Monday, April 6, 2020

UMEZALIWA ILI UFANIKIWE / YOU ARE BORN TO SUCCEED . HUFANIKIWI KWA SABABU ZIFUATAZO :--

 Mambo kumi ( 10 ) unayopenda kufanya kila siku, ambayo yanakuzua isifikie ushindi wako :--
( 1 ). HUJACHAGUA  KUWA  MSHINDI.
Hatua ya kwanza kuchukua ili kufikia ushindi kwenye maisha yako, ni kuchagua ushindi unaotaka kwenye maisha yako. Upo usemi kwamba kama hujui unakokwenda, njia yoyote itakuwa sahihi kwako. Hivi ndivyo wengi wanaendesha maisha yao, hawajui wanataka nini, ila wako bize kweli kweli.
Chagua leo unataka ushindi wa aina gani kwenye maisha yako ili uweze kuchukua hatua sahihi za kukufikisha kwenye ushindi huo.
( 2 ). HUJACHUKUA  JUKUMU  LA  MAISHA  YAKO.
Kama umewahi kulalamika au kumlalamikia mtu mwingine juu ya jambo lolote linalohusu maisha yako, basi jua unajizuia kushinda. Washindi wanachukua jukumu la maisha yao kwa asilimia 100. Chochote kinachotokea kwenye maisha yao, wanajua wa kwanza kulaumiwa na kulalamikiwa ni wao wenyewe. Kulalamika na kulaumu ni rahisi, lakini inakufanya ujione usiye na hatia na uwezo wa kupambana kwenye maisha yako.
Amua leo kushika hatamu ya maisha yako, chukua jukumu la maisha yako kwa asilimia 100 kwa kutokulalamika au kumlaumu yeyote.
(3 ). HUAMINI  KWAMBA  UNAWEZA  KUSHINDA / KUFANIKIWA.
Unapokutana na changamoto kidogo, unakata tamaa na kuona safari ya mafanikio haiwezekani. Watu wanapokupinga na kukukosoa unawasikiliza na kuona wapo sahihi kuliko wewe. Na hilo limekuwa kikwazo kwako. Ushindi unataka ujiamini kupitiliza, uamini unaweza kufanya chochote unachopanga, licha ya ugumu au changamoto unazopitia. Na ukweli ni kwamba, ukiamini na kuamua, hakuna kinachoshindikana.
Jiamini kwamba unaweza kushinda, licha ya magumu na changamoto unazopitia, endelea kuweka juhudi na utafikia ushindi mkubwa. 
( 4 ). HUNA  MALENGO  YANAYOPIMIKA.
Dhana yako ya malengo ni potofu, kwa sababu unajiambia tu kwamba mwaka huu nitafanikiwa zaidi, nitaongeza kipato, nitaanzisha biashara na kadhalika. Kujiambia kauli kama hizo siyo malengo, bali ni matamanio. Malengo ni pale unapopanga nini unataka, kwa kiwango gani na kufikia lini. Kama umepanga kuanza biashara, unajiambia kabisa ni biashara ya aina gani na utakuwa umeianza kufikia tarehe gani. Kama huwezi kupima malengo, huwezi kuyafikia.
Weka malengo yanayopimika na kila siku jipime kwa malengo hayo, gawa malengo hayo kwenye hatua za kuchukua na kila siku chukua hatua hizo bila kuacha na utafika kwenye ushindi.
( 5 ) . UMEKOSA   UAMINIFU.
Umekuwa unasikiliza kauli za wale walioshindwa, ambao wanaamini wale waliofanikiwa kuna namna wamefanya. Utawasikia masikini wakisema matajiri ni wezi na walaghai. Utawasikia wasioweka juhudi wakisema waliofanikiwa wana bahati. Wengine wanakuja kwako na njia za mkato za kufanikiwa, ambazo hazihitaji kazi yoyote. Wewe kwa kutokuijua misingi ya mafanikio, unaingia kwenye mitego hiyo, kinachotokea ni unajikuta unapoteza muda wako na hakuna hatua unazopiga.
Chagua kuwa mwaminifu, kufanya kile kilicho sahihi kulingana na misingi ya mafanikio na siyo kudanganyika au kufuata mkumbo. Njia zisizo sahihi zinaweza kukupa ushindi, lakini hautadumu. 
(6). HUWEKI  KAZI.
