Tunaishi katika zama ambazo watu wanakumbana na matukio mbalimbali na kupitia matukio hayo wanapoteza utulivu mkubwa wa ndani. Utulivu unapopotea ndani ya mtu maisha nayo huanza kuvurugika kabisa. Kufukuzwa kazi, mahusiano yamevunjika, biashara imeanguka, soko limeshuka, magonjwa yamejitokeza matukio kama haya yanapotokea kwa mtu, basi wengi hupata masumbuko ya moyo na wanapoteza ustahimilivu ndani yao.
Falsafa ya Ustoa si kuwa inakuandaa usiwe mtu wa hisia la hasha bali kukusaidia kuwa mtu ambaye hata katika lolote litakalojitokeza uwe imara ndani yako. Ukikosa uimara ndani yako umekosa kitu kikubwa maishani. Maisha hayataacha kutupa changamoto, magumu, matatizo si kutuharibu ndani yetu ila kutupa ukweli wa maisha kuwa maisha hayatakosa magumu toka kuzaliwa kwetu hadi kufa kwetu.
Magumu ni vikwazo ambavyo unaona vinatokea njiani au katika safari ya maisha. Kinapojitokeza kikwazo tu basi eneo moja linalojeruhika haraka ni hisia zetu kuhusu yale yalotokea. Kinachotuumiza wakati wote kwa matukio yoyote ambayo hujitokeza ni tafsiri ambazo huwa tunazitoa kuhusu yalotutokea. Tafsiri yako kuhusu mambo ndio inayokuumiza siku zote na inakutengenezea ugumu katika mambo.
Marcus Aurelius anasema “The first rule is to keep an untroubled spirit. The second is to look things in the face and know them for what they are.” Hii ikiwa na maana “Sheria ya Kwanza ni Kutoruhusu Roho Kusumbuliwa. Pili ni Kuangalia Mambo Jinsi yenyewe Yalivyo – Sheria ya kwanza ni kuzuia roho kusumbuliwa na pili kuyaacha mambo jinsi yenyewe yalivyo. Hizi sheria mbili zinaweza kukusaidia kukabiliana na magumu ambayo utayapitia katika safari ya maisha.
Chochote kile ambacho kitakutokea uwe umetarajia au hujatarajia kitakupima juu ya uimara wako ndani. Ikiwa jambo litajitokeza na huna uwezo wa kuhimili ndani basi litakuharibu na kukuyumbisha. Watu wote ambao tunawaita hodari si kuwa mambo wanayokutana nayo ni mepesi hapana ila wana nguvu ya kustahimili toka ndani wakijua lilijitokeza limekuwa hivyo na wanabadili namna la kuliona.
Pili kubali mambo yanavyotokea kuwa imekuwa hivyo yametokea. Ondoa tafsiri yako kuhusu chochote kinachotokea maana kuweka tafsiri yako ni kuandaa mazingira ya kujiumiza na huo ndo mwanzo wa masumbuko makubwa katika maisha. Usisumbuke na mambo yanavyotokea ila imarishwa katika kuwa na utulivu kwa lolote ambalo litatokea. Usiyumbishwe na chochote au kushangazwa na chochote maana maisha yatakutana na ugumu ambao hautakoma hadi tunahitimisha ukomo wa maisha yetu.
Ili utunze utulivu ndani yako basi tambua kuwa njia ya maisha itakumbana na mfululizo wa magumu yasokoma. Ukweli huu unapokubali unakusaidia kuwa hodari na shujaa kuwa hili ambalo limejitokeza au litakalojitokeza limepaswa kuwepo na si kulaumu ila kuwa na ustahimilivu na nguvu ya kufurahia maisha. Maisha licha yatabakia na ugumu ila namna unavyoona mambo na kuyatafsiri itakupa wepesi wa mambo mengi na matukio ya kimaisha yanayoendelea kutokea. Tunayoyapitia zama hizi walowahi kuishi nao walipitia na njia ya maisha imeendelea kuwa na magumu tofauti tofauti kulingana na nyakati.