Sunday, September 2, 2018

JINSI YA KUDHIBITI TABIA YA KUNUNUA VITU OVYO ! KWA KUTUMIA SHERIA YA SIKU 30 KWENYE FEDHA.

Moja ya tatizo kubwa ambalo watu wanalo kwenye fedha ni kushindwa kudhibiti matumizi. Watu wanapokuwa na fedha, na wakakutana na kitu kizuri, wanajikuta wameshanunua.
Ndiyo maana watu wanaishia kuwa na nguo ambazo hawazivai, vitu ambavyo hawavitumii, lakini wamenunua. Ukiwauliza kwa nini walinunua hata hawawezi kukupa jibu la wazi. Wengine watakuambia ilikuwa rahisi na wasingeweza kupata kwa bei rahisi vile. Wengine watakuambia wanajua watakuja kuhitaji kitu hicho siku moja.
Haijalishi unajifariji kwa maneno gani, kama umenunua kitu ambacho hukitumii sana, umepoteza fedha. Au kama umenunua kitu, lakini inakulazimu ukitumie ili usijione umepoteza fedha, jua umeshapoteza fedha.
Sasa, ipo sheria inayoweza kukusaidia usirudie tena makosa uliyofanya huko nyuma ya kununua kitu ambacho hukitumii. Sheria hiyo ni sheria ya siku 30.
Sheria hii inasema kwamba, kama umekutana na kitu na ukajishawishi unahitaji kukinunua, usikinunue hapo hapo. Badala yake andika mahali kwamba unataka kununua kitu hicho, kisha subiri kwa siku 30 kabla hujakinunua. Sasa kama siku 30 zitaisha na bado ukawa unauhitaji mkubwa wa kitu hicho, au hata siku 30 hazijaisha uhitaji unakuwa mkubwa mno la sivyo maisha hayawezi kwenda, nunua kitu hicho.
Rafiki, kwa sheria hii, usijidanganye kwamba hii ni bei rahisi na hutapata tena, au kitu hicho ni cha mwisho na hakitapatikana tena. Sheria ni moja, subiri siku 30 zipite na utanunua.
Kitu ambacho utanufaika nacho kwenye sheria hii ni kwamba baada ya siku tatu kupita, wala hata hutakumbuka kama ulipanga kununua kitu hicho.

 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki  /+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment