Mheshimiwa
Rais, nianze kwa kukupa pole kwa majukumu mazito uliyonayo ya kulijenga taifa
letu. Wananchi wanyonge wamekuwa na imani kubwa na wewe kutokana na juhudi zako
ambazo umeishazionyesha katika kuwaletea maendeleo tangu uingie madarakani.
Tunakutia moyo na kukuombea uendelee na juhudi hizo na tunaahidi kuwa nyuma
yako katika kulijenga taifa letu.
Mheshimiwa
Rais, nina mambo muhimu ya kukueleza kuhusu mfumo wa elimu yetu. Nimeamua kukuandikia
wewe kwa sababu wewe ndiye mkuu wa nchi yetu na mambo yote yako chini yako.
Serikali yako ikifanya vizuri, wewe ndiye utakayepongezwa, na ikifanya vibaya
wewe ndiye utakayebebeshwa mzigo wa lawama.
Jambo
la pili lililonifanya nikuandikie ni umuhimu wa elimu katika maendeleo ya
taifa. Elimu ndiyo injini ya taifa lolote duniani. Taifa lililoelimisha
wananchi wake kwa kuwapa elimu bora, huwa na maendeleo makubwa. Mataifa mengi
duniani yameendelea kutokana na kuwekeza katika elimu bora kwa wananchi wake.
Elimu hiyo bora imewasaidia kupata wataalamu mbalimbali waliochangia kuleta
maendeleo katika nchi zao na hata nje ya mipaka ya nchi zao.
Mheshimiwa
Rais, elimu bora inaundwa na mafiga matatu, yaani walimu bora, mazingira bora
na vitabu bora. Nimetumia neno “mafiga”, kuonyesha kutegemeana kwa mambo hayo
matatu. Ili mpishi aweze kupika chakula chake hadi kiive vizuri, hana budi
kutumia mafiga matatu yenye ukubwa na ubora sawa. Ngoja nikupe mchapo mmoja
uliowahi kutokea kijijini kwetu wakati nikiwa bado mdogo. Kuna mkulima mmoja
aliondoka nyumbani kwake asubuhi na mapema kwenda shambani kulima, ulipofika
muda wa mchana alihisi njaa, aliamua kurudi nyumbani kuandaa chakula.
Alipofika
nyumbani kwake alitafuta mafiga matatu kwa ajili ya kupikia chakula. Mafiga
mawili kati ya hayo yalikuwa na ukubwa sawa, na figa moja lilikuwa dogo kuliko
yale mawili. Majirani zake walimshauri atafute mafiga yanayolingana, lakini
yeye hakusikiliza ushauri wao. Aliwasha moto na kuweka sufuria la chakula
kwenye mafiga, sufuria liliinama upande lakini yeye hakujali. “Unajua nini
kilichotokea?” Chakula kilipoanza kuchemka kilimwagikia kwenye moto na kuuzima.
Majirani zake walimcheka, alitokea jirani mmoja msamaria mwema aliyemuonea
huruma na kumpa chakula alichokuwa nacho kutokana na njaa kali aliyokuwa nayo.
Baada ya kukupa mchapo huo, naomba nianze kuelezea figa moja baada ya jingine.
Walimu
bora. Hawa ni watu muhimu sana katika kutoa maarifa kwa wanafunzi. Walimu
wakiandaliwa vizuri huweza kutoa maarifa sahihi kwa wanafunzi. Nchini Tanzania
kazi ya ualimu inaonekana kupewa hadhi ya chini ukilinganisha na kazi nyingine,
hii inatokana na sababu zifuatazo: kwanza, ni kipato kidogo wanacholipwa walimu
ukilinganisha na kazi wanazofanya; pili, ni ufaulu wa kiwango cha chini kwa wanafunzi
wanaoenda kusomea taaluma ya ualimu. Asilimia kubwa ya wanafunzi wanaoenda
kusomea ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada ni wale ambao hawakufanya
vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari. Kutokana na ufaulu
huo wa kiwango cha chini, wengine hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya
elimu ya juu na hivyo kulazimika kujiunga na vyuo vya ualimu kama kimbilio
pekee. Utaratibu huu wa vyuo vya ualimu kuchukua wanafunzi ambao hawakufanya
vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari, umeifanya jamii
iione kazi ya ualimu kama ni ya watu waliofeli na kukosa njia nyingine ya
kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Siku
moja nilimsikia baba mmoja akimuuliza jirani yangu, “vipi matokeo ya kijana
wako?” Jirani alijibu, “hajafanya vizuri sana”, yule baba aliuliza, “hawezi
kupata hata nafasi ya ualimu?” Hii inaonyesha wazi kwamba, jamii inaiona
taaluma ya ualimu kama ni ya watu waliofeli katika mitihani yao ya sekondari.
Kutokana na mtazamo huo, wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri kwenye mitihani yao
ya mwisho katika elimu ya sekondari hukataa kwenda kusomea ualimu. Tujiulize,
kama vyuo vya ualimu vinachukua wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika
mitihani yao, tunaandaa taifa la wataalamu wa aina gani?
Tukitaka
kupata walimu bora watakaojitoa kufanya kazi kwa ufanisi, hatuna budi
kuzingatia mambo yafuatayo:
1.
