Sunday, June 12, 2016

MBINU ZA KUBADILISHA TABIA MBOVU



Kwenye kitabu nilichosoma hivi karibuni, The Power of Habit (Kwa Kiswahili: Nguvu ya Kubadilisha Tabia) mwandishi Charles Duhigg anatoa somo juu ya namna ya kubadilisha tabia zisizofaa.
Ni kitabu kilichochapishwa mwaka 2012 na kampuni ya Random House Trade Paperbacks ya New York nchini Marekani na kimewahi kuongoza kwa mauzo kwenye orodha ya vitabu vyenye mauzo makubwa vinavyoorodheshwa na Gazeti la New York Times.
Swali la msingi analouliza mwandishi, na ambalo analitafutia jibu ni: kwanini tunafanya vitu ambavyo tunafanya? Majibu anayotoa yanarahisisha kubadilisha tabia mbovu.
Wote tunatambua kuwa ziko tabia kuu mbili: nzuri na mbaya. Duhigg anamwambia msomaji kuwa hakuna tabia mbovu ambayo haiwezi kubadilishwa. Na jambo kuu la kuweza kubadilisha hizi tabia ni, kwanza, kutambua hulka ya tabia na jinsi gani zinashamiri na; pili, kuweka nia ya kuzibadilisha.
Mwandishi ameandika kitabu kutokana na utafiti wake mwenyewe, lakini ametumia zaidi matokeo ya utafiti wa kina ambao umefanyika kubaini sababu za kuwapo au kutokuwapo kwa tabia zisizofaa.
Tabia zisizofaa tunazihusisha zaidi na mwanadamu, lakini yapo makundi mawili yanayohusishwa na tabia: tabia za taasisi au mashirika, na tabia za jamii. Na kote huku anasisitiza mwandishi, kwa kutumia mifano mingi, hata taasisi/mashirika, na jamii zinaweza kuwa na tabia mbaya, na zinaweza kuweka mikakati ya kubadilisha hizi tabia.
Lakini kwa kuwa mhusika mkuu katika maeneo yote haya matatu ni mwanadamu, basi ni dhahiri kuwa mwenye ufunguo wa kuibua tabia chanya ndani ya taasisi/mashirika na jamii ni mwanadamu huyo huyo.
Kimsingi, tabia ni mchakato wenye hatua tatu. Ubongo umeundwa kukwepa kufanya kazi ngumu ya kufikiri kila wakati, kwa hiyo ili kuongeza ufanisi wake, na ili ubongo utumike pale inapolazimu tu, ipo sehemu ya ubongo inayoitwa basal ganglia ambayo huweka kumbukumbu za tabia tunazojenga.
Hatua ya kwanza ya mchakato unaokamilisha tabia inaanzishwa na kichocheo. Katika hatua ya pili, kichocheo kinasababisha tufuate desturi iliyohifadhiwa ndani ya basal ganglia na inayohusishwa na kichocheo hicho mahsusi. Unaweza kufananisha basal ganglia na maktaba ya kanda zinazohifadhi desturi zetu, na kila tunapoona, kugusa, kusikia, au kunusa kichocheo fulani basi kile kichocheo kinaoanishwa na kanda mahsusi ya kichocheo hicho. Kumbukumbu ya hiyo kanda inatufanya tufuate desturi fulani.
Hatua ya mwisho ya mchakato wa tabia ni manufaa ambayo tunayapata kutokana na kutekeleza wa hiyo desturi ya hatua ya pili.
Wengi tunakubaliana kuwa tabia ambayo haina mtetezi ni unywaji pombe uliokithiri. Pamoja na kuwa upo ukweli kuwa ni tatizo ambalo linasababishwa zaidi na masuala ya afya ya akili, bado tunaambiwa na mwandishi kuwa upo mchakato wa kitabia wenye hatua tatu ndani ya unywaji pombe na ambao unaweza kubadilishwa na kumwepusha mtu na unywaji pombe. Wengi wanaokunywa pombe hawanywi kwa sababu ya kutaka kulewa, bali hutafuta manufaa (hatua ya tatu) kama kujaribu kusahau matatizo, kupumzisha akili, kupata watu wa kuongea nao, au kukwepa jambo fulani linalowasumbua.
Katika kuweka nia ya kubadilisha tabia, hatua ya kwanza (kichocheo) na ya tatu (manufaa) havibadiliki. Tunachojaribu kufanya ni kubadilisha hatua ya pili (desturi). Kwa mfano, kama kichocheo ni msongo wa mawazo na huo ndio unatuchochea kwenda hatua ya pili ya kukaa kwenye baa na kuanza kunywa pombe, suluhisho ni kubadilisha desturi ya kuhamia kwenye baa na kuweka desturi nyingine ambayo italeta manufaa yale yale ya hatua ya tatu.
Badala ya msongo wa mawazo kusababisha kwenda baa kutafuta watu wa kuongea nao, desturi ya kwenda baa inabadilishwa na desturi ya kutafuta ndugu, jamaa, na marafiki ambao kwa kuzungumza nao mwathirika anaweza kupata faida ile ile ya kupata watu wa kuzungumza nao.
Ukitaka kumchekesha mlevi mwambie anaweza kuacha kunywa pombe kwa kuacha kwenda baa kupiga gumzo na wanywaji wenzake, na badala yake azunguke kwa majirani na kuongea nao na kuwa anaweza kupata faida ile ile ambayo anaipata kwenye baa. Kwa ufupi, kama ilivyo kwa tabia nyingi zisizofaa, tabia zinazosababisha watu kulewa chakari siyo rahisi kuzibadilisha. Lakini inapojengeka nia, yote yanawezekana.
Ukiangalia yale yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, utagundua kuwa ipo jitihada ya kugeuza jamii ya Watanzania kuwa na tabia tofauti katika masuala kadhaa. Serikali ya Rais John Magufuli imeanza kazi kwa kujaribu kubadilisha tabia tulizozowea zamani, na kujaribu kutufundisha tabia mpya.
Lakini ni wazi kuwa hatua ya pili na ya tatu katika mchakato wa kitabia wa enzi hizi za awamu ya tano zinabadilika. Zamani kwenye hatua ya kwanza kiliibuka kichocheo kilichomfanya mtumishi wa umma aingie hatua ya pili ya kupokea mshahara wake na wa watu wengine kadhaa. Hatua ya tatu ikawa yale manufaa ya mapato kuongezeka kwa kupata mshahara zaidi ya mmoja.
Sasa, falsafa ya Hapa Kazi Tu inaweka msimamo kuwa desturi ya kupokea mshahara zaidi ya mmoja kinyume cha sheria si desturi inayopaswa kuvumiliwa.
Desturi mpya inayojengeka sasa ni ya watumishi kupokea mshahara mmoja, na manufaa mapya yanakuwa kuendelea kuajiriwa na kuepuka kwenda gerezani na kufanya kazi bila malipo.
Mwandishi Charles Duhigg anatahadharisha kwenye utangulizi wa kitabu chake kuwa kubadilisha tabia si jambo rahisi, lakini ni jambo ambalo linawezekana. Na yeye anaonesha njia ya namna ya kufanya hivyo.

CHANZO   CHA   MAARIFA :  GAZETI  LA  JAMHURI , 08  JUNI , 2016.

No comments:

Post a Comment