Sunday, June 12, 2016

KIDOLE CHAMPONZA SUGU , APELEKWA KAMATI YA MAADILI

 
 JOSEPH   MBILINYI

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), atashtakiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa tuhuma za kuwaonesha wabunge wenzake kidole cha kati, kinachodaiwa kuwa ni ishara ya matusi.

Uamuzi huo ulitolewa bungeni jana mchana na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, wakati akijibu mwongozo ulioombwa Juni 6, 2016 na Mbunge wa Viti Maalumu, Backline Msongozi (CCM).

Katika mwongozo huo, Msongozi alitaka kujua uhalali wa kitendo kilichofanywa na mbunge huyo cha kuonesha kidole cha kati ambacho alisema ishara yake ni matusi.
Dk. Tulia alisema ametoa majibu ya mwongozo huo baada ya kujiridhisha kupitia kamera iliyomwonyesha Sugu akionesha kidole hicho wakati akitoka bungeni.
“Msongozi alisimama kwa mujibu wa kanuni ya 68 ya Bunge kuomba mwongozo wa Spika kuhusu kitendo cha Mbilinyi kulidhalilisha Bunge na kudharau kiti cha Spika kwa kuonesha dole kitendo ambacho ni matusi.

Katika kujenga hoja ya mwongozo huo, alisema mwakilishi wa kambi ya upinzani baada ya kuwasilisha hoja na kuanza kuondoka alionyesha dole ambayo ni ishara ya matusi kwa Bunge na pia alidhalilisha kiti.
“Jambo linaloombewa mwongozo linatokana na maadili ya Bunge kutokana na mbunge kuonesha kitendo ambacho kinatafsiri ya matusi endapo kitendo hicho kitathibitika itakuwa ni kinyume na masharti ya kanuni ya 74, inayohimiza maadili.

“Hivyo naelekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kufanya uchunguzi kuhusu kitendo kinachodaiwa kufanywa na Mbilinyi kwa mujibu wa kanuni za Bunge na kuchukua hatua stahiki,” alisema Naibu Spika Dk. Tulia.
Wiki iliyopita mbunge huyo aliwashangaza wabunge wenzake, baada ya kuwanyooshea kidole cha kati akiwa bungeni.

Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, alifanya hivyo baada ya kuwasilisha taarifa ya maoni ya kambi ya upinzani Azimio la Bunge la kuridhia mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu katika michezo, lililowasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

CHANZO   CHA  HABARI :  GAZETI   LA  MTANZANIA , NA  HAMISI  MKOTYA ,DODOMA ,11/06/2016

No comments:

Post a Comment