Sunday, March 24, 2019

ENEO LA FAMILIA :Ulipo Sasa, Unakotaka Kufika, Viwango vya Kujiwekea, Kitabu cha Kusoma.

Familia yako ni mahusiano ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yako. Haya ni mahusiano ambayo yana mchango mkubwa sana kwenye mlinganyo wako wa mafanikio. Kadiri mafanikio haya yanavyokuwa bora, ndivyo unavyokuwa bora.

ULIPO SASA; je unafurahia kurudi nyumbani baada ya siku yako ya kazi kuisha? Je unajua lipi jukumu lako kuu kwenye familia? Na je familia kwako ni watu gani? Unaamini familia ni mzigo kwako au kichocheo kwako kufanikiwa?

UNAKOTAKA KUFIKA; pata picha ya familia bora kwako, inawahusisha watu gani, mahusiano yapoje na kila mtu ana mchango gani kwenye familia hiyo? Weka juhudi katika kujenga familia hii bora kwako na siyo kuishi kwenye familia usiyoifurahia.

VIWANGO VYA KUJIWEKEA; weka lengo la kutenga muda wa kufanya mambo ya kifamilia. Tenga muda wa kuwa pamoja na familia, mfano mzuri ni kuwa na chakula cha pamoja, kutoka pamoja au kwenda kutembelea ndugu na jamaa kama familia. Haya yanaimarisha mahusiano ya kifamilia.

KITABU CHA KUSOMA; kitabu MASTERY OF LOVE cha Don Miguel Ruiz kitakupa msingi mkuu wa mafanikio kwenye familia ambao ni upendo.

ENEO LA MAPENZI : Ulipo sasa, Unakotaka Kufika, Viwango vya Kujiwekea . Kitabu cha Kusoma.

Hili ni eneo linalohusu mahusiano yako ya kimapenzi na mwenza wako. Ni eneo muhimu sana kwa sababu hili linagusa kila eneo la maisha yetu. Kama mahusiano yako ya kimapenzi yako vizuri basi maisha yako yanakuwa vizuri. Lakini kama eneo hili lina matatizo, hutaweza kutuliza akili yako kwenye jambo lolote.

ULIPO SASA; Tafakari pale ulipo sasa kwenye mahusiano yako ya kimapenzi, je umeoa au kuolewa au upo peke yako? Na je kwenye hali ya mahusiano uliyopo, unayafurahia? Unayaelezeaje mapenzi? Ni kitu gani unatoa na kipi unapokea kutoka kwenye mahusiano yako ya mapenzi? Je unaamini mapenzi yanaleta maumivu? Je upo tayari kumpenda kweli mwenzako na kumwonesha kwamba unampenda? Je unajiona ni mtu unayestahili kupendwa kweli? Jiulize na kujipa majibu ya maswali hayo na yatakupa picha ya pale ulipo sasa.

UNAKOTAKA KUFIKA; Katika kuboresha zaidi mahusiano yako ya kimapenzi, unapaswa kuwa na picha ya wapi unataka mahusiano hayo yafike. Katika kutengeneza picha ya unakotaka kufika, jiulize na kujipa majibu ya maswali haya; je mahusiano bora ya kimapenzi kwako unataka yaweje? Pata picha ya mahusiano yenye mafanikio, mnawasilianaje, kuchukulianaje, vitu gani mnafanya pamoja na jinsi mnavyoyafurahia maisha pamoja. Kuwa na picha hii kila wakati na ifanyie kazi, itakusukuma kuwa bora zaidi.

VIWANGO VYA KUJIWEKA; Katika eneo la mapenzi unapaswa kujiwekea viwango ambavyo utavizingatia ili kuimarisha eneo hili. Viwango vya kujiwekea ni muda wa kuwa pamoja wewe na mwenza wako, inaweza kuwa kwenye mtoko mnaofanya pamoja, kufanya mazoezi pamoja na hata kuwa na ratiba ya kuwa na faragha nyinyi wawili pekee kwa ajili ya yale muhimu kwenu. Zingatia sana hili la kupata muda wa kuwa na mwenzako na weka kiwango cha muda huo.

KITABU CHA KUSOMA; Kujiweka vizuri kwenye eneo la mahusiano ya mapenzi soma kitabu kinachoitwa MEN ARE FROM MARS, WOMEN ARE FROM VENUS Kilichoandikwa Na John Gray. Kitabu hiki kitakufundisha jinsi ya kuishi na mwenzako.

Thursday, March 21, 2019

LIPE TATIZO LAKO MUDA KAMA NJIA ZINGINE ZIMESHINDIKANA.

Wenye busara walisema muda ni tiba ya kila kitu. Kwamba hakuna kitu ambacho muda haukiathiri, hivyo kama kuna kitu kinakusumbua, ambacho unaona kimekushinda, uachie muda ufanye kazi yake.
 
Hakuna kitu ambacho muda unakiacha jinsi ulivyo bila ya kukiathiri, kadiri muda unavyokwenda, tatizo linakosa nguvu au njia bora za kulitatua inapatikana.
 
Hata kama kwa sasa huoni kabisa namna ya kuvuka ugumu unaopitia, usikate tamaa, jua muda uko upande wako. Unachohitaji ni uvumilivu na kusahau tatizo hilo kwa muda, kwa kutoruhusu likutawale wakati huna cha kufanya.
 
Kila ugumu unaopitia, jua kwamba utaupatia jawabu au muda utatoa jawabu. Hivyo kama umeshafanya kila unachoweza kufanya na zaidi, lakini hupati majibu, hapo siyo mwisho, muda una nafasi kubwa ya kuhangaika na tatizo hilo. Kubali na songa mbele na mengine yaliyo ndani ya uwezo wako, na muda utahangaika na hilo lililokushinda.

Saturday, March 9, 2019

TUMBO LA JUU NI ENEO LA NGUVU KWENYE MIILI YETU---KINAHUSIKA NA MATAKWA YETU,NGUVU ZETU ,UDHIBITI , HAMASA , MSUKUMO NA UTAWALA.

TUMBO  LA  JUU, ni   eneo   la  nguvu   kwenye   miili  yetu ,hili ni eneo la mwili juu ya kitovu. Kituo hiki kinadhibiti tumbo la chakula, utumbo mwembamba, bandama, ini, mfuko wa nyongo, figo na tezi zilizopo juu ya figo.
Kituo hiki kinahusika na matakwa yetu, nguvu zetu, udhibiti, hamasa, msukumo na utawala. Hiki ni kituo cha mashindano na nguvu binafsi, kujithamini na hata kuwatawala wengine.
Kituo hiki kinapokuwa vizuri, unaweza kutumia nguvu za kituo hiki kufikia malengo yako, kuwa na hamasa ya kupiga hatua zaidi na kuzivuka changamoto mbalimbali unazokutana nazo. Kituo hiki pia kinakupa nguvu ya kujilinda wewe mwenyewe na kuwalinda wale wa karibu kwako.
Watu wamekuwa wanatumia vibaya nguvu za kituo hiki kwa kujiona wao ni wa muhimu kuliko wengine, kutaka kuwatawala wengine na hata kuwaonea wengine pale mtu anapokuwa na mamlaka au nguvu fulani.
Kutumia vizuri nguvu za kituo hiki tunapaswa kujijua sisi wenyewe na kujua nini hasa tunachotaka kisha kuweka nguvu zetu kwenye maeneo hayo. Hatupaswi kujionesha kwa wengine au kuwalazimisha wengine wawe kama tunavyotaka sisi.

Friday, March 8, 2019

TUMBO LA CHINI NI KITUO CHA NGUVU KWENYE MWILI KINAHUSU ULAJI WETU NA MAHUSIANO YETU NA WENGINE.

Tumbo la chini  ni   kituo  cha nguvu kwenye mwili hili ni eneo la mwili kwenye usawa wa kitovu. Kituo hiki kinadhibiti utumbo mpana, kongosho, kiuno, mifuko ya mayai na tumbo la uzazi kwa wanawake.
Kituo hiki kinahusika na ulaji, umeng’enyaji na utoaji wa mabaki ya chakula mwilini. Homoni mbalimbali huzalisha kwenye kituo hiki ambazo zinahusika na umeng’enyaji wa vyakula.
Kazi kubwa ya kituo hiki ni mahusiano ya kijamii, familia, utamaduni na hata mahusiano baina ya mtu mmoja na mwingine. Hiki ni kituo cha kushikilia au kuachilia au kuondoa.  Kituo hiki kinapokuwa vizuri, mtu unakuwa na utulivu na kujisikia salama na amani.
Watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu ya kituo hiki vibaya kwa kuwa na hasira na vinyongo kwa wengine na kukosa maelewano mazuri na wengine. Kila unaposhikilia kitu ndani yako dhidi ya mtu mwingine, unashikilia nguvu ambayo ungeweza kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Ulaji uliopitiliza pia unaathiri kituo hiki kwa nguvu kubwa kutumika kumeng’enya chakula na kuondoa uchafu mwilini kitu ambacho kinazuia nguvu hiyo kutumika kwenye kutenda miujiza.
Ili kuweza kutumia vizuri nguvu ya kituo hiki, tunapaswa kudhibiti ulaji wetu na kuimarisha mahusiano yetu na wengine.

VIUNGO VYA UZAZI NI KITUO AMBACHO HUPOTEZA NGUVU NYINGI ZA WATU.

Kituo cha kwanza cha nguvu kipo kwenye viungo vyetu vya uzazi na kinadhibiti sehemu za mwili zilizopo chini ya kitovu. Hapa inahusika uke, uume, kibofu cha mkojo, sehemu ya mwisho ya utumbo na hata ngozi na misuli inayozunguka maeneo haya.
Kazi kubwa ya kituo hiki ni uzazi, jinsia, kujamiiana na kutoa uchafu mwilini. Homoni za uzazi huzalishwa kwenye kituo hiki. Kituo hiki kina nguvu kubwa sana ya ubunifu na uumbaji, fikiria nguvu ambayo inatumika katika kujamiiana na hata kupata mtoto.
Watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu ya kituo hiki vibaya kwa kuelekeza nguvu zao nyingi kwenye kujamiiana na kuwa na mahusiano mengi ya kingono. Hili linawapunguzia uwezo wa kufanya makubwa kwenye maisha yao.
Ili uweze kutumia nguvu hii ya kituo cha kwanza katika kufanya miujiza, unapaswa kujidhibiti sana kwenye eneo la ngono, kwa kuwa hili ndiyo linapoteza nguvu za wengi.

Monday, February 25, 2019

NGUVU YA KUFANYA KWA MALENGO.

Kinachowatofautisha wale wanaofikia ubobezi na wale wanaoishia kuwa kawaida siyo wanachofanya, bali namna wanavyofanya kile wanachofanya. Watu wawili wanaweza kuwa wanafanya kitu kimoja, lakini mmoja akabobea na mwingine asibobee.
Mwandishi anatuambia zipo aina tatu za ufanyaji ambazo zinawatofautisha wanaobobea na wanaokuwa kawaida.
Aina ya kwanza ni kufanya kwa kawaida, hapa mtu anafanya kile ambacho amezoea kufanya kila wakati, hakuna kipya anachofanya na hivyo hawezi kubobea. Hivi ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao, wanaonekana kufanya sana lakini hakuna hatua wanapiga. Hii ni kwa sababu wanafanya kwa mazoea.
Aina ya pili ni kufanya kwa malengo, hapa mtu anafanya kitu kwa malengo, na hivyo anakuwa na hatua anazopanga kupiga zinazomsukuma kufanya zaidi. Katika kufanya kwa malengo mtu anapiga hatua zaidi kwa sababu malengo anayojiwekea yanamsukuma zaidi. Kwenye kufanya kwa malengo mtu anakuwa na sifa nne; moja anakuwa na lengo la wapi anataka kufika, mbili anaweka umakini wake wote kwenye kile anachofanya. Tatu anakuwa na njia ya kujipima na kupata mrejesho wa hatua anazochukua na nne anajisukuma kutoka nje ya mazoea, kufanya vitu vipya ambavyo vinamwezesha kupiga hatua zaidi.
Aina ya tatu ni kufanya kwa makusudi, kama mwandishi anavyoita DELIRATE PRACTICE, hapa mtu anakuwa na kusudi kubwa linalomsukuma kufanya kitu. Hii ndiyo aina ya ufanyaji ambayo inazalisha watu wenye ubobezi wa hali ya juu. Kufanya kwa makusudi kuna sifa kama za kufanya kwa malengo, lakini ina sifa nyingine mbili za nyongeza. Ya kwanza ni eneo ambalo mtu anakuwa amechagua kubobea linapaswa kuwa na wabobezi ambao wanaweza kuangaliwa na mtu akajifunza kwao. Mtu anapoweza kuwaangalia wabobezi na kujifunza kile wanachofanya na namna wanavyofanya, inakuwa rahisi kwake naye kufanya. Sifa ya pili ni kuwa na mwalimu au kocha ambaye anamfundisha na kumsimamia mtu kwenye hatua anazochukua. Kwa kuwa na mtu wa nje anayetoa maelekezo au kupima hatua mtu anazochukua na kutoa mrejesho, kunamfanya mtu apige hatua kubwa zaidi.
Hizo ndizo aina tatu za ufanyaji na aina ya tatu ndiyo mwandishi ameijadili kwa kina sana kwenye kitabu cha PEAK.