Umesikiwa watu wanakuambia usifanye kazi kwa nguvu, bali fanya kwa akili, wana kiingereza chao wanakuambia Don’t work hard, work smart. Ni uongo, hakuna ushindi unaopatikana bila kuweka nguvu na akili, tena kwa viwango vya juu sana. Watu wengi ni mashabiki na wafuatiliaji wa michezo mbalimbali. Nitajie mchezaji mmoja unayemkubali sana, ambaye wakati wenzake wanaenda kwenye mazoezi ya nguvu, yeye anafanya mazoezi kwa akili? Hakuna. Halafu wewe unajidanganya kwamba unaweza kufikia ushindi kwa akili bila nguvu!
Amua kuweka kazi, kazi hasa na siyo ya kitoto. Fanya kazi kwa juhudi na maarifa, nenda hatua ya ziada, toa thamani kubwa na ushindi utakuwa wako.
(7 ). HUTHAMINI  MUDA  WAKO.
Unauchukulia muda wako poa sana, unautawanya kama vile una chemchem ya muda isiyo kauka. Unapoteza muda wako wa thamani kwenye mambo yasiyo na mchango wowote kwenye ushindi wako, kwa sababu hujui hata thamani ya muda huo. Unahangaika na habari mbalimbali, umbeya, udaku, maisha ya wengine na mengine mengi. Halafu unakuja kulalamika kwamba huna muda wa kufanya zaidi yale uliyopanga kufanya.
Upe muda wako thamani, jua ni kiasi gani cha kipato unataka kupata, kisha kigawe kwa masaa na jua saa yako moja ina thamani ya shilingi ngapi. Hivyo unapopoteza muda, unajua kabisa ni kiasi gani cha pesa umepoteza.
(8 ). UNASIKILIZA  SANA  HOFU  ZAKO.
Hakuna mtu asiyekuwa na hofu, ila wewe unazisikiliza sana hofu zako, hivyo huthubutu kufanya kitu chochote kipya na kikubwa, kwa sababu unahofia kushindwa. Wanaoshinda wanapata hofu kama zako, lakini wanajua dawa ya hofu ni kufanya. Kuwa na hofu ni kawaida, ila kuzisikiliza hofu zako na kuzifuata ni kuchagua kuukosa ushindi.
Amua leo kuchukua hatua kwenye yale unayohofia, kwa sababu ndiyo yamebeba mafanikio yako na dawa ya hofu ni kufanya unachohofia.
( 9 ). HUJIFUNZI  KILA  SIKU.
Unapata muda wakula mara tatu kwa siku, kufuatilia habari, kufuatilia maisha ya wengine na kulala, lakini unajiambia huna muda wa kusoma vitabu. Hapo ndipo unapoagana na ushindi wako. Kwa sababu hakuna mshindi ambaye hajifunzi kila siku. Moja ya mahitaji ya maisha ya ushindi ni kila siku kuwa bora kuliko siku iliyopita, na ubora pekee utaupata kupitia kujifunza kila siku na kufanyia kazi yale unayojifunza.
Chagua sasa kujifunza kila siku, haijalishi siku yako imebana kiasi gani, hakikisha unatenga muda wa kujifunza kupitia usomaji wa vitabu na mafunzo ya aina nyingine. Usikubali siku ipite hujajifunza kitu kipya.
( 10 ). BADALA  YA  KUZALISHA  MATOKEO , UNAZALISHA  SABABU.
Kabla hata hujaanza kufanya kitu, tayari umeshatengeneza sababu za kujitetea utakaposhindwa kwenye kitu hicho. Hivyo badala ya kuweka nguvu zako kubwa kuzalisha matokeo ya ushindi unayotaka, unapeleka nguvu hizo kuzalisha sababu za kujitetea. Huwezi kuzalisha sababu na matokeo kwa pamoja, chagua kuzalisha sababu na kuachana na matokeo au kuzalisha matokeo na kuachana na sababu.
Kataa kuwa mtu wa sababu, kuwa mtu wa kujisukuma kwa kila namna kupata matokeo unayotaka, usiwe mtu wa kukimbilia sababu.

1 comment:

  1. Nashukuru mwl.wangu nimejifunza kipande hiki nimepata mwanga juu ya hofu zangu,nitawasiliana nawe kwa NJIA ya WhatsApp ili kujifunza zaidi,Mungu wa mbinguni akulinde na kukubariki milele.

    ReplyDelete