Thursday, December 20, 2018

WEKA AKIBA SEHEMU YA KUMI YA KIPATO CHAKO.

Kwenye kila kipato unachoingiza, asilimia kumi ya kipato hicho hupaswi kuitumia kwa shughuli nyingine yoyote, bali unapaswa kujilipa wewe mwenyewe. Hichi ni kipato ambacho unakiweka pembeni maalumu kwa ajili ya uwekezaji ambao utakulipa zaidi baadaye.
Unapopata fedha, kabla hujaanza kulipa bili mbalimbali unazodaiwa au kununua vitu unavyohitaji, jilipe wewe mwenyewe kwanza. Hii ni tabia moja rahisi ambayo imewawezesha wengi kufikia utajiri mkubwa, bila ya kujali kiasi cha kipato walichonacho. Unapaswa kujilipa kwanza kabla hujafanya matumizi, kwa sababu ukisema utumie halafu itakayobaki ndiyo ujilipe, hutabakiwa na kitu.
Zoezi la kufanya; kwenye kila kipato unachoingiza, kabla hujaanza kupangilia unakitumiaje, ondoa kwanza asilimia kumi ya kipato hicho na weka pembeni, weka mahali ambapo hutakitumia hata iweje. Kipato hicho ni kwa ajili ya uwekezaji, ndiyo kitakachokufanyia wewe kazi.

DHIBITI MAWAZO NA HISIA ZAKO KILA SIKU.


Ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuzitawala hisia na mawazo yako kila wakati. Hupaswi kuruhusu mawazo hasi kuingia kwenye akili yako. Hisia hasi kama za hasira, wivu, huzuni, hofu na hata kukata tamaa, hazipaswi kupata nafasi ndani yako.
Unapaswa kuwa bize na malengo na mipango yako ya kila siku kiasi kwamba mawazo na hisia hasi havipati nafasi kabisa kwenye akili yako. Na ukiweza kufanya hivi hutapata nafasi ya kuwa na huzuni au kupata sonona.
Zoezi la kufanya; kila wakati kagua mawazo na hisia ambazo unazo, je ni hasi au chanya. Kama ni hasi badili mara moja kwenda chanya. Huwezi kufanikiwa ukiwa na mawazo na hisia hasi. Lazimisha akili yako ifikiri chana na mara zote jiweke kwenye hisia chanya. Hili litakuwezesha kuona matumaini na kujituma zaidi.

Tuesday, December 18, 2018

TABIA 33 ZA WAJASIRIAMALI WENYE MAFANIKIO MAKUBWA.


1. Anzia sokoni, wengi huanza kufanya kitu kwa mapenzi yao wenyewe na siyo mapenzi ya soko. Kama unataka kufanikiwa, anza kujua watu wanataka nini kisha wape hicho wanachotaka.
 
2. Usiogope kushindwa, kabla hujafanikiwa, utakutana na vikwazo na changamoto mbalimbali, utashinda kwenye mengi, lakini kama hutakata tamaa, mwishowe utashinda.
 
3. Gundua fursa zilizojificha kwenye majanga mbalimbali. Unapokutana na majanga au changamoto, usiangalie upande wa matatizo, badala yake jiulize ni fursa gani iko hapa, na utaziona fursa nyingi zilizojificha kwenye majanga.
 
4. Toa thamani kubwa kwa wateja wako, wateja wataendelea kununua kwako kama kuna thamani wanaipata. Hakikisha mteja hakusahau kabisa, kwa namna unavyompa thamani ya kipekee.
 
5. Amka asubuhi na mapema, hii ni tabia moja ambayo itakupa ushindi mkubwa sana kwenye siku yako. Unapoamka mapema kuliko wengine na ukatumia muda huo kwa maandalizi na kufanya yaliyo muhimu, utaweza kupiga hatua sana.
 
6. Tenga muda wako na fanya jambo moja kwa wakati. Watu wengi huwa wanafikiria kufanya mambo mengi kwa pamoja ni kuokoa muda, lakini matokeo ni kinyume, kadiri mtu anavyofanya mengi kwa pamoja, ndivyo anavyopoteza muda na umakini wake. Kama unataka kukamilisha mengi, tenga muda wako na kisha fanya jambo moja kwa wakati.
 
