujua utakipataje kwa
hatua zipi unazopaswa kuchukua.
Utaona tofauti kubwa kati ya hali hizo
mbili, unaposema unataka fedha zaidi, ukipata elfu kumi ambayo hukuwa
nayo ni fedha zaidi. Lakini unaposema unataka milioni 50 au bilioni
moja, hapo sasa unakuwa na uhakika nini unataka.
Usiweke malengo yanayoelea hewani, jua
kabisa nini unataka na nenda mbali zaidi kujua unakipataje na kwa
kufanya nini. Pia unapaswa kuwa na kwa nini inayokusukuma kufikia lengo
hilo.
(2). LENGO LIPIMIKE (MEASURABLE).
Kigezo cha pili kwenye kuweka malengo
utakayoweza kuyafikia ni kila lengo linapaswa kuwa linapimika. Hapa
unapaswa kuona kabisa ni jinsi gani kupata kile unachotaka kutabadili
maisha yako.
Pia unapaswa kuligawa lengo lako kubwa
kwenye hatua ndogo ndogo ambazo unaweza kuzitumia kupima maendeleo yako
kwenye lengo hilo.
Kwa mfano kama lengo lako ni kupata
milioni 50 kwa mwaka, unaweza kuligawa kwa miezi 12 na ukapata kama
milioni 4 kwa mwezi, hii inakuwa rahisi kwako kujipima kila mwezi kuona
unaelekeaje kwenye lango lako.
Kuweza kuligawa lengo lako kubwa kwenye
hatua ndogo ndogo zinazopimika kutakuondolea kukata tamaa pale lengo
linapoonekana ni kubwa sana.
Hakikisha kila lengo unaloweka unaweza
kupata taswira ya ukiwa umelikamilisha kisha ligawe kwenye hatua ndogo
ndogo ambazo ni rahisi kwako kupima.
(3). LENGO LIWE NINAFIKIKA (ATTAINABLE).
Kigezo cha tatu ni lengo liwe
linafikika. Tumekuwa tunayaelewa sana mafunzo ya maendeleo binafsi
ambayo yanatufundisha kwamba ndani yetu tuna uwezo mkubwa na tunaweza
kufanya chochote tunachotaka kufanya. Hili ni kweli kabisa kwamba tuna
uwezo mkubwa na kuweza kufanya chochote tunachotaka.
Lakini inahitaji muda, nguvu na hata
vipaji kufikia lengo lolote tunalojiwekea. Hivyo unapoweka lengo, lazima
ujiulize je kwa muda, nguvu, rasilimali na hata vipaji ulivyonavyo
utaweza kufikia lengo hilo? Kama siyo unajidanganya.
Kwa mfano kama mwaka huu kipato chako ni
shilingi milioni moja kwa mwezi, kujiambia kwamba mwaka kesho unataka
upate bilioni moja ni kujidanganya na kujiandaa kushindwa. Ni kweli
lengo la bilioni moja linafikika, lakini linachukua muda, na linahitaji
jitihada zaidi.
Kwenye kila lengo unalojiwekea, angalia
rasilimali ulizonazo kisha weka lengo kubwa ambalo litakusukuma, lakini
lisikukatishe tamaa.
(4). LENGO LIWE NA UHUSIANO NA KUSUDI LA MAISHA YAKO (RELEVANT).
Kigezo cha nne kwenye kuweka malengo
utakayoyafikia ni lengo liwe na uhusiano na kusudi la maisha yako. Mara
nyingi wengi wamekuwa wanaweka malengo ambayo siyo yao. Kwa sababu
wamesikia wengine wakiweka malengo hayo basi na wao wanaona inabidi
wayaweke la sivyo wataachwa nyuma.
Watu wengi wamekuwa wanafuata mkumbo
kwenye uwekaji wa malengo, wanaweka malengo ambao hayahusiani kabisa na
lile kusudi walilonalo kwenye maisha. Wanapokuja kugundua hili
wanashindwa kuendelea na malengo yao.
Kwenye kila lengo unalojiwekea,
hakikisha linaendana na kusudi kubwa la maisha yako. Hata kama ni lengo
kubwa kiasi gani, kama halitokani na kusudi lako kubwa, utaishia
kushindwa.
Usijiambie unataka kupata mabilioni ya
fedha kupitia biashara fulani ambayo inaonekana kuwa yenye faida kubwa,
wakati wewe unapenda kufanya kitu kingine tofauti kabisa. Lengo
unaloweka liendane na kile unachopenda na kujali kufanya.
(5).LENGO LIWE NA UKOMO WA MUDA (TIMELY).
Kigezo cha tano katika kuweka malengo
ambayo utayafikia ni kuwa na ukomo wa muda. Wote tunajua jinsi ambavyo
ukomo wa muda unavyotusukuma kuchukua hatua. Watu wanaweza kupewa nafasi
ya kufanya kitu kwa muda mrefu lakini wasifanye, inapofikia tarehe ya
ukomo ndiyo kila mtu anafanya.
Tumia nguvu hii ya ukomo wa muda kwenye
malengo unayoweka, kila lengo liwe na ukomo wake wa muda na ujikumbushe
ukomo huo ili uweze kujisukuma kufanya zaidi na kufikia lengo hilo.
Kwenye kila lengo ulilogawa kwenye hatua ndogo, jiwekee ukomo kwenye
kila hatua na ufuate ukomo huo.
Kama umejiambia unataka kupata bilioni
moja ndani ya miaka kumi, basi gawa kiasi cha kupata kila mwaka, kila
mwezi, kila wiki na hata kila siku, kisha weka muda wa kufuatilia kila
kiwango unachotaka kupata ili kuona maendeleo yako yakoje.
Rafiki, hivyo ndivyo vigezo vitano
muhimu unavyopaswa kuvitumia kuweka malengo ambayo kwa hakika
utayafikia. Tumia vigezo hivi katika kila lengo unaloweka na utaona
jinsi utakavyolielewa lengo lako vizuri, kuona kila hatua unayopaswa
kuchukua na kuwa na msukumo wa kuchukua hatua kabla muda uliojiwekea
haujaisha.
BADILI FIKRA.FIKIRI TOFAUTI .BADILI MAISHA.JITAMBUE .JIFUNZE ELIMU YA SAIKOLOJIA,TEOLOJIA , FEDHA ,UTAMBUZI(SELF HELP EDUCATION),FALSAFA YA MAISHA,MAISHA NA MAFANIKIO,BIASHARA / UJASIRIAMALI.FURAHIA WASAA WAKO NA MAISHA NA MAFANIKIO BLOGU.THIS IS THE COMMUNITY CAPACITY BUILDING BLOG.ENJOY THE BLOG.STRETCH YOUR MIND. YOU CAN CHANGE YOUR LIFE FOR EVER. YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment