1.
Anzia sokoni, wengi huanza kufanya kitu kwa mapenzi yao wenyewe na siyo
mapenzi ya soko. Kama unataka kufanikiwa, anza kujua watu wanataka nini
kisha wape hicho wanachotaka.
2. Usiogope
kushindwa, kabla hujafanikiwa, utakutana na vikwazo na changamoto
mbalimbali, utashinda kwenye mengi, lakini kama hutakata tamaa, mwishowe
utashinda.
3. Gundua fursa zilizojificha kwenye majanga mbalimbali. Unapokutana
na majanga au changamoto, usiangalie upande wa matatizo, badala yake
jiulize ni fursa gani iko hapa, na utaziona fursa nyingi zilizojificha
kwenye majanga.
4. Toa thamani kubwa kwa wateja wako, wateja wataendelea kununua kwako kama kuna thamani wanaipata. Hakikisha mteja hakusahau kabisa, kwa namna unavyompa thamani ya kipekee.
5. Amka asubuhi na mapema, hii ni tabia moja ambayo itakupa ushindi mkubwa sana kwenye siku yako. Unapoamka mapema kuliko wengine na ukatumia muda huo kwa maandalizi na kufanya yaliyo muhimu, utaweza kupiga hatua sana.
6. Tenga muda wako na fanya jambo moja kwa wakati. Watu
wengi huwa wanafikiria kufanya mambo mengi kwa pamoja ni kuokoa muda,
lakini matokeo ni kinyume, kadiri mtu anavyofanya mengi kwa pamoja,
ndivyo anavyopoteza muda na umakini wake. Kama unataka kukamilisha mengi, tenga muda wako na kisha fanya jambo moja kwa wakati.
7. Fanya mambo yanayoendana pamoja. Unapopanga
ratiba ya kufanya vitu vyako, vile vitu ambavyo vinaendana, panga
kuvifanya pamoja, hasa pale vitu hivyo vinapokuwa havihitaji umakini
mkubwa. Kwa njia hii inakuwa rahisi kwako kukamilisha yale yanayoendana. Na
hii haipingani na namba sita ya kufanya jambo moja kwa wakati, ila hapa
unayaweka pamoja yale yanayoendana ili uweze kuyakamilisha.
8. Kuwa na mapumziko ya mara kwa mara. Kazi zetu nyingi tunafanya tukiwa tumekaa, hili linaleta uchovu na pia ni hatari kiafya. Suluhisho
ni kuwa na mapumziko ya mara kwa mara ambapo unasimama na kutembea
kidogo au kujinyoosha kabla ya kuendelea na jukumu jingine.
9. Kuwa na orodha mbalimbali, popote unapokuwa, kuwa na orodha unayofanyia kazi. Na
unapopata wazo jipya, liandike mahali, usiamini kumbukumbu zako,
utaishia kusahau mengi au kuijaza akili yako vitu visivyo muhimu kwenye
kile unachofanya kwa wakati huo.
10. Weka malengo ambayo unaweza kuyafanyia kazi, malengo yanayopimika na unayoweza kuona ni wapi unakwenda na unafikaje pale. Bila ya malengo unayoweza kufanyia kazi, hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
11.
Tumia vizuri muda wa uzalishaji mkubwa kwako. Kila mmoja wetu ana muda
ambao anakuwa na uzalishaji mkubwa sana. Huu ni muda ambao akili ya mtu
inakuwa inafikiri kwa umakini na mwili unakuwa na nguvu ya kutosha. Jua
ni wakati gani wa siku unakuwa kwenye hali hii kisha weka yale majukumu
muhimu kwenye muda huo.
12. Pima maendeleo yako kibiashara kwenye yale maeneo muhimu. Kila biashara ina maeneo yake muhimu, ambayo hayo yakienda vizuri basi biashara inakuwa ya mafanikio makubwa. Yajue maeneo muhimu kwenye biashara yako kisha pima maendeleo yako, pima hatua unazopiga ukilinganisha na malengo uliyojiwekea. Hii ndiyo njia rahisi ya kupima hatua unazopiga.
13. Epuka kujilisha vitu visivyo na maana. Habari, mitandao ya kijamii na kelele nyingine zimekuwa zinachukua muda wa wengi na wanashindwa kufanya yale muhimu. Epuka kujilisha vitu hivyo visivyo na maana na tumia muda wako kwa yale majukumu muhimu kwako.
14.
Tengeneza muda wa kujitenga na teknolojia. Teknolojia zinarahisisha
sana maisha, lakini pia zimekuwa usumbufu mkubwa sana kwenye maisha
yetu. Tenga
muda ambao utajitenga na teknolojia hizi, ili uwe na utulivu
unaokuwezesha kufikiri kwa kina na hata kutekeleza majukumu ambayo ni
muhimu kwako, yanayohitaji utulivu wa hali ya juu.
15. Weka mkazo kwenye uimara wako. Kuna
maeneo ambayo una uimara na maeneo ambayo una udhaifu, unachopaswa
kufanya ni kuweka mkazo kwenye uimara wako kuliko kukazana na madhaifu
wako. Tafuta wenye uimara kwenye madhaifu wako na wape wafanyie kazi maeneo hayo.
16.
Jitofautishe na wengine. Ukifanya kile ambacho wengine wanafanya
utapata wateja wa kawaida. Ukifanya kile ambacho hakuna mwingine
anayefanya utapata wateja wengi na wakipekee. Unapaswa kujitofautisha kabisa na wengine ili kupata wateja wa kipekee, ambao wanakuwa mashabiki wa biashara yako.
17.
Tumia vizuri muda uliokufa kujifunza na kupiga hatua. Moja ya hitaji la
kila mjasiriamali ni kuendelea kujifunza na kupiga hatua zaidi. Lakini
mahitaji ya kila siku yanamfanya mtu akose kabisa muda wa kujifunza. Pamoja na majukumu mengi unayoweza kuwa nayo, bado kuna muda mwingi unaokuwa nao ambao huwezi kufanya chochote. Huu ndiyo muda uliokufa. Mfano
muda unaokuwa kwenye foleni barabarani au kusubiri huduma fulani, muda
unaofanya mazoezi au kufanya kazi zisizohitaji umakini mkubwa. Unaweza kutumia muda huo kujifunza zaidi.
18. Soma kwa dakika 30 kila siku. Huwezi kupiga hatua kama husomi na kujifunza, hivyo kila siku tenga angalau dakika 30 ambazo utazitumia kusoma.
Na linda muda huo usiupoteze kwa kingine chochote. Hata kama una mengi
kiasi gani, usikose kutenga muda wa kujisomea, ni muhimu sana kwa ukuaji
wako.
19. Jifunze ujuzi mpya unaoweza kuutumia kuikuza biashara yako zaidi. Pamoja na kusoma kila siku, unahitaji kujifunza na kuongeza ujuzi ambao utaweza kuutumia kupiga hatua zaidi kibiashara. Biashara
zinabadilika kila siku, ushindani unazidi kuwa mkali, unapaswa kuwa na
ujuzi wa ziada ambao utakuwezesha kupiga hatua zaidi.
20. Kamata mawazo bora yanayokujia kwenye siku yako kwa kuyaandika chini kabla hujayasahau. Unaweza kufanya hivi kwa kuwa na kijitabu kidogo na kuandika, au pia unaweza kutumia simu yako kuandika mawazo unayokutana nayo. Usikubali wazo lolote linalokujia likupotee.
21.
Tengeneza na kuza mtandao wako. Huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe,
unahitaji msaada wa wengine ili kuweza kufanikiwa. Hivyo unahitaji
kutengeneza na kukuza mtandao wako wa kibiashara. Utengeneze mahusiano bora na wafanyabiashara ambao wanapiga hatua zaidi ambao watakusukuma na wewe upige hatua zaidi.
22. Timiza ahadi unazotoa. Njia rahisi ya kuwapoteza wateja kwenye biashara ni kuwaahidi vitu halafu usivitekeleze. Jijengee
sifa nzuri kwenye biashara yako kwa kuwa mtekelezaji wa kila
unachoahidi, kwa kufanya hivyo wateja wanakutegemea na kukuamini.
23. Tumia nguvu ya HAPANA. Kinachowafanya wengi kushindwa kutimiza ahadi wanazotoa ni kusema NDIYO haraka bila ya kufikiri kwa kina. Kadiri unavyokubali mambo mengi, ndivyo unavyotawanya muda na nguvu zako na ufanisi wako unashuka.
Jifunze kusema HAPANA ili kuweka mkazo kwenye yale maeneo muhimu ya
biashara yako. Kama kitu siyo muhimu sema HAPANA, na usione aibu waka
kuogopa.
24. Kuwa kiongozi na siyo meneja. Unapowaajiri
watu wakusaidie kazi kwenye biashara yako, kuwa kiongozi kwa
kuwahamasisha kuchukua hatua na kuwapa uhuru wa kuweza kutumia uwezo
mkubwa uliopo ndani yao. Usiwe meneja ambaye kila kitu kwenye uchukuaji hatua unakisimamia wewe na mtu hawezi kufanya kitu mpaka wewe umwelekeze kwanza. Hilo litakuchosha sana.
25.
Jifunze kuongea. Mtu anayeweza kuongea kwa kujiamini kuhusu kile
anachouza anaaminika zaidi na wateja. Na asiyeweza kuongea vizuri, hata
kama anauza kitu kizuri, wateja hawatamwamini sana. Jifunze jinsi ya kuongea vizuri, kwa ushawishi na ubobezi na utawafanya watu waamini kwenye kile unachowaelezea.
26. Jifunze kusikiliza. Kuongea tu hakutakusaidia sana kama hutakuwa msikilizaji, jifunze kusikiliza pale wengine wanapoongea. Na
siyo unasikiliza tu kwa masikio, bali pia unaangalia lugha za vitendo
ambazo mwongeaji anakuwa anatumia, hivi ni viashiria ambavyo vitakueleza
mengi zaidi.
27. Fanya mazoezi mara kwa mara. Mazoezi
ya viungo yana manufaa makubwa sana kwako kiafya na kiufanisi kwenye
majukumu yako, hivyo tenga muda wa kufanya mazoezi kila siku. Ukiweza
kupata dakika 30 za mazoezi kila siku, utapunguza hatari ya magonjwa
kama kisukari na presha, na pia utaongeza ufanisi wako kwenye kazi zako.
Pia tafiti zinaonesha watu wanaofanya mazoezi wana kipato kikubwa
kuliko watu wasiofanya mazoezi. Hebu anza kufanya mazoezi kila siku na
utashangaa jinsi kipato chako kitakavyoanza kuongezeka.
28.
Ishi maisha bora kiafya. Mazoezi ni hatua moja ya kuwa na afya bora.
Hatua nyingine ni ulaji na kujikinga na hatari za magonjwa. Kula kiafya, epuka vyakula vya haraka, epuka vilevi, sigara, madawa ya kulevya na jiepushe na vihatarishi vya magonjwa. Afya yako ni mtaji muhimu sana kwako, isipokuwa imara hutaweza kufanya chochote kikubwa.
29. Pata usingizi wa kutosha. Wajasiriamali wengi hujisifia kwa jinsi wanavyoweza kulala kidogo na kufanya kazi masaa mengi. Usiingie kwenye mtego huo, hakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala, kulingana na uhitaji wa mwili wako. Miili
yetu inatofautiana, kwa wastani masaa nane yanashauriwa kiafya, lakini
wapo wanaohitaji machache zaidi ya hayo na wapo wanaohitaji mengi zaidi.
Hivyo jua uhitaji wa mwili wako, kama masaa nane ndiyo yanakutosha basi
pata masaa nane. Kama masaa 6 au 7 yanakutosha pata muda huo wa kulala.
Kitu muhimu zaidi kupima kwako siyo masaa mangapi hujalala, bali umezalisha nini kwenye muda wako. Kadiri unavyopumzika zaidi, ndivyo unavyoweza kuzalisha zaidi.
30.
Fanya tahajudi au kuandika jarida lako kila siku. Tahajudi ni zoezi
ambalo huwa linafanywa na karibu dini na falsafa zote. Kila dini au
falsafa watu wana utaratibu wao wa kutuliza fikra zao na kutafakari yale
muhimu. Pia unaweza kuandaa zoezi lako la tahajudi kwa kutafakari yale
muhimu zaidi kwako. Pia
unaweza kufanya zoezi la kuandika jarida lako kila siku, kila siku
unakaa chini na kuandika mawazo yako kwenye kijitabu chako, kwa njia hii
unapata utulivu wa kipekee kwako.
31. Fanya kile unachopenda kufanya. Pamoja na kuwa kwenye biashara, unapaswa kutenga muda wa kufanya kile unachopenda kufanya, ambacho hakihusiani na biashara yako. Hupaswi kuwa mtu wa kufanya na kufikiria kazi muda wote. Tenga muda wa mapumziko ambao utautumia kufanya vile vitu unavyopenda kufanya, ambavyo havihusiani na kazi au biashara yako.
32. Wasaidie wengine. Ni rahisi kukazana na malengo ambayo umejiwekea na kuona huna muda wa kuwasaidia wengine. Lakini njia rahisi ya kupata chochote unachotaka ni kuwasaidia wengine kupata kile wanachotaka. Mara
kwa mara jitolee kufanya kazi za kijamii, wasaidie wanaoweza na hata
biashara yako iwe ina lengo la kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora
zaidi na siyo tu kupata faida.
33. Jiamini. Kadiri unavyokuwa kwenye ujasiriamali, ndivyo hali ya wasiwasi inavyojijenga ndani yako. Unapata
hali fulani ya hofu kwamba huenda mafanikio unayopata ni bahati tu na
ipo siku mambo yatabadilika na kila mtu atagundua kwamba hukuwa na
mafanikio halisi bali bahati tu. Jua hali hii humpata kila anayepiga hatua za mafanikio, na njia pekee ya kuishinda ni kujiamini wewe mwenyewe.
Hata kama kuna bahati umekutana nayo, amini juhudi na maandalizi
uliyoweka yamekusaidia. Na pia jua hata kama utapoteza kila ulichonacho,
utaweza kuanza tena na kufanikiwa.
No comments:
Post a Comment