Hofu ni kama magugu shambani, huwa yanaanza kidogo kidogo na yasipodhibitiwa yakiwa madogo, baadaye yanakuwa makubwa na kuharibu kabisa mazao.
Kadhalika, hofu huanza kidogo kidogo ndani yetu, lakini zisipodhibitiwa zikiwa ndogo, zinakua na kuzaliana kiasi cha mtu kushindwa kuchukua hatua kabisa.
Hivyo pale unapokuwa na hofu ya kufanya kitu, unapaswa kuanza kukifanya hapo hapo ili kuidhibiti hofu hiyo. Kwa sababu njia pekee ya kuishinda hofu ni kufanya kile unachohofia.
Unapofanya, unagundua vitu vingi ulivyokuwa unahofia havijatokea. Mara nyingi hofu ni hadithi tunayojielezea sisi wenyewe kwenye vichwa vyetu, ambayo siyo ya kweli.
Jiwekee utaratibu wa unapopata hofu ya kufanya kitu, basi unakifanya hapo hapo bila ya kusubiri. Mfano kuna mtu unataka kumuuliza kitu, lakini unapata hofu atakuchukuliaje, hapo hapo muulize mtu huyo kitu unachotaka kuuliza na utashangaa utakavyopata majibu bora kabisa. Na hata kama hutapata majibu unayotarajia, bado hakuna madhara yoyote unayokuwa umeyapata.
Ni wakati sasa wa kuacha kujidanganya na kuwa watu wa kuchukua hatua kwa kila tunachokutana nacho na tukakihofia.
Dawa ya hofu ni kuikabili ikiwa ndogo kabla haijaota mizizi na kuwa sugu.