7. Fanya mambo yanayoendana pamoja. Unapopanga ratiba ya kufanya vitu vyako, vile vitu ambavyo vinaendana, panga kuvifanya pamoja, hasa pale vitu hivyo vinapokuwa havihitaji umakini mkubwa. Kwa njia hii inakuwa rahisi kwako kukamilisha yale yanayoendana. Na hii haipingani na namba sita ya kufanya jambo moja kwa wakati, ila hapa unayaweka pamoja yale yanayoendana ili uweze kuyakamilisha.
 
8. Kuwa na mapumziko ya mara kwa mara. Kazi zetu nyingi tunafanya tukiwa tumekaa, hili linaleta uchovu na pia ni hatari kiafya. Suluhisho ni kuwa na mapumziko ya mara kwa mara ambapo unasimama na kutembea kidogo au kujinyoosha kabla ya kuendelea na jukumu jingine.
 
9. Kuwa na orodha mbalimbali, popote unapokuwa, kuwa na orodha unayofanyia kazi. Na unapopata wazo jipya, liandike mahali, usiamini kumbukumbu zako, utaishia kusahau mengi au kuijaza akili yako vitu visivyo muhimu kwenye kile unachofanya kwa wakati huo.
 
10. Weka malengo ambayo unaweza kuyafanyia kazi, malengo yanayopimika na unayoweza kuona ni wapi unakwenda na unafikaje pale. Bila ya malengo unayoweza kufanyia kazi, hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
 
11. Tumia vizuri muda wa uzalishaji mkubwa kwako. Kila mmoja wetu ana muda ambao anakuwa na uzalishaji mkubwa sana. Huu ni muda ambao akili ya mtu inakuwa inafikiri kwa umakini na mwili unakuwa na nguvu ya kutosha. Jua ni wakati gani wa siku unakuwa kwenye hali hii kisha weka yale majukumu muhimu kwenye muda huo.
 
12. Pima maendeleo yako kibiashara kwenye yale maeneo muhimu. Kila biashara ina maeneo yake muhimu, ambayo hayo yakienda vizuri basi biashara inakuwa ya mafanikio makubwa. Yajue maeneo muhimu kwenye biashara yako kisha pima maendeleo yako, pima hatua unazopiga ukilinganisha na malengo uliyojiwekea. Hii ndiyo njia rahisi ya kupima hatua unazopiga.
 
13. Epuka kujilisha vitu visivyo na maana. Habari, mitandao ya kijamii na kelele nyingine zimekuwa zinachukua muda wa wengi na wanashindwa kufanya yale muhimu. Epuka kujilisha vitu hivyo visivyo na maana na tumia muda wako kwa yale majukumu muhimu kwako.
 
14. Tengeneza muda wa kujitenga na teknolojia. Teknolojia zinarahisisha sana maisha, lakini pia zimekuwa usumbufu mkubwa sana kwenye maisha yetu. Tenga muda ambao utajitenga na teknolojia hizi, ili uwe na utulivu unaokuwezesha kufikiri kwa kina na hata kutekeleza majukumu ambayo ni muhimu kwako, yanayohitaji utulivu wa hali ya juu.
 
15. Weka mkazo kwenye uimara wako. Kuna maeneo ambayo una uimara na maeneo ambayo una udhaifu, unachopaswa kufanya ni kuweka mkazo kwenye uimara wako kuliko kukazana na madhaifu wako. Tafuta wenye uimara kwenye madhaifu wako na wape wafanyie kazi maeneo hayo.
 
16. Jitofautishe na wengine. Ukifanya kile ambacho wengine wanafanya utapata wateja wa kawaida. Ukifanya kile ambacho hakuna mwingine anayefanya utapata wateja wengi na wakipekee. Unapaswa kujitofautisha kabisa na wengine ili kupata wateja wa kipekee, ambao wanakuwa mashabiki wa biashara yako.
 
17. Tumia vizuri muda uliokufa kujifunza na kupiga hatua. Moja ya hitaji la kila mjasiriamali ni kuendelea kujifunza na kupiga hatua zaidi. Lakini mahitaji ya kila siku yanamfanya mtu akose kabisa muda wa kujifunza. Pamoja na majukumu mengi unayoweza kuwa nayo, bado kuna muda mwingi unaokuwa nao ambao huwezi kufanya chochote. Huu ndiyo muda uliokufa. Mfano muda unaokuwa kwenye foleni barabarani au kusubiri huduma fulani, muda unaofanya mazoezi au kufanya kazi zisizohitaji umakini mkubwa. Unaweza kutumia muda huo kujifunza zaidi.
 
18. Soma kwa dakika 30 kila siku. Huwezi kupiga hatua kama husomi na kujifunza, hivyo kila siku tenga angalau dakika 30 ambazo utazitumia kusoma. Na linda muda huo usiupoteze kwa kingine chochote. Hata kama una mengi kiasi gani, usikose kutenga muda wa kujisomea, ni muhimu sana kwa ukuaji wako.
 
19. Jifunze ujuzi mpya unaoweza kuutumia kuikuza biashara yako zaidi. Pamoja na kusoma kila siku, unahitaji kujifunza na kuongeza ujuzi ambao utaweza kuutumia kupiga hatua zaidi kibiashara. Biashara zinabadilika kila siku, ushindani unazidi kuwa mkali, unapaswa kuwa na ujuzi wa ziada ambao utakuwezesha kupiga hatua zaidi.
 
20. Kamata mawazo bora yanayokujia kwenye siku yako kwa kuyaandika chini kabla hujayasahau. Unaweza kufanya hivi kwa kuwa na kijitabu kidogo na kuandika, au pia unaweza kutumia simu yako kuandika mawazo unayokutana nayo. Usikubali wazo lolote linalokujia likupotee.
 
21. Tengeneza na kuza mtandao wako. Huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe, unahitaji msaada wa wengine ili kuweza kufanikiwa. Hivyo unahitaji kutengeneza na kukuza mtandao wako wa kibiashara. Utengeneze mahusiano bora na wafanyabiashara ambao wanapiga hatua zaidi ambao watakusukuma na wewe upige hatua zaidi.
 
22. Timiza ahadi unazotoa. Njia rahisi ya kuwapoteza wateja kwenye biashara ni kuwaahidi vitu halafu usivitekeleze. Jijengee sifa nzuri kwenye biashara yako kwa kuwa mtekelezaji wa kila unachoahidi, kwa kufanya hivyo wateja wanakutegemea na kukuamini.
 
23. Tumia nguvu ya HAPANA. Kinachowafanya wengi kushindwa kutimiza ahadi wanazotoa ni kusema NDIYO haraka bila ya kufikiri kwa kina. Kadiri unavyokubali mambo mengi, ndivyo unavyotawanya muda na nguvu zako na ufanisi wako unashuka. Jifunze kusema HAPANA ili kuweka mkazo kwenye yale maeneo muhimu ya biashara yako. Kama kitu siyo muhimu sema HAPANA, na usione aibu waka kuogopa.
 
24. Kuwa kiongozi na siyo meneja. Unapowaajiri watu wakusaidie kazi kwenye biashara yako, kuwa kiongozi kwa kuwahamasisha kuchukua hatua na kuwapa uhuru wa kuweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yao. Usiwe meneja ambaye kila kitu kwenye uchukuaji hatua unakisimamia wewe na mtu hawezi kufanya kitu mpaka wewe umwelekeze kwanza. Hilo litakuchosha sana.
 
25. Jifunze kuongea. Mtu anayeweza kuongea kwa kujiamini kuhusu kile anachouza anaaminika zaidi na wateja. Na asiyeweza kuongea vizuri, hata kama anauza kitu kizuri, wateja hawatamwamini sana. Jifunze jinsi ya kuongea vizuri, kwa ushawishi na ubobezi na utawafanya watu waamini kwenye kile unachowaelezea.
 
26. Jifunze kusikiliza. Kuongea tu hakutakusaidia sana kama hutakuwa msikilizaji, jifunze kusikiliza pale wengine wanapoongea. Na siyo unasikiliza tu kwa masikio, bali pia unaangalia lugha za vitendo ambazo mwongeaji anakuwa anatumia, hivi ni viashiria ambavyo vitakueleza mengi zaidi.
 
