Rafiki yangu mpendwa, mdau wangu
Mtaji umekuwa sababu ambayo wengi wanaitumia kama kikwazo kwao kufanikiwa.
Na wengi wanapozungumzia mtaji, huwa wanaangalia mtaji wa aina moja tu, fedha.
Kuna
mitaji mingine muhimu ambayo mtu anakuwa nayo na anaweza kuitumia
kufanya makubwa kwenye maisha yake, lakini haitambui wala kuitumia.
Anang’ang’ana na mtaji mmoja tu, ambao hata akiupata bado changamoto kwake haziishi.
Leo nakwenda kukushirikisha aina nyingine ya mtaji ambao unapaswa kujijengea na kuulinda ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kabla sijakuambia mtaji huo ni upi, kwanza nikupe taarifa muhimu kuhusu mafanikio, ambazo wengi wamekuwa hawakupi.
MOJA; mafanikio yanataka uweze kufanya maamuzi bora na haraka kuliko wengine. Maamuzi yanawatofautisha sana wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
MBILI; mafanikio yanataka uweze kufanya kazi kwa juhudi kubwa na kwa muda mrefu kuliko wengine. Haijalishi unafanya nini, juhudi zinahitajika sana.
TATU; mafanikio yanakutaka uwe na uvumilivu mkubwa licha ya kupitia magumu na kukatishwa tamaa. Wanaofanikiwa siyo kwamba njia yao inakuwa rahisi, ila wanakuwa wagumu kuliko magumu wanayokutana nayo.
Vitu
hivyo vitatu ni muhimu kuliko kingine chochote kwako kufanikiwa.
Kufanya maamuzi sahihi, kuweka juhudi kuwa na kuwa mvumilivu.
Vyote hivi vitatu ni zao la AFYA.
Na hiyo AFYA ndiyo mtaji muhimu mno kwako kuweza kufanikiwa.
Bila ya afya bora, hakuna makubwa unayoweza kufanya kwenye maisha yako.
Wengi hudhani afya ni kutokuwa na magonjwa, lakini hilo siyo kweli.
Shirika la afya duniani linaeleza afya kama kuwa vizuri kimwili, kiakili, kiroho, kijamii na kiuchumi.
Kwa maana hiyo ya afya, unaweza kuwa huna ugonjwa wowote, lakini bado afya yako ikawa siyo nzuri.
Unaweza kujionea hapa ni kwa nini afya ndiyo mtaji muhimu kwako kufikia mafanikio makubwa, kwa sababu imegusa kila eneo la maisha.
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kujenga afya yako kwenye maeneo haya matano.
( 1 ). MWILI.
Mwili wako ndiyo hekalu la maisha yako, ndiyo gari la kukufikisha kwenye mafanikio yako makubwa.
Bila mwili imara, hutaweza kuweka juhudi za kutosha ili uweze kufanikiwa.
Maana mafanikio yanakutaka uweke juhudi kubwa na kwa muda mrefu.
Jenga afya yako ya mwili kwa kuwa na ulaji mzuri, kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika.
Linda afya yako ya mwili kwa kuepuka magonjwa na tabia hatarishi.
Mwili unapokuwa imara, unaweza kuendesha mapambano ya mafanikio.
( 2 ). AKILI.
Akili
yako ndiyo inayofanya maamuzi, mafanikio yanahitaji sana maamuzi sahihi
kwenye maisha. Hivyo ni muhimu kuijenga afya ya akili ili uweze kufanya
maamuzi bora kwenye maisha yako.
Jenga afya yako ya akili kwa
kuilisha maarifa sahihi na kufanya mazoezi ya kufikiri kwa kina katika
hali mbalimbali. Pia kuwa na muda wa kutafakari mambo yako.
Linda
afya yako ya akili kwa kuepuka habari hasi, vilevi mbalimbali na
mitandao ya kijamii. Vyote hivyo vinadhoofisha akili yako na kuifanya
isiweze kufanya maamuzi bora.
Bila ya maamuzi bora, mafanikio yatakuwa magumu kwako.
( 3 ). ROHO.
Roho
yako ndiyo kichocheo cha wewe kuendelea na safari ya mafanikio hata
pale unapokutana na magumu yanayokatisha tamaa. Kama haupo imara kiroho,
hutaiweza safari ya mafanikio kwa sababu ina magumu na inakatisha sana
tamaa.
Jijengee afya ya kiroho kwa kusali, kufanya tahajudi na kuwa na imani imara.
Linda afya yako ya kiroho kwa kuepuka waliokata tamaa na wasiokuwa na imani, maana mambo hayo huambukizwa kwa urahisi.
( 4 ). UCHUMI.
Uchumi
ni eneo muhimu kinalokupa utulivu wa kuyaendesha maisha yako. Kama
hujui kesho utapata wapi fedha ya kula, akili yako haiwezi kutulia
kwenye mafanikio makubwa unayotaka kufikia.
Hivyo unapaswa kujenga
afya yako ya kiuchumi ili uwe na uhakika wa kuyaendesha maisha yako
wakati unaendelea kupambana na mafanikio.
Kujenga afya yako ya
kiuchumi hakikisha una akiba ya kuweza kuyaendesha maisha yako kwa
angalau miezi sita hata kama utapoteza kipato unachoingiza sasa.
Kulinda
afya yako ya kiuchumi epuka matumizi kuzidi mapato yako. Kwa kila
kipato unachoingiza, tenga sehemu ya kipato hicho ambayo utaweka kama
akiba.
( 5 ). JAMII.
Jamii
ni wale wanaokuzunguka, ambao unawahitaji sana kwenye safari yako ya
mafanikio. Huwezi kufanikiwa peke yako, chochote unachotaka kinatoka kwa
watu wengine.
Jenga afya yako ya kijamii kwa kuboresha mahusiano
yako na wengine, kuwajali na kuweka maslahi yao mbele. Jua utapata
unachotaka kwa kuwapa wengine kile wanachotaka.
Linda afya yako ya
kijamii kwa kuepuka kuwasema wengine vibaya, majungu na kuwadhulumu
wengine. Hata kama unaona unaweza kufanya kwa siri, jua kuna siku mambo
yote yatakuwa hadharani.
Jenga afya yako kwenye maeneo hayo matano na utakuwa moto wa kuotea mbali kwenye safari yako ya mafanikio. Kwani utakuwa na mwili wenye nguvu ya kupambana, akili yenye uwezo wa kufanya maamuzi bora, roho yenye hamasa ya mafanikio, uchumi unaokuweka huru na jamii inayokupa kile unachotaka.
KARIBU UJIUNGE " DARASA ONLINE " na ujifunze jinsi ulivyo na nguvu kubwa ndani yako za kukuwezesha kufanya makubwa mno.
Unaweza
kuwa unajichukulia poa na kuona huwezi kufika kwenye mafanikio makubwa,
lakini kwa kujifunza zaidi kwa undani utaona wazi nguvu zako zilipo na jinsi
ya kuzitumia kufanya makubwa na kufanikiwa. HAKUNA UCHAWI.
Rafiki,
umejifunza hapa jinsi AFYA ilivyo mtaji muhimu kwako kufanikiwa, chukua
hatua sahihi sasa ili kujenga afya imara itakayokuwezesha kufika kwenye
mafanikio makubwa.
Rafiki yako anayekupenda sana,
KOCHA MWL. JAPHET MASATU, DAR ES SALAAM , TANZANIA
Tuwasiliane nami sasa ili nikuunge katika "DARASA ONLINE " kwa kutumia EMAIL YAKO YA GMAIL "
( WhatsApp + 255 716 92 4136 ) / + 255 755 400128