Wednesday, December 5, 2018

TEGEMEA NGUVU ZAKO NA SIYO HURUMA ZA WENGINE.

Kwenye MAISHA, kwa chochote unachochagua kufanya basi unapaswa kutegemea zaidi nguvu zako, uimara wako na siyo kutegemea huruma za wengine. Kila unapoanza kutegemea huruma za wengine, ndipo unapoingia kwenye shimo zaidi na kukosa uhuru wako.
 
Kila unapokuwa unategemea wengine wafanye kitu ndiyo wewe uweze kupata unachotaka, utajikuta unakosa uhuru wa kuishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
 
Kwa sababu yeyote yule unayemtegemea sana, ambaye huwezi kupiga hatua fulani bila yeye, anageuka na kuwa kikwazo kwako, kwa sababu asipofanya kama unavyotegemea, basi wewe hutaweza kupata kile unachotaka kupata.
 
Unapaswa kuyatengeneza maisha yako kwenye msingi huu wa KUJITEGEMEA binafsi kwenye mambo mengi ya maisha yako, kujua namna ya kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kutoruhusu mtu mmoja au watu wachache wawe na maamuzi ambayo yanaweza kuathiri sana maisha yako.
 
Kama maisha yako yanategemea sana maamuzi ya mtu mmoja au watu wachache, utakosa uhuru mkubwa kwenye maisha yako, kwa sababu hata kama mtu huyo hakusumbui, bado ndani yako utakosa amani, kwa sababu hujui ni namna gani mtu huyo anaweza kubadilika siku za mbeleni.
 
Maisha ya uhuru kamili, maisha ya kupata kile unachotaka ni kuweza kutumia uwezo wako mkubwa, kutengeneza maisha ambayo hayana utegemezi mkubwa kwa mtu mmoja au watu wachache. Hilo linajumuisha hata wewe binafsi.
 
Kwa mfano kama kipato chako kinategemea wewe ufanye kazi, bado hujawa huru, kama huwezi kuingiza kipato hata kama wewe hufanyi kazi, unaendelea kuwa mfungwa kwenye upande wa kipato. Lazima uwe na mfumo huru unaoweza kutengeneza kipato iwe unafanya kazi au la.
 
Una uwezo mkubwa sana ndani yako, una nguvu kubwa sana ambazo kama utaanza kuzitumia, utayabadili sana maisha yako, utawafanya wengine wakutegemee wewe zaidi kuliko unavyowategemea wao. Na kadiri wengi wanavyokutegemea wewe, ndivyo unavyokuwa huru zaidi.
 
Na hili ni zuri na muhimu sana kwa wale watu ambao wanapenda kufanya kazi zao za ajira, lakini wanapenda kuwa huru. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anapenda kufanya kazi fulani, lakini ataifanya vizuri kama atakuwa ameajiriwa sehemu fulani. Kwa mtu huyu kutumia vizuri uwezo wake mkubwa na nguvu zake, anajitengenezea hali ya kutegemewa kwenye kile anachofanya, kitu ambacho kinamfanya aheshimiwe na kuwa na uhuru zaidi kuliko wale ambao hawategemewi na badala yake wanategemea zaidi kazi wanayofanya

No comments:

Post a Comment