27. Fanya mazoezi mara kwa mara. Mazoezi ya viungo yana manufaa makubwa sana kwako kiafya na kiufanisi kwenye majukumu yako, hivyo tenga muda wa kufanya mazoezi kila siku. Ukiweza kupata dakika 30 za mazoezi kila siku, utapunguza hatari ya magonjwa kama kisukari na presha, na pia utaongeza ufanisi wako kwenye kazi zako. Pia tafiti zinaonesha watu wanaofanya mazoezi wana kipato kikubwa kuliko watu wasiofanya mazoezi. Hebu anza kufanya mazoezi kila siku na utashangaa jinsi kipato chako kitakavyoanza kuongezeka.
 
28. Ishi maisha bora kiafya. Mazoezi ni hatua moja ya kuwa na afya bora. Hatua nyingine ni ulaji na kujikinga na hatari za magonjwa. Kula kiafya, epuka vyakula vya haraka, epuka vilevi, sigara, madawa ya kulevya na jiepushe na vihatarishi vya magonjwa. Afya yako ni mtaji muhimu sana kwako, isipokuwa imara hutaweza kufanya chochote kikubwa.
 
29. Pata usingizi wa kutosha. Wajasiriamali wengi hujisifia kwa jinsi wanavyoweza kulala kidogo na kufanya kazi masaa mengi. Usiingie kwenye mtego huo, hakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala, kulingana na uhitaji wa mwili wako. Miili yetu inatofautiana, kwa wastani masaa nane yanashauriwa kiafya, lakini wapo wanaohitaji machache zaidi ya hayo na wapo wanaohitaji mengi zaidi. Hivyo jua uhitaji wa mwili wako, kama masaa nane ndiyo yanakutosha basi pata masaa nane. Kama masaa 6 au 7 yanakutosha pata muda huo wa kulala. Kitu muhimu zaidi kupima kwako siyo masaa mangapi hujalala, bali umezalisha nini kwenye muda wako. Kadiri unavyopumzika zaidi, ndivyo unavyoweza kuzalisha zaidi.
 
30. Fanya tahajudi au kuandika jarida lako kila siku. Tahajudi ni zoezi ambalo huwa linafanywa na karibu dini na falsafa zote. Kila dini au falsafa watu wana utaratibu wao wa kutuliza fikra zao na kutafakari yale muhimu. Pia unaweza kuandaa zoezi lako la tahajudi kwa kutafakari yale muhimu zaidi kwako. Pia unaweza kufanya zoezi la kuandika jarida lako kila siku, kila siku unakaa chini na kuandika mawazo yako kwenye kijitabu chako, kwa njia hii unapata utulivu wa kipekee kwako.
 
31. Fanya kile unachopenda kufanya. Pamoja na kuwa kwenye biashara, unapaswa kutenga muda wa kufanya kile unachopenda kufanya, ambacho hakihusiani na biashara yako. Hupaswi kuwa mtu wa kufanya na kufikiria kazi muda wote. Tenga muda wa mapumziko ambao utautumia kufanya vile vitu unavyopenda kufanya, ambavyo havihusiani na kazi au biashara yako.
 
32. Wasaidie wengine. Ni rahisi kukazana na malengo ambayo umejiwekea na kuona huna muda wa kuwasaidia wengine. Lakini njia rahisi ya kupata chochote unachotaka ni kuwasaidia wengine kupata kile wanachotaka. Mara kwa mara jitolee kufanya kazi za kijamii, wasaidie wanaoweza na hata biashara yako iwe ina lengo la kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na siyo tu kupata faida.
 
33. Jiamini. Kadiri unavyokuwa kwenye ujasiriamali, ndivyo hali ya wasiwasi inavyojijenga ndani yako. Unapata hali fulani ya hofu kwamba huenda mafanikio unayopata ni bahati tu na ipo siku mambo yatabadilika na kila mtu atagundua kwamba hukuwa na mafanikio halisi bali bahati tu. Jua hali hii humpata kila anayepiga hatua za mafanikio, na njia pekee ya kuishinda ni kujiamini wewe mwenyewe. Hata kama kuna bahati umekutana nayo, amini juhudi na maandalizi uliyoweka yamekusaidia. Na pia jua hata kama utapoteza kila ulichonacho, utaweza kuanza tena na kufanikiwa.

Wednesday, December 5, 2018

TEGEMEA NGUVU ZAKO NA SIYO HURUMA ZA WENGINE.

Kwenye MAISHA, kwa chochote unachochagua kufanya basi unapaswa kutegemea zaidi nguvu zako, uimara wako na siyo kutegemea huruma za wengine. Kila unapoanza kutegemea huruma za wengine, ndipo unapoingia kwenye shimo zaidi na kukosa uhuru wako.
 
Kila unapokuwa unategemea wengine wafanye kitu ndiyo wewe uweze kupata unachotaka, utajikuta unakosa uhuru wa kuishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
 
Kwa sababu yeyote yule unayemtegemea sana, ambaye huwezi kupiga hatua fulani bila yeye, anageuka na kuwa kikwazo kwako, kwa sababu asipofanya kama unavyotegemea, basi wewe hutaweza kupata kile unachotaka kupata.
 
Unapaswa kuyatengeneza maisha yako kwenye msingi huu wa KUJITEGEMEA binafsi kwenye mambo mengi ya maisha yako, kujua namna ya kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kutoruhusu mtu mmoja au watu wachache wawe na maamuzi ambayo yanaweza kuathiri sana maisha yako.
 
Kama maisha yako yanategemea sana maamuzi ya mtu mmoja au watu wachache, utakosa uhuru mkubwa kwenye maisha yako, kwa sababu hata kama mtu huyo hakusumbui, bado ndani yako utakosa amani, kwa sababu hujui ni namna gani mtu huyo anaweza kubadilika siku za mbeleni.
 
Maisha ya uhuru kamili, maisha ya kupata kile unachotaka ni kuweza kutumia uwezo wako mkubwa, kutengeneza maisha ambayo hayana utegemezi mkubwa kwa mtu mmoja au watu wachache. Hilo linajumuisha hata wewe binafsi.
 
Kwa mfano kama kipato chako kinategemea wewe ufanye kazi, bado hujawa huru, kama huwezi kuingiza kipato hata kama wewe hufanyi kazi, unaendelea kuwa mfungwa kwenye upande wa kipato. Lazima uwe na mfumo huru unaoweza kutengeneza kipato iwe unafanya kazi au la.
 
Una uwezo mkubwa sana ndani yako, una nguvu kubwa sana ambazo kama utaanza kuzitumia, utayabadili sana maisha yako, utawafanya wengine wakutegemee wewe zaidi kuliko unavyowategemea wao. Na kadiri wengi wanavyokutegemea wewe, ndivyo unavyokuwa huru zaidi.
 
Na hili ni zuri na muhimu sana kwa wale watu ambao wanapenda kufanya kazi zao za ajira, lakini wanapenda kuwa huru. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anapenda kufanya kazi fulani, lakini ataifanya vizuri kama atakuwa ameajiriwa sehemu fulani. Kwa mtu huyu kutumia vizuri uwezo wake mkubwa na nguvu zake, anajitengenezea hali ya kutegemewa kwenye kile anachofanya, kitu ambacho kinamfanya aheshimiwe na kuwa na uhuru zaidi kuliko wale ambao hawategemewi na badala yake wanategemea zaidi kazi wanayofanya

PATA MUDA WA KUKAA MWENYEWE KWENYE CHUMBA KWA UTULIVU. USIJIOGOPE WEWE MWENYEWE.

Mwanasayansi na hisabati Blaise Pascal aliwahi kusema matatizo yote ya binadamu yanatokana na mtu kushindwa kukaa mwenyewe kwenye chumba kwa utulivu.
 
Na hili ni sahihi kabisa, kinachowafanya watu wengi kuingia kwenye matatizo mbalimbali, ni kushindwa kutulia na mawazo yao, kukosa ujasiri wa kukaa na kutafakari chochote walichonacho kwenye mawazo yao.
 
Mimi nakwenda mbali na kusema kwamba watu wengi tunajiogopa sisi wenyewe. Ndiyo maana tukikutana na upweke tu tunakimbia haraka sana.
 
Kama unabisha jiangalie tu tabia yako, huwa unafanya nini pale unapojikuta upo mwenyewe. Lazima utatafuta kitu cha kuchukua muda wako na kushika mawazo yako. Labda utaanza kuchezea simu, utaanza kusoma kitu au hata kuwatafuta watu ambao hukuwa umepanga kuwatafuta.
 
Yote hayo ni kuepuka tu kuwa peke yako, upweke umekuwa hofu kubwa kwetu, hatutaki kabisa kukaa wenyewe, tukiwa tumeachwa na fikra zetu.
 
Rafiki, hebu acha kujiogopa, hebu rudisha urafiki kwako binafsi. Unapopata nafasi ya kuwa na upweke, itumie hiyo kuyatafakari maisha yako, itumie hiyo kujijengea taswira ya kule unakoenda.
 
Usijiogope na kukimbia kila unapojikuta mpweke, badala yake tumia nafasi hiyo kujenga urafiki na wewe binafsi na hata kujijua zaidi na kujua kwa kina kule unakokwenda.

Friday, November 30, 2018

SAFARI YA MAFANIKIO INAANZA NA WATU WENGI SANA. WENGI HUISHIA NJIANI, KWANINI ??


Watu wengi wanakata tamaa kwenye safari ya mafanikio kwa sababu ya kutokujua kwamba mafanikioo yanataka muda mrefu. Katika kipindi cha kutafuta mafanikio yako unatakiwa ujitoe hasa, kuvumilia na kutoa kila ulichonacho hadi ufanikiwe.
Kwa mfano, ilichukua muda wa miaka 11 hadi program ya ‘Microsoft’ ya bilionea mkubwa duniani kuanza kufanya kazi na kuleta mafanikio makubwa. Mafanikio yake hayakutokea tu ghafla kuna miaka ilikataika hapa katikati.
Pia ilimchukua miaka 29 kwa Abraham Lincoln hadi kuweza kuwa Rais wa marekani. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba mafanikio si kitu cha mara moja tu, unatakiwa kuwekeza muda ili uweze kufanikiwa kwenye mafanikio hayo uyatakayo.
Kwenye akili yako sasa weka wazi, mafanikio ni safari ya muda mrefu. Unatakiwa kabisa utenge miaka angalau kuanzia 5 hadi 15 ya kutafafuta mafanikio yako ya kweli na ya kudumu. Ukikurupuka na kutaka mafanikio ya chapu chapu utakwama.
Kama utakuwa ni mtu wa kutaka mafanikio na halafu ukategemea mafanikio hayo yakatokea ghafla ghafla kwa muda mchache ni rahisi sana kwako kuweza kukata tamaa na kuona ni kitu ambacho hakiwezekani au mafanikio ni ya watu wa aina fulani tu lakini si wewe.

JIWEKEE MUDA WA UKOMO KWA CHOCHOTE UNACHOPANGA KUFANYA.

Mtu mmoja amewahi kusema kwamba jukumu huwa linachukua muda uliopangwa lifanyike. Akimaanisha kama kuna jukumu ambalo linapaswa kufanywa kwa masaa mawili, litakamilika ndani ya masaa mawili. Jukumu hilo hilo likipangwa kufanyika ndani ya masaa matano, litachukua masaa matano.
Huwa tunasukumwa kufanya zaidi pale ambapo muda unakuwa mdogo, na tunaahirisha mambo pale muda unapokuwa mwingi. Ndivyo maana wanafunzi ni vigumu sana kusoma siku za kawaida, lakini mtihani unapokaribia, hamasa ya kusoma inakuwa juu.
Jiwekee muda wa ukomo kwa chochote unachopanga kufanya, na muda huo uwe mfupi kuliko muda uliozoeleka. Kwa kuwa na muda huu na kuufuata, utaweza kujisukuma kufanya zaidi. Kadiri unavyokuwa na muda mfupi wa kutekeleza jambo, ndivyo mawazo ya kuahirisha yanavyopotea kwenye akili yako. Waahidi watu kwamba jukumu litakamilika mapema kuliko kawaida, na tekeleza hilo uliloahidi.