Kuboresha maslahi ya walimu, kuwapa stahiki zao zote na kuwapandisha madaraja
kwa wakati. Kisheria mwalimu anapomaliza miaka mitatu kazini tangu aajiriwe
anastahili kupandishwa daraja na kuongezewa mshahara, lakini hilo halifanyiki
kwa walimu walio wengi, jambo ambalo linawavunja walimu moyo wa kujitolea
kufanya kazi kwa bidii;
2.
Kuwapa wathibiti ubora wa shule mamlaka ya kupendekeza wakuu wa shule pamoja na
wasaidizi wao kulingana na sifa na utendaji kazi wao tofauti na ilivyo sasa,
ambapo wakuu wa shule huteuliwa na maafisa elimu wa wilaya ambao hawako karibu
na walimu na hawawajui vizuri ukilinganisha na wathibiti ubora wa shule ambao
wako karibu zaidi na walimu na wanafahamu vizuri uwezo wa kila mwalimu;
3.
Kuboresha maslahi ya wakuu wa shule na wasaidizi wao ili waifanye kazi ya
kuwasimamia walimu kikamilifu; 4. Kuboresha idara ya uthibiti ubora wa shule
kwa kuipatia mahitaji yote muhimu yanayotakiwa katika kazi yao pamoja na
vitendea kazi kama vile magari ya kutosha ili waweze kuzungukia shule zote na
kukagua utendaji kazi wa walimu pale inapotakiwa.
Nina
imani kuwa walimu wakisimamiwa vizuri na kupandishwa madaraja kwa wale
watakaoonekana kuifanya kazi yao vizuri, watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa; 5.
Kuwajengea walimu nyumba za kuishi karibu na mazingira ya shule ili wawe karibu
na vituo vyao vya kazi; 6. Kuboresha mazingira ya shule za vijijini kwa
kuhakikisha kuwa kuna huduma za afya, maji, miundombinu mizuri na umeme wa jua
kama umeme wa gridi ya taifa haujafika huko;
7.
Kuwa na mgawanyo sawa wa walimu kati ya shule zilizoko mijini na zile zilizoko
vijijini tofauti na ilivyo sasa, ambapo shule nyingi za mijini zina walimu
wengi ukilinganisha na shule zilizoko vijijini, mfano mzuri ni shule ya msingi
Mahina iliyopo Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza ina jumla ya walimu 45 na
shule ya msingi Tandari iliyopo Kata ya Bunduki, Mkoa wa Morogoro ina walimu
wawili (2) tu wanaofundisha kuanzia darasa la kwanza hadi la saba;
8.
Vyuo vinavyoandaa walimu wa shule za msingi, vianzishe utaratibu wa kuandaa
walimu watakaofundisha masomo yasiyozidi matatu ambayo waliyafaulu vizuri
kwenye mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari, kuliko utaratibu uliopo
sasa unaowaandaa walimu kufundisha masomo yote hata yale waliyopata daraja “F”
kwenye mitihani yao ya elimu ya sekondari;
9.
Kuongeza idadi ya vyuo vinavyofundisha elimu ya awali ili tupate walimu wengi
watakaokidhi mahitaji, tofauti na ilivyo sasa ambapo katika shule nyingi,
walimu wanaofundisha elimu ya awali, wengi wao hawajasomea taaluma hiyo. Elimu
ya awali ndio inayomjengea mtoto msingi bora wa elimu. Tukumbuke kwamba, mtoto
anapokuwa hajaanza shule, ubongo wake huwa hauna mambo mengi na hupokea kwa
haraka na kuyashika yale anayoyaona na kuyasikia.
Kama
tukiziboresha shule zote za awali kwa kuwa na walimu waliosomea taaluma ya
kufundisha na kulea watoto na kuzipatia vifaa vyote vya kufundishia na
kujifunzia, tutawajengea watoto wetu msingi bora wa elimu na kuwafanya waipende
shule na pindi watakapoanza darasa la kwanza, watakuwa wanafunzi wenye mwanga
mzuri;
10.
Kuwaimarisha walimu kiutendaji kwa kuchukua hatua zifuatazo: kuwapatia mafunzo
kazini kwa nia ya kuwaimarisha katika masomo yao, kuwapanga katika makundi ya
masomo yao (specialization) mfano masomo ya Sayansi na Hesabu; Kiswahili na
Kiingereza; Historia, Jiografia na Uraia; 11. Kuanzisha taasisi za mikopo kwa
walimu (sacoss) ili wapate mikopo ya kuboresha maisha yao.
Tukizingatia
yote hayo, tutawavutia hata wale waliokuwa hawapendi kusomea ualimu, na hivyo
kupata walimu wengi bora na si bora walimu. Je, ni mazingira yapi yatamfanya
mwalimu kutoa elimu bora? Ni vitabu vipi vitamfanya mwanafunzi kupata elimu
bora? Usiikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo kwa mwendelezo wa ujumbe huu
mahususi kwa Rais John Pombe Magufuli.
CHANZO CHA
HABARI : GAZETI LA
JAMHURI , 31, MEI , 2016.
Barua
hii imeandikwa na Ndugu:-
KALISTI
MJUNI
Mdau
wa elimu (msomaji wa JAMHURI) 0762488763
Email:
kalimjuni_25@yahoo.com
No comments:
Post a Comment