Sunday, September 16, 2018

JIFUNZE KUJITHIBITI, KUWA HALISIA , KUJITAMBUA ,KUJIENDELEZA UTAFANIKIWA SANA KIMAISHA.

(1).  KUJIDHIBITI
Eneo la kwanza kabisa unalohitaji kulifanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni kwenye udhibiti. Unahitaji kujidhibiti wewe mwenyewe, la sivyo utawapa wengine nafasi ya kukudhibiti wewe. Unahitaji kujipangia nini utafanya na kipi hutafanya na kufuata mpango huo.
Muda ulionao kila siku ni mfupi sana, ni muda ambao kama ukiweza kujidhibiti utaweza kufanya makubwa. Lakini ukishindwa kujidhibiti, utashangaa muda unaisha na hakuna ulichofanya. Lazima uweze kujiambia HAPANA wewe mwenyewe, pale unapojiona unakosa udhibiti. Pia lazima uweze kujiadhibu wewe mwenyewe pale unapokwenda kinyume na mipango uliyojiwekea wewe mwenyewe.
Jidhibiti wewe mwenyewe na kila siku yako itakuwa siku ya ushindi, kwa sababu utafanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

(2). KUWA  HALISIA / ACHA MAIGIZO
Kitu kimoja ambacho dunia inakazana sana kufanya kwako ni wewe uwe kama wengine. Kwa sababu dunia inajua ukiwa wewe, utakuwa msumbufu, hutafaa kutawaliwa na hivyo inakazana sana uwe kama wengine, uwe ndani ya kundi ili uweze kutawaliwa na kutumiwa vizuri na wengine.
Hivyo eneo la pili la kufanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni uhalisi. Unapaswa kukazana kuwa halisi kila siku, kuishi maisha yako kwa uhalisia, kuacha kuigiza na kuacha kufanya vitu ili kuwaridhisha wengine au uonekane na wewe unafanya.
Hutaweza kufanikiwa kama huishi maisha halisi kwako, hata kama utapata vitu vingi kiasi gani, kama maisha unayoishi siyo halisi kwako, kila mara utasikia sauti inakuambia wewe bado sana. Na hapa ndipo wengi husema wamefanikiwa lakini hawana furaha.
Shida yao ni moja tu, maisha wanayoishi siyo halisi kwao, ni maisha feki na hivyo mafanikio yoyote wanayopata yanakuwa yanaonekana na wengine lakini siyo ndani yao binafsi.
Kuwa halisi kwako, jua uimara wako, jua madhaifu yako, jua yapi yenye maana kwako na jua kusudi la maisha yako ni lipi. Kisha tumia kila dakika ya siku yako kuishi maisha ambayo ni halisi kwako. Utafanikiwa kariri unavyoishi maisha halisi kwako.

(4). JITAMBUE.
Kujitambua ni eneo muhimu sana la kufanyia kazi, na linatangulia uhalisia. Kwa sababu bila ya kujitambua, hutaweza kuishi uhalisia wako. Na changamoto ya kujitambua ni kwamba ni zoezi endelevu.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri wakishajua wanataka nini kwenye maisha yao, wakishaweka malengo makubwa basi wamemaliza. Hiyo siyo sahihi, unachojua leo kuhusu wewe, kinaweza kuwa tofauti kabisa na utakachotambua kesho kuhusu wewe.
Kubadili mazingira, kukutana na changamoto, kote huko kutakufunulia kwa undani kuhusu wewe. Mara nyingi huwezi kujua una uwezo wa kufanya makubwa kiasi gani mpaka pale unapokutana na changamoto kubwa kwenye maisha yako.
Hivyo zoezi la kujitambua ni endelevu, kila siku, kwa kila unachopitia, jiulize ni kipi kipya umejua kuhusu wewe. Na wakati mzuri wa kujipima ni pale unapopitia mambo magumu. Utaweza kupima uwezo wako wa kudhibiti hasira pale unapokasirishwa hasa. Unaweza kujua unaweza kuvumilia ugumu kiasi gani pale unapokutana na ugumu zaidi.
Kila siku mpya ya maisha yako ni siku ya kujitambua zaidi, ishi kila siku kwa kutaka kujitambua na maisha yako yatakuwa bora sana.


(4).KUJIENDELEZA.
Eneo la nne ambalo unapaswa kulifanyia kazi kila siku ni kujiendeleza wewe binafsi. Kila siku lazima ukazane kuwa bora zaidi kuliko siku iliyopita. Kila siku unapaswa kujifunza kitu kipya. Usikubali siku iishe ukiwa kama siku ya jana ilivyoisha.
Weka kipaumbele kwenye kujifunza. Jifunze kupitia kusoma, kusikiliza, kuangalia na hata kufanya. Soma vitabu, sikiliza mafundisho mbalimbali, waangalie wengine kwa namna wanavyofanya na jaribu vitu vipya kwa ajili ya kujifunza kwa kufanya.
Jinsi unavyojifunza kila siku, unazidi kuwa bora na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Rafiki yangu mpendwa, maeneo haya manne ni muhimu sana kwako kuyafanyia kazi kila siku. Ninaposema kila siku, namaanisha kila siku ya maisha yako. Na usiache hata siku moja, mpaka siku unaondoka hapa duniani.
Kama unajiambia huwezi kila siku, kama unajiambia utajisahau au kupitiwa na maisha mengine, ninayo nafasi ya kukumbusha hili kila siku, na kukushirikisha fursa za kujifunza na kujitambua kila siku. Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utapata nafasi ya kuingia kwenye kundi la wasap, na kila siku utajifunza kwenye maeneo hayo manne na mengine mengi.


 Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment