Sunday, June 12, 2016

MBINU ZA KUBADILISHA TABIA MBOVU



Kwenye kitabu nilichosoma hivi karibuni, The Power of Habit (Kwa Kiswahili: Nguvu ya Kubadilisha Tabia) mwandishi Charles Duhigg anatoa somo juu ya namna ya kubadilisha tabia zisizofaa.
Ni kitabu kilichochapishwa mwaka 2012 na kampuni ya Random House Trade Paperbacks ya New York nchini Marekani na kimewahi kuongoza kwa mauzo kwenye orodha ya vitabu vyenye mauzo makubwa vinavyoorodheshwa na Gazeti la New York Times.
Swali la msingi analouliza mwandishi, na ambalo analitafutia jibu ni: kwanini tunafanya vitu ambavyo tunafanya? Majibu anayotoa yanarahisisha kubadilisha tabia mbovu.
Wote tunatambua kuwa ziko tabia kuu mbili: nzuri na mbaya. Duhigg anamwambia msomaji kuwa hakuna tabia mbovu ambayo haiwezi kubadilishwa. Na jambo kuu la kuweza kubadilisha hizi tabia ni, kwanza, kutambua hulka ya tabia na jinsi gani zinashamiri na; pili, kuweka nia ya kuzibadilisha.
Mwandishi ameandika kitabu kutokana na utafiti wake mwenyewe, lakini ametumia zaidi matokeo ya utafiti wa kina ambao umefanyika kubaini sababu za kuwapo au kutokuwapo kwa tabia zisizofaa.
Tabia zisizofaa tunazihusisha zaidi na mwanadamu, lakini yapo makundi mawili yanayohusishwa na tabia: tabia za taasisi au mashirika, na tabia za jamii. Na kote huku anasisitiza mwandishi, kwa kutumia mifano mingi, hata taasisi/mashirika, na jamii zinaweza kuwa na tabia mbaya, na zinaweza kuweka mikakati ya kubadilisha hizi tabia.
Lakini kwa kuwa mhusika mkuu katika maeneo yote haya matatu ni mwanadamu, basi ni dhahiri kuwa mwenye ufunguo wa kuibua tabia chanya ndani ya taasisi/mashirika na jamii ni mwanadamu huyo huyo.
Kimsingi, tabia ni mchakato wenye hatua tatu. Ubongo umeundwa kukwepa kufanya kazi ngumu ya kufikiri kila wakati, kwa hiyo ili kuongeza ufanisi wake, na ili ubongo utumike pale inapolazimu tu, ipo sehemu ya ubongo inayoitwa basal ganglia ambayo huweka kumbukumbu za tabia tunazojenga.
Hatua ya kwanza ya mchakato unaokamilisha tabia inaanzishwa na kichocheo. Katika hatua ya pili, kichocheo kinasababisha tufuate desturi iliyohifadhiwa ndani ya basal ganglia na inayohusishwa na kichocheo hicho mahsusi. Unaweza kufananisha basal ganglia na maktaba ya kanda zinazohifadhi desturi zetu, na kila tunapoona, kugusa, kusikia, au kunusa kichocheo fulani basi kile kichocheo kinaoanishwa na kanda mahsusi ya kichocheo hicho. Kumbukumbu ya hiyo kanda inatufanya tufuate desturi fulani.
Hatua ya mwisho ya mchakato wa tabia ni manufaa ambayo tunayapata kutokana na kutekeleza wa hiyo desturi ya hatua ya pili.
Wengi tunakubaliana kuwa tabia ambayo haina mtetezi ni unywaji pombe uliokithiri. Pamoja na kuwa upo ukweli kuwa ni tatizo ambalo linasababishwa zaidi na masuala ya afya ya akili, bado tunaambiwa na mwandishi kuwa upo mchakato wa kitabia wenye hatua tatu ndani ya unywaji pombe na ambao unaweza kubadilishwa na kumwepusha mtu na unywaji pombe. Wengi wanaokunywa pombe hawanywi kwa sababu ya kutaka kulewa, bali hutafuta manufaa (hatua ya tatu) kama kujaribu kusahau matatizo, kupumzisha akili, kupata watu wa kuongea nao, au kukwepa jambo fulani linalowasumbua.
Katika kuweka nia ya kubadilisha tabia, hatua ya kwanza (kichocheo) na ya tatu (manufaa) havibadiliki. Tunachojaribu kufanya ni kubadilisha hatua ya pili (desturi). Kwa mfano, kama kichocheo ni msongo wa mawazo na huo ndio unatuchochea kwenda hatua ya pili ya kukaa kwenye baa na kuanza kunywa pombe, suluhisho ni kubadilisha desturi ya kuhamia kwenye baa na kuweka desturi nyingine ambayo italeta manufaa yale yale ya hatua ya tatu.
Badala ya msongo wa mawazo kusababisha kwenda baa kutafuta watu wa kuongea nao, desturi ya kwenda baa inabadilishwa na desturi ya kutafuta ndugu, jamaa, na marafiki ambao kwa kuzungumza nao mwathirika anaweza kupata faida ile ile ya kupata watu wa kuzungumza nao.
Ukitaka kumchekesha mlevi mwambie anaweza kuacha kunywa pombe kwa kuacha kwenda baa kupiga gumzo na wanywaji wenzake, na badala yake azunguke kwa majirani na kuongea nao na kuwa anaweza kupata faida ile ile ambayo anaipata kwenye baa. Kwa ufupi, kama ilivyo kwa tabia nyingi zisizofaa, tabia zinazosababisha watu kulewa chakari siyo rahisi kuzibadilisha. Lakini inapojengeka nia, yote yanawezekana.
Ukiangalia yale yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, utagundua kuwa ipo jitihada ya kugeuza jamii ya Watanzania kuwa na tabia tofauti katika masuala kadhaa. Serikali ya Rais John Magufuli imeanza kazi kwa kujaribu kubadilisha tabia tulizozowea zamani, na kujaribu kutufundisha tabia mpya.
Lakini ni wazi kuwa hatua ya pili na ya tatu katika mchakato wa kitabia wa enzi hizi za awamu ya tano zinabadilika. Zamani kwenye hatua ya kwanza kiliibuka kichocheo kilichomfanya mtumishi wa umma aingie hatua ya pili ya kupokea mshahara wake na wa watu wengine kadhaa. Hatua ya tatu ikawa yale manufaa ya mapato kuongezeka kwa kupata mshahara zaidi ya mmoja.
Sasa, falsafa ya Hapa Kazi Tu inaweka msimamo kuwa desturi ya kupokea mshahara zaidi ya mmoja kinyume cha sheria si desturi inayopaswa kuvumiliwa.
Desturi mpya inayojengeka sasa ni ya watumishi kupokea mshahara mmoja, na manufaa mapya yanakuwa kuendelea kuajiriwa na kuepuka kwenda gerezani na kufanya kazi bila malipo.
Mwandishi Charles Duhigg anatahadharisha kwenye utangulizi wa kitabu chake kuwa kubadilisha tabia si jambo rahisi, lakini ni jambo ambalo linawezekana. Na yeye anaonesha njia ya namna ya kufanya hivyo.

CHANZO   CHA   MAARIFA :  GAZETI  LA  JAMHURI , 08  JUNI , 2016.

MUHAMMAD ALI , BONDIA ALIYETIKISA DUNIA



Muhammad Ali (74), bingwa wa zamani wa dunia wa ngumi za uzani wa juu na mmoja kati ya wanamasumbwi bora zaidi duniani, aliyefariki katika Hospitali ya Phoenix Area, Arizona, nchini Marekani mwishoni mwa wiki iliyopita. 

Bondia huyo aliyetamba katika miaka ya 1960 mpaka 1980 alipoamua kujiuzuru, atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa katika mchezo huo. Mwanamichezo huyo wa masumbwi, alijulikana zaidi kwa jina la “The Greatest” Alilazwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na tatizo la upumuaji uliosababishwa na ugonjwa Parkison Disease.
Alizaliwa katika kitongoji cha Cassius Marcellus Clay,Louisville, Kentucky, Januari 17, mwaka 1942. Alikuwa ni kijana wa mtoto wa mchoraji. Akiwa na umri wa miaka 12, aliibiwa baiskeli na aliwaambia maafisa wa polisi atahakikisha kwamba anawapata wezi wake. 

 Enzi za uhai wake alikuwa amevunja rekodi ya kutwaa ubingwa wa dunia mara tatu wa ngumi za Uzani wa Juu. Mwaka 1981 aliamua kustaafu mchezo wa ndondi. Baadaye alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa Parkinson hadi alipofikwa na mauti wiki iliyopita.
Pamoja na kusumbuliwa na ugonjwa huo, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi na maambukizi katika njia ya mkojo. Msemaji wa familia ya bondia huyo, Bob Gunnell alisema kabla ya kufariki kwake alikuwa chini ya uangalizi wa Jopo la Madaktari na kwamba alikuwa anatarajia kutembelea jiji la London lakini alijikuta akisumbuliwa na maradhi hayo.
 
Kilichosababisha kujiunga na mchezo huo
Muhammad Ali hakuwa na nia ya kujiunga na mchezo wa ndondi, bali aliingia huko kwa bahati tu. Akiwa na umri wa miaka 12 akiwa na rafiki zake ndipo baiskeli yake ikaibwa.
Baada ya kugundua kwamba baiskeli yake imeibwa alishauriwa kwenye nyumba ya taasisi ya mafunzo ya Columbia ambako alimkuta Ofisa wa Polisi aliyefahamika kwa jina la Joe Martin aliyekuwa akisimamia mafunzo ya ndondi.
Alipomweleza Ofisa huyo wa Polisi kuhusu tukio la kuibwa kwa baiskeli yake na mtu ambaye hakufahamika alishauriwa kuanza kunoa ngumi zake kwa kujifunza mchezo huo wa ngumi kabla ya kuanza kumsaka mwizi huyo.
Alifanya bidii katika mafunzo hayo ya ndondi na alipofikisha umri wa miaka 18 alikuwa ameshinda medali ya dhahabu, katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika jijini Rome, Italia.
Ali alikuwa akiishi Louisville katika jimbo la Kentucky akijulikana kwa jina Mercellus Cassius Clay Jr kabla ya kubadili dini mwaka 1975 na kuitwa Muhammad Ali akiwa amefikisha umri wa miaka 33.
 
Rekodi yake ulingoni
Alicheza jumla ya mapambano 61, kati ya hayo alishinda 56, huku akishinda mapambano 37 kwa “knock out” na alipigwa katika  mapambano mitano tu.  
Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 22 alivunja rekodi ya kutwaa ubingwa wa ngumi za uzani wa juu, ambayo baadaye ilikuja kuvunjwa na Mike Tyson mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 20. 

Hata hivyo baada ya kutwaa taji la dunia la uzito wa juu mwaka 1967,  alikamatwa na kutupwa jela kwa kosa la usaliti, kwa kukataa kujiunga na Jeshi la Marekani ili kushiriki katika vita vya Vietnam. Ali alivunja rekodi ya kutwaa mataji matatu ya uzito wa juu wa dunia mwaka 1964, 1974 na 1978.
 
Mazishi yake
Mazishi ya Muhammad Ali yatkuwa ni ya wazi katika eneo la makaburi, matayarisho ya mazishi pamoja na zoezi zima la vitafanyika siku ya Ijumaa, nyumbani kwake, Louisville.
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton anatarajiwa kushiriki. Bingwa huyo wa ndondi za uzito wa juu mara tatu wa mmoja wa wanamichezo wa aina yake katika karne ya 20. 
 
Nukuu zake 
“Pepea kama kipepeo, ng’ata kama nyuki. Mikono haiwezi kupiga kitu ambacho macho hayaoni,” Maneno hayo yalikuwa yakirudiwa mara kwa mara kuelezea stairi yake ya kupigana anapokuwa kwenye ringi.
“Nilipigana na mamba, nikapambana na nyangumi, nilikumbatia moto, niliipeleka jela radi, mimi ni mtu mbaya ….Wiki iliyopita niliua mwamba, nikajeruhi jiwe, nilisababisha jiwe likalazwa hospitali. Mimi ni hatari, ninaweza kusababisha dawa zikaugua,” maneno hayo aliyasema huku akicheka alipokuwa anaingia kwenye pambano lake la mwaka 1974, lililochezwa katika ardhi ya Afrika, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kumshinda mpinzani wake George Foreman, katika pambano lililoitwa ‘Rumble in the Jungle’ 

CHANZO  HABARI : GAZETI  LA  JAMHURI ,08  JUNI